Mume Hakufuata Taratibu Za Talaka

 

SWALI:

Assalam Alaykum, tafadhali nataka unijulishe kama naitafsir sawa aya ya 1 na ya 2 katika sura talaq. Nifahamuvyo mimi ikiwa mume hakufatia utaratibu alivyoelezewa Moh'd {saw} basi huwa hakuna talaq ilopita hata ikiwa mume ameandika, kwa sababu hakufata maagizo yake, je niko sawa? Naona itakuwa ni kama swala bila udhu huwa haifai, mambo yote yako na utaratibu wake ndio litimie, je hili la talaq halina? Ikitamkwa tu au kuandikwa tu yapita, lakini tukirudi kwa mengine huwa mapaka ufatie utaratibu fulani kama swala na udhu, na mengineo. Tafadhali tufahamishe tupate fata njia yahaq. Shukran



  

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunapenda kukupa nasaha kwamba haifai kuita hivyo jina la Mtume wetu (Swalla Allaahu 'alayhi wa alihi wa sallam) kama ulivyoandika (Moh'd),  na haifai kumkatisha na kumfupishia jina lake kama tunavyofanyiana sisi au kukatana majina na kuitana majina ya kipuuzi. Inapasa tulitamke na kuliandika ipasavyo yaani 'Muhammad'

 

Pia,  kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta’ala) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Mtume. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea na kivivu.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka. Hakika ni kuwa ipo tofauti baina ya talaka ya Bid'ah na kuswali bila wudhuu. Sababu kubwa ni kuwa katika Swalah, Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema wazi kuwa hakuna Swalah kwa mtu ambaye hana wudhuu. Ama katika talaka tunampata Ibn 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhuma) aliyemtaliki mkewe akiwa katika ada ya mwezi. Talaka hiyo iliyotolewa ikahesabiwa kuwa ni talaka lakini akawa ni mkosa.

Kwa hivyo, mwanamme akitoa talaka wakati mkewe yu katika hedhi yake au twahara aliyostarehe naye mume atakuwa amekosa na anapata dhambi lakini talaka itakuwa imepita na kuhesabiwa kisheria. Twatumai kuwa hilo limeeleweka inshaAllaah.

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share