Ameishi Na Mume Zaidi Ya Miaka 20, Ameoa Mke Mwingine Hakuna Maelewano Tena, Hatimizi Haki Ya Matumizi

SWALI:

 

Assalaam Aleykum,

Mimi nina mume kwa muda wa zaidi ya miaka 20, na kwa kipindi cha zaidi ya miaka 10 tumekuwa ni watu wenye machafuko na nimeshapeleka malalamiko yangu miaka mingi tu lakini bado dharau, jeuri na kashfa zinaniandama dhidi yangu pamoja na familia yangu, na nimeshadai talaka kwa vipindi tofauti, na jawabu kutoka kwa mume anasema eti niwatume watu wangu au niende korti ikiwa nataka talaka. Kipindi kirefu tumekuwa tukiishi miji mbali mbali na yeye mwenzangu huko aliko ameshaoa, mimi nipo na watoto wote na ndie mshughulikiaji mkuu wa watoto kwa mambo yote. Ukidai chochote huwa anasema yeye hana uwezo cha kushangaza zaidi kuwa hata hiyo simu anasema yeye hana pesa za kunipigia


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kutotimiza mahitaji yako kama mke wake.

Hakika ni kuwa dharau ya wanaume mara nyingi inatokea kwa kuwa wanawake hawajui majukumu yao wala haki zao. Tatizo kubwa zaidi ya ndoa zetu ni kuwa mke ameolewa na mume asiyefuata Dini. Hivyo, kwa kukosa kufuata maagizo ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika uchaguzi wa mume, mke anaingia matatizoni.

 

Matumizi ya nyumbani ni wajibu kabisa wa mume kwa hali yoyote ile. Hata hivyo, kwa ulaini wa akina mama, huwa wanadhulumiwa na waume na huwa hawataki kuchukua hatua za kisheria ili kupata haki zao. Kwa hiyo, dada yetu katika hali uliyo nayo inatakiwa ufanye yafuatayo ili kuweza kusaidika:

 

1.     Kuweza kuitisha kikao baina yako, mumeo, wazazi wako na wazazi wake. Ikiwa wazazi hawapo itabidi mtafute wawakilishi wa kuweza kuleta suluhu na upatanishi baina yenu au mume atoe talaka ili asikufunge wewe kwa ndoa ambayo ni ya dhuluma na ambayo yeye mwenyewe haitaki.

 

2.     Ikiwa hakukupatikana suluhu ya aina yoyote ile itabidi uende ukashitaki kwa Qaadhi na wala usiwe na huruma. Ni huruma yenu ndiyo inayowafanya wanaume wengi wawasumbue na kuwadhulumu wanawake huku wakijua kuwa hakuna chochote wanawake wanachoweza kufanya. Ni muhimu uweke mfano ambao mume huyo au mwengine hatothubutu kufanya tena baada ya hiyo. Ikiwa upo sehemu ambayo hakuna Qaadhi basi inatakiwa uende kwa wenye elimu (Mashaykh) wenye kusifika kwa uchaji Mngu, elimu na uadilifu ili awasikilize.

 

 

Bonyeza viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi:

 

Talaka Tatu Pamoja Inakubalika? Mume Hatimizi Zamu Kisha Ametoa Talaka Mara Tatu Kwa Pamoja

 

Mume Hana Bashasha Hatimizi Wajib Wake

 

Mume Wangu Ameoa Mke Wa Pili Ananidhulumu

 

Haki Za Mke Mkubwa Na Mke Mdogo

 

Tunakutakia kila la kheri katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo lako hilo.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share