Zamu Ya Mke Wa Pili Aliyesafiri, Zilipwe Akirudi?

 

SWALI:

 

Shukurani zote anastahiki Allah, Mola aloumba kila kitu katika ulimwengu huu, sala na salam zimshukie mpenzi wetu Mtume Muhammad (SAW) na ahli zake, nasi inshallah atujaalie miongoni mwa waja wema na wenye kusamehewa makosa yetu.

Suala langu ni hili, mume akiwa na mke zaidi ya mmoja, na mkewe mmoja akawa amesafiri, kipindi chote hicho akawa hapiti katika nyumba yake ambayo mkewe hayupo, ijapokuwa alipoondoka hawajakubaliana utaratibu gani utakaotumika katika kipindi chote ambacho mkewe mmoja hayupo. Hivyo akawa anatumia siku zake zote kwa wake zake waliokuwepo hapo, suala je atakapo rudi huyo mume atakuwa anawajibu gani kwa mkewe huyo?

Ahsante, nashukuru kwa kupata nafasi ya kuuliza suala langu. 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako. Uislamu umeweka mpango madhubuti katika masuala yake yote, yakiwa ni ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kadhalika. Ikiwa mke mmoja amesafiri kwa ruhusa aliyopewa na mume bila mapatano yoyote baina yao kwa ugao wa siku baina yao atakaporudi wataanzwa kugawiwa siku upya kama zamani bila ya kulipwa zile siku alipokuwa hayupo mjini.

Hii ni kuwa hatujapata kuona kuwa wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliporudi katika safari zake alikuwa analipiza siku kwa wake ambao hakuwachukua katika safari hiyo. Inafahamika kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa anafanya kura wakati anaposafiri na yule mwenye kupata kura alikuwa akichukuliwa. Aliporudi mjini kwake, Madiynah zamu zilikuwa zikirudi tena kama kawaida.

Lau wangekuwa wamekubaliana hivyo kabla ya safari basi ingekuwa ni lazima kwa mume kufuata mapatano hayo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share