Mwanamme Aliyebaka Mwanamke Na Mwanamme Nini Hukmu Yake?

 

SWALI:

 

Ni nini hukmu ya mwanamme ambaye

1) Amembaka mwanamke

2) Amembaka mwanamme? 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu ovu hilo. Ni ajabu kuona au kusikia maovu haya ya kubaka wanawake na kwa sasa hata wanaume yamekithiri katika jamii yetu. Hakika ilikuwa yatakikana sisi ndio tuwe mbali sana na maovu haya. Kwa wakati huu maovu haya yamekuwa ni mema na mema yamekuwa maovu. Mwenye kufanya mema anaonekana kuwa ni mshamba, mjinga na hastahiki kuitwa msomi hata akiwa ni msomi.

Hatuna budi kuibadilisha hali hii na kurudi katika machimbuko yetu ya Dini ili tuweze kuongoza ulimwengu wote kwa maadili mema tuliyofunzwa na Dini yetu tukufu. Hakuna jambo zuri ila Uislamu umehimiza na kulipatia kipaumbele na hakuna ovu isipokuwa Uislamu umelipiga vita kwa kiasi kikubwa. Kufanya jema ni katika maslahi yetu na pia kuacha baya ni hivyo hivyo.

Maswali yako mawili yameegemea katika zinaa na liwati lakini ya kutumia mabavu. Haya maovu mawili ni janga na balaa kwa wanadamu mbali na kuwa tunapuuza hilo. Utekelezaji wa maovu haya unaleta magonjwa kama ukimwi, kisonono na kadhalika, huleta mmomonyoko wa maadili, madhara ya kinafsi na kijamii na pia kuleta watoto wasio na nasaba yoyote ile.

Ni wazi kuwa hukumu ya Uislamu kuhusu zinaa ni haraam. Hiyo ni kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

 'Wala usikaribie zinaa' (17: 32).

Pia Aliyetukuka Ametuelezea sifa za waumini wa kweli pale Aliposema: '…wala hawazini na mwenye kufanya hivyo anapata madhambi' (25: 68).

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 'Hazini mzinifu wakati anapozini na hali ni Muumini' (al-Bukhaariy na Muslim).

Ama kuhusu adhabu ya zinaa iko wazi kabisa ya kubaka itakuwa ni zaidi ya hiyo kwa yale madhara yanayomfikia aliyebakwa. Zinaa ya kawaida ikiwa aliyefanya hajaoa atapigwa mijeledi mia moja (Tazama Qur-aan 24: 2) na kutolewa mjini kwa mwaka mmoja. Na Imaam au Khaliyfah anaweza kumpatia adhabu ya ziada (ta'aziyr) kama anavyoona ni munasibu na sawa. Na ikiwa atatumia nguvu kama kutumia kisu, panga au bunduki ataingia katika Aayah ifuatayo:

Basi malipo ya wale wanaompiga vita Allaah na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuawa, au kusulubiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa” (5: 33).

Ama akiwa ameoa basi anafaa apigwe mawe hadi kufa. Hii ni kwa kauli ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

'Si halali damu ya Muislamu ila kwa moja katika mambo matatu: Mzinifu mwenye mke (au mwenye mume), nafsi kwa nafsi na mwenye kuacha Dini yake, aliyejitenga na Waislamu' (al-Bukhaariy na Muslim).  

Liwati nayo imeharamishwa na Uislamu kwa uwazi kabisa. Allaah Aliyetukuka Anasema:

'Mnawaendea wanaume katika walimwengu na munawaacha wale Alikuumbieni Mola wenu Mlezi katika wake zenu? Hakika nyinyi ni kaumu mlio maadui' (26: 165 – 166).

Na amesema Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 'Amelaaniwa mwenye kufanya kitendo cha kaumu Luutw; Amelaaniwa mwenye kufanya kitendo cha kaumu Luutw; Amelaaniwa mwenye kufanya kitendo cha kaumu Luutw Amelaaniwa mwenye kufanya kitendo cha kaumu Luutw Amelaaniwa mwenye kufanya kitendo cha kaumu Luutw' (al-Haakim).

Pia:

'Watu aina nne wanapambazuka na kuingia na usiku wakiwa wameghadhibikiwa na Allaah'. Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) akasema: 'Ni nani hao ewe Mtume wa Allaah?' Akasema: 'Wanaume wenye kujifananisha na wanawake; wanawake wenye kujifananisha na wanaume; wenye kuwajia wanyama (kufanya kitendo cha ndoa na mnyama; na wenye kuwajia wanaume' (atw-Twabaraaniy na al-Bayhaqiy).

Ama adhabu haina utata wowote kwani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

'Mnayemuona akifanya amali ya kaumu ya watu wa Luutw, muueni anayefanya na anayefanywa' (Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

Pengine hapa kutakuja utata kwa kuwa mwenye kufanywa hakufanya kitendo hicho kwa hiyari bali ametenzwa nguvu, itakuwaje? Suala hili linajibiwa na kauli ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale aliposema:

'Hakika Allaah Amenisamehea Ummah wangu kukosea kwao, kusahau kwao na waliyotendeshwa nguvu' (Ibn Maajah, al-Bayhaqiy na wengineo).

Hivyo, kwa mujibu wa kauli hii aliyefanywa kwa nguvu anasamehewa na sheria.

Na Allaah Anajua zaidi

Share