Kutia Wudhuu Bila Ya Kuvaa Nguo Inafaa?

 

SWALI: 

Assalam 'alaikum

Asanteni sana kwanza kwa kazi hii tukufu munayoifanya kuelemisha ummah wa kiislam. Many of us learned a lot from this site and still learning. Allah subhanah wataala akujaalieni na kila la kheri waendeshaji wa alhidaaya.

Halafu suali langu la leo ni kuhusu kutiya udhu. Naomba kujuwa mfano mtu unakoga wakatikaribu na sala. Jee inafaa pale pale upo kwenye shower bila ya nguo yeyote kujitiya udhu au lazma ushuke uvae nguo au kujifunika halafu ndio utiye udhu wako?

Japokuwa nimetafuta kutumiya service yenu ya search kabla yakutuma hili suali langu bila ya mafanikio. Natanguliza radhi ikiwa suali hili tayari lipo na mimi sikuliona.

WASALAAM ALAYKUM WARAHMATULLAH WABARAKATUH.

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Tunakushukuru kujua kwamba umejitahidi kwanza kutafuta jibu la Swali lako na pia tumefurahi kujua kwamba unajifunza mengi kutoka Alhidaaya. 

Vile vile tunashukuru sana kwa du'aa zako nzuri ambazo tunaomba inshaAllaah zitakabaliwe ili kutuwezesha kuendeleza hizi kazi nyingi  mno na ngumu. Tunamuomba Allaah Azidi kutuelimisha na kuweza kukunufaisheni.

Jibu la swali lako ungeliweza kulipata katika majibu yafuatayo, hata hivyo kifupi ni kwamba hakuna ubaya kutia wudhuu wakati unaoga, au ikiwa hukuvaa nguvo zozote, kwani hakuna dalili yoyote inayokataza jambo hilo. Hukumu kama hizo zisemwazo ni kujitia mashakani tu katika kutekeleza ibada za dini yetu,  kwani hakika ingelikuwa vigumu sana mtu asiweze kutia wudhuu hadi ajifunike. Hivyo kutokukatazwa kwake ni kheri na Rahma kwetu kutufanyia ibada zetu wepesi.

Vilevile mafunzo ya Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ya kuoga janaba, yanatuonyesha kuwa mtu anatia wudhuu wakati anaoga, na inajulikana kuwa mtu huoga bila nguo, kwa hiyo, hiyo ni dalili tosha kuwa hilo ni jambo linaloruhusika kwani hatukuona kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kutuelekeza kuwa tunatakiwa tena tuchukue wudhuu mara ya pili tukiwa na nguo baada ya ule tuliochukua wakati wa kuoga kama alivyofundisha. 

Hivyo, ukichukua wudhuu wako wakati umevaa nguo zako ni vizuri, lakini kukibidi kutokuwa na nguo wakati wa wudhuu hakuna tatizo na wala kuvaa nguo si sharti la kuchukua wudhuu.

Melezo zaidi ya yanayovunja wudhuu utapata katika viungo vifuatavyo:

Wudhuu Unavunika Ikiwa Hukujifunika Vizuri?

Na Allah Anajua zaidi

Share