Tukio La Karatasi

 

Tukio La Karatasi

 

Tukio la ‘Karatasi’ (Qirtwaas) lililonakiliwa katika vitabu vya Al-Bukhaariy na Muslim kuwa siku tatu kabla ya kufariki Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitamka; “Nipeni kalamu na wino ili niwaandikie maelezo yatakayowafanya watu wasipotee” (Nipeni kalamu na wino niwaandikie usia ambao utawafanya watu wasipotee), halina ukweli kama ambavyo Mashia wanavyolielezea na kuitafsiri. Kutokana na kauli hii inadaiwa kuwa ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) alihutubia watu na kusema kuwa “Mtume yupo katika maumivu makali, Qur-aan kama muongozo unatosha kwa watu. Baadhi ya watu wakasema Mtume amepoteza fahamu. Ipo kauli pia isemayo maneno haya yamesemwa na ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) Khalifa wa pili.

 

 

Moja ya Hadiyth hizo zimo katika kitabu cha al-Bukhaariy juzuu ya kwanza Hadiyth namba 114 katika ukurasa wa 86 tafsiri ya kiarabu, isemavyo hivi: Amesimulia ‘Ubaydullaah bin Abdillaah, kuwa Ibn ‘Abbaas amesema:

 

“Hali ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ilipokuwa mbaya alisema:“Nileteeni karatasi ya kuandikia tamko litalowapelekea kutopotea”. Lakini ‘Umar (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema; “Mtume unaumwa sana na tuna kitabu cha Allaah Ambacho kinatosheleza. Lakini Maswahaba wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakatofautiana juu ya jambo hili. Kutokana na zogo hili Mtume akawaambia; “Ondokeni (na niacheni peke yangu) sio sahihi mbishane mbele yangu.

Ibn ‘Abbaas akatoka nje na kusema: Imekuwa bahati mbaya na msiba mkubwa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amezuiwa kuandika tamko kwa sababu ya kutokubaliana kwao na makelele yao.” 

Mashia wanasema kuwa hiyo ndiyo siku ambayo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alitaka kumchagua ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu)  awe ndiye Imam wa Waislam baada ya kufa kwake. Wakazua mengi kutokana na yaliyotokea siku hiyo wakijaribu kuuthibitisha uongo wao huo.

Wanasema hivi:

“Maswahaba wote walikuwepo nyumbani kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya Alkhamiys, siku tatu kabla ya kufariki kwake, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

“Leteni kidawati na kalamu nikuandikieni maneno yatakayokukingeni na upotovu baada yangu”.

‘Umar akasema: “Mtume wa Allaah anasema bila fahamu (hii ni kauli ya Mashia). Munayo Qur-aan, kinatutosha kitabu cha Allaah”.

Maswahaba wakaasi amri, na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akuwafukuza nyumbani kwake bila ya kuwaandikia chochote”.

Katika vitabu vyao, wanakielezea kisa hiki kwa ufupi na kwa kubadilisha badilisha maneno.

Katika vitabu vingine wanasema:

Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhuma) alisema:

“Siku ya Alkhamiys, na kipi kitakachokujulisha hiyo siku ya Alkhamiys, siku hiyo maumivu yalimzidi Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akasema:“Ngojeni nikuandikieni maandishi, hamtopotoka baada yake”. ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu)  akasema:“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasema bila fahamu, na tunayo Qur-aan, kinatutosha kitabu cha Allaah.”

Wakakhtilafiana na watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kukasirikiana, na kwamba wapo waliokuwa wakisema:

“Jisogezeni ili aandike yale ambayo baada yake hamtapotea tena”Na wapo waliokuwa wakisema yale aliyosema ‘Umar. Na mazungumzo na khitilafu zilipozidi, Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

“Ondokeni karibu yangu”.

Ibn ‘Abbaas akawa anasema: “Msiba wa kweli hasa ni kule Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoweza kuwaandikia maandishi yale kutokana na kukhitilafiana kwao”.

