004-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Sababu Za Kuandika Kitabu Hiki

 

Sababu Za Kuandika Kitabu Hiki Na Baadhi Ya Vipengele Vyake

 

 

Kwa vile sijapata kuona kitabu chenye maarifa mengi kuhusu maudhui hii, nimehisi imeniwajibikia kutoa kitabu ambacho kitakusanya sifa nyingi za Swalah ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa ajili ya manufaa ya ndugu zangu Waislamu wapendao kufuata uongofu wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katika ibada zao, hadi iwe wepesi kwa yeyote mwenye kumpenda kweli  Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aweze kutumia kitabu hiki kutimiza amri yake: ((Swalini Kama Mlivyoniona nikiswali)).

 

Hivyo nikaianza kazi hii ngumu, na kufanya utafiti wa Hadiyth zinazohusika kutoka vyanzo mbali mbali za Hadiyth hadi kitabu hiki kilichokuwa sasa mikononi mwako kuwa ni matokeo yake yote. Nikajiwekea masharti nafsini mwangu kwamba nitaziweka Hadiyth zilizokuwa na isnaad Swahiyh pekee kutokana na kanuni za msingi na sheria ya Sayansi ya Hadiyth. Nimepuuza Hadiyth yoyote ambayo imetegemewa na msimulizi asiyejulikana au dhaifu ikiwa imehusianina na maelekezo ya nje, adhkhaar, ubora n.k. wa Swalah. Hii ni kwa sababu naamini kwamba Hadiyth Swahiyh[1] zinatosheleza, na hakuna haja ya zilizo dhaifu kwani zilizo dhaifu hazizidishi kitu isipokuwa dhana (makisio, mashaka) na makisio yasiyo sahihi ni kama Anavyosema Allaah (سبحانه و تعالى):

 

  وَإِنَّ الظَّنَّ لَا يُغْنِي مِنَ الْحَقِّ شَيْئًا

 

((Na dhana haisaidii chochote mbele ya haki))[2]

 

Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kasema: ((Tahadharini na dhana kwani dhana ni kauli ya uongo))[3]

 

Kwa hiyo hatuwezi kumuabudu Allaah kwa kufuata Hadiyth zisizo Swahiyh, bali Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ametukataza akisema: ((Jiepusheni na kusema yanayonihusu isipokuwa muyajuayo))[4]. Kwa vile ametukaza kusimulia masimulizi dhaifu, basi pia haipasi kuzitekeleza.

 

Nimekigawa hiki kitabu katika sehemu mbili; kubwa na ndogo, matini kuu na matini ya kisaidizi/matini ndogo.

 

Matini kuu imejumuisha matini ya Hadiyth au ibara ilivyochukuliwa humo, pamoja na maneno yanayolingana kuunga pamoja ili kukifanya kitabu chepesi tokea mwanzo hadi mwisho. Nimekuwa makini kuibakisha matini ya kila Hadiyth kama ilivyopatikana katika vitabu vya Sunnah; ambako Hadiyth ilikuwa na meneno tofauti na nimechagua maelezo yaliyo bora kabisa yanayowafikiana na ufasaha, wepesi n.k.. Lakini nimekusanya maneno mengine pamoja; hivyo: "(katika usemi kadha na kadhaa…..)" au "(katika usimulizi kadhaa na kadhaa …)". Sikumtaja Swahaba aliyesimulia Hadiyth ila kwa nadra tu nimefanya hivyo, wala sikumtaja Imaam gani wa Hadiyth aliyekusanya Hadiyth, ili kufanya wepesi usomaji na marejeo.

 

Ama matini ya kisaidizi/ndogo ni maelezo kutokana na matini kuu. Humo nimefuatilia Hadiyth kutoka asili yake nikifumbua maelezo mbali mbali na njia za usimulizi. Pamoja nayo, nimetoa maelezo katika isnaad zao na usimulizi unaotilia nguvu, pamoja na tanbihi Swahiyh na zenye kutezwa kwa wasimulizi, ikiwa ni Swahiyh au dhaifu kutokana na hukumu za Sayansi ya Hadiyth. Aghlabu njia ya usimulizi moja huwa na nyongeza ya maneno ambayo hayapatikani katika njia nyingine, hivyo nimezitia hizi katika Hadiyth ya asili zilizotajwa katika matini kuu kila ilipowezekana bila ya kuharibu ufasaha, nikiweka nyongeza katika mabano ya mraba […]. bila ya kutaja chanzo gani kilichonacho nyongeza hiyo. Hii imefanywa ikiwa Hadiyth asili yake imetoka kwa Swahaba mmoja, au sivyo nimeitoa peke yake; mfano katika Du'aa za kufungulia n.k. Nyongeza hii ya maneno ziada ni manufaa makubwa ambayo hutoyapata katika vitavu vingi – Sifa njema zote ni za Allaah Ambaye Kwa Neema Zake Mema hutimia.

 

Kisha, nikataja katika matini ya kisaidizi/matini ndogo Madhehebu ya Maulamaa kuhusu Hadiyth tulizozitoa na dalili zake kila moja pamoja na hoja zake na kubainisha uzito wake na udhaifu wake. Kisha tukachagua rai iliyo sahihi ambayo tumeiweka katika matini kuu. Pia katika matini ya kisaidizi tumetoa baadhi ya mas-ala ambayo hakuna matini katika Sunnah, lakini imehitaji Ijtihaad, na haikuja chini ya maudhui ya kitabu hiki.

 

Kwa vile kuchapishwa kitabu kuwekwa matini kuu na matini ya kisaidizi haiwezekani sasa kwa sababu mbali mbali, tumeamua kukichapisha kikiwa na matini kuu ya kitabu (pamoja na tanbihi fupi) kwa uwezo wa Allaah, na kukiita 'Swiffatus-Swalat 'An-Nabiyy (صلى الله عليه وآله وسلم)Min At-Takbiyr ilaa At-Tasliym Kaannaka Taraaha' (Sifa ya Swalah ya  Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) Kuanzia Takbiyra Ya Mwanzo hadi Kumalizika kwa Salaam Kama Kwamba Unaiona)"

 

 

Namuomba Allaah Ajaalie kazi hii iwe khaswa kwa ajili Yake, na iwasaidie ndugu zangu katika Iymaan kunufaika nayo kwani Yeye ni Mwenye Kusikia Aliye Karibu.

 

 

 

 

 

[1] Istilahi ya 'Hadiyth Swahiyh' inajumuisha Swahiyh na Hasan mbele ya macho ya Muhaddithiyn, ikiwa ni Hadiyth Swahiyh lidhaatihi au Swahiyh lighayrihi, au Hasan lidhaatihi au Hasan lighayrihi.

 

[2] An-Najm: 53: 28

[3] Al-Bukhaariy Na Muslim

[4] Swahiyh – imekusanywa na At-Tirmidhiy, Ahmad na Ibn Abi Shaybah.

 

 

 


Share