Mume Anawasiliana Na Wanawake Kwa Maandishi Ya Mapenzi Kwa Njia Ya Simu Ya Mkononi – Nikimkataza Ananiambia Niende Kwetu

 

SWALI:

A/alaykum, mimi ni binti nilieolewa huku ulaya, nimejaaliwa mtoto mmoja, lakini ndoa yetu haina raha ndani yake, na tatizo kuu ni huyu mume wangu, tangu mimi kuja nchi hii amekua akiwasiliana na wasichana kwa njia ya simu (txt msgs) na hizo msg zimejaa mahaba ndani yake, nimeshamuuliza ni kina nani, nae husema ni rafiki ambao hawezi kuachana kuwasilana nao, jambo hili hunikera sana, kwani huona ni kinyume cha sharia, na pia humwambia kua ni haram kuwa na rafiki wa kike hasa ikiwa yupo kwenye ndoa, lakini huona mimi ni mpuuzi na huona mimi na mtaabisha hata imefikia wakati kuniambia mimi niende kwetu kwa maudhiko ya mara kwa mara, jee nifanye nini kwa sababu mimi nimetoa uaminifu kwake.

W/ alaykumJIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati dada yetu kwa swali lako zuri. Hakika ni kuwa hili ni tatizo sugu katika jamii yetu ya Waislamu. Maswali kama ya matatizo ya kindoa yamekua yakikariri kila uchao. Wanandoa wamekua hawana raha katika ndoa zao mbali na kuwa tumearifiwa na Aliyetukuka kuwa ndoa ni rehema na mapenzi. Kukosekana kwa mapenzi na huruma baina ya wanandoa kunamaanisha kuwa sisi tuna matatizo makubwa hivyo kupata mitihani hiyo.

Tatizo linaanza katika malezi majumbani mwetu na kukosa kuchagua mke au mume aliyeshika Dini. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea sifa za kuangalia wakati unaposa au kuposwa lakini mara nyingi huwa tunatazama sifa zilizokatazwa. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatueleza yafuatayo kuhusu kuposa: 'Mwanamke huolewa kwa moja kati ya sababu nne: Mali yake; nasaba yake; uzuri wake na Dini yake. Chagua mwenye Dini uokoke' (al-Bukhaariy na Muslim).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amewausia wazazi: 'Anapokujieni mnayemridhia Dini na maadili yake muozesheni kwani mkitofanya hivyo kutakuwa na fitina katika ardhi na ufisadi mkubwa' (at-Tirmidhiy).

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuonya tena: 'Mwenye kumuoa mwanamke kwa ajili ya utukufu wake, Allaah Hamzidishii ila udhalilifu; na mwenye kumuoa kwa sababu ya mali Allaah Hamzidishii ila ufukara; na mwenye kumuoa kwa ajili ya nasaba yake, Allaah Hamzidishii ila unyonge; na mwenye kumuoa mwanamke hataki kwake ila kuinamisha macho yake, kuilinda tupu yake au kuunganisha kizazi, Allaah Atambarikia kwake na Atambariki (mwanamke) kwake' (atw-Twabaraaniy).

Huu ni mfumo mzuri wenye kuwasaidia wanandoa pamoja na familia zao na jamii kwa jumla ili kufanikisha zoezi hili. Kuacha mfumo huu ni kuhasirika hapa duniani na kesho Akhera.

Wazazi wanatakiwa watumie busara zao kumuelekeza binti yao katika kheri inapokuja sio kutazama mali au nasaba. Na binti naye pia anafaa atazame zile sifa zilizotajwa wala asiburuzwe katika shari badala ya kheri. Kukosekana hayo ndio tunaibuka na shida moja baada ya nyingine. Watu wa mke kumchunguza mume inajuzu na kinyume chake ili wasiingie katika matatizio na tabu baadaye kwa kukosa kumfahamu atakayeishi naye.

Kulingana na maelezo ya muulizaji inaonyesha kama hayo hayakufanyika ndio unakuja gundua kumbe mume wangu ana wasichana ambao anawasiliana naye. Uislamu umekataza jinsia mbili kuwasiliana kama huyo mwanamme ameoa au laa. Hata hivyo, kwa aliyeoa akifanya kosa hilo madhambi yake huwa ni makubwa zaidi.

Kabla hatujakupatia nasaha zetu ni vyema kuangazia juu ya ibara yako uliyosema: 'Hata imefikia wakati kuniambia mimi niende kwetu kwa maudhiko ya mara kwa mara'. Hii ibara ina utata mkubwa kwani amali zote zinategemea nia ya mwenye kufanya. Je, kukuambia kwenda kwenu ni kuwa tayari amekupatia talaka au vipi? Ikiwa nia yake ni talaka itakuwa wewe si mke wake na kwa sababu baada ya kusema hayo amefanya nawe kitendo cha ndoa atakuwa amekurudia. Hautajapita wakati amekuambia tena bila kujali ile athari inayopatikana kwa maneno hayo.

Ama nasaha zetu kwako ni kuwa tunakuomba ufanye yafuatayo, huenda kwayo ukapata ufumbuzi wa tatizo hilo ulilonalo. Nazo ni kama zifuatazo:

  1. Awali ya yote unatakiwa uzungumze naye kinaganaga maana hasa ya ibara 'nenda kwenu'. Je, hii ameimanisha kuwa ni talaka au ni vipi?

  2. Ikiwa hakumaanisha talaka, anataka muishi namna gani kama wanandoa mnaosikilizana. Je, mnataka muishi kwa masikilizano mazuri au katika mavurugano? Kama wanandoa mliokomaa kiakili ni lazima mzungumze kwa njia nzuri na ya busara ili mtatue tatizo hilo wala msirudie tena.

  3. Ikiwa katika mazungumzo yenu hamkuweza kufikia suluhisho lolote basi inabidi muitishe kikao ambacho wewe na mumeo mtakuwepo. Mbali na nyinyi kunatakiwa kuwepo kwa mwakilishi au wawakilishi wa upande wako na wake ili msuluhishe mzozo huo mara moja usiwe ni wenye kurudi tena katika maisha yenu. Katika mkutano huo inatakiwa kila mmoja awe wazi ili kupatikane ufumbuzi baina yenu.

  4. Ikiwa hakukupatikana ufumbuzi wowote unatakiwa upeleke mashitaka yako kwa Qaadhi ikiwa wapo huko, na ikiwa hawapo basi uende kwa Shaykh mwenye kuaminika karibu nanyi ambaye atasikiliza kesi yenu na kuwatolea suluhisho muafaka baina yenu kulingana na sheria za Kiislamu.

Katika kufikia upatanishi huu ni lazima uwe na subira na uvumilivu mkuu ili muweze kupata suluhisho. Hakika kufanya kwako huko hakutapotea bure bali utapata thawabu kubwa mbele ya Allaah Aliyetukuka.

Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupatie tawfiki na Aidumishe ndoa yenu na Amuondolee mumeo tatizo hili alilonalo.

Na Allaah Anajua zaidi

Share