Mashia wanajaribu kulifasiri tukio hili kama kwamba jambo jipya litakalokata mzizi wa fitna baina ya Waislam ambalo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku hiyo alitaka kuwaandikia Maswahaba (Radhiya Allaahu anhum), ni usia wa kumchagua ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Khalifa wa Waislam baada ya kufa kwake na kwamba ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyajua hayo, ndio maana akawaambia watu kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajui nini anasema na kwamba tunayo Qur-aan inatutosha.

 

 

Zingatio

Kutokana na Hadiyth hii ni dhahiri kuwa Ibn ‘Abbaas ameshuhudia tukio hili na akatoka nje na kusema kauli hii. “Ukweli sio huu kwa sababu Ibn ‘Abbaas alikuwa anatamka kauli hii alipokuwa anasimulia Hadiyth hii, lakini yeye binafsi hakushuhudia tukio hili.” Kwa maelezo zaidi juu ya hili rejea Fat-hul-Baariy juzuu ya 1, ukurasa wa 220.

Atakayeichunguza Hadiyth hii kwa njia zake zote zilizopokelewa ataona kuwa Mashia wanajaribu kuchanganya maneno na kuacha maneno.

Kwa mfano, katika Hadiyth iliyotolewa na al-Bukhaariy katika Kitabu cha Al-Maghaazi Hadiyth Nambari 4168 inasema hivi:

“Wakasema: Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hana fahamu juu ya anayoyasema, jamani hebu msikilizeni vizuri." wakamuendea huku wakimuuliza. Akawaambia:

“Niacheni, maana haya niliyonayo ni bora kuliko mnayoniitia”, kisha akawausia mambo matatu; akasema:

“Watoeni washirikina nje ya Bara ya Arabu na wapokeeni vizuri wageni kama nilivyokuwa nikiwapokea”. (kisha msimulizi wa Hadiyth hii Ibn 'Abbaas, hakusema juu ya jambo la tatu au alisema; ‘nimelisahau’)” Swahiyh al-Bukhaariy 'Kitabul Maghaazi'

 

Pamoja na kuwepo kwa maandishi juu ya tukio hili la wanahistoria kuwa na mifano ya tafsiri tofauti, hakuna ushahidi wa kutosha kama tukio hili kwa maelezo ya Mashia limetokea kweli au ni maandishi tu yenyewe yaliyopachikwa ili kukidhi haja ya waliyobuni tamko hili. Tafsiri ya tukio hili halina ukweli wa kihistoria kwa sababu zifuatazo:

 

Ni muhimu kudhania kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kuzuiwa na Swahaba au na yeyote asiye Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala) kutekeleza jambo la utume wake; inashangaza zaidi kuwataja Maswahaba kuwa wanaweza kumpinga Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika Utume wakati huu akiwa katika kitanda cha mauti. Linaloshangaza zaidi ni lengo la tukio hili: Kwa mujibu wa maelezo yaliyopo ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuandika tamko alilokusudia ingawa aliishi siku nne baada ya tukio hili akiwa katika hali isiyo mbaya sana hata Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu) akarudi kitongojini kwake, kulipokuwa na umbali wa maili mbili hivi kutoka mjini Madiynah. Kama hali ilikuwa hii kwanini basi usia huu usiandikwe? Mbali zaidi ni tukio hili linavyonasibishwa na maudhui ya Aayah tatu za mwanzo wa Suratul Hujuraat zinazosomeka hivi:

 

 

  1. “Enyi mlioamini; Msitangulize (kusema lenu) mbele ya (neno la) Allaah na Mtume Wake na Mcheni Allaah Hakika ni Mwenye Kujua.”

 

  1. “Enyi mlioamini; Msipaze sauti zenu kuliko sauti ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wala msiseme naye kwa sauti ya nguvu kama mnavyosemezana nyinyi kwa nyinyi, visije vitendo vyenu vikakosa thawabu, na hali hamtambui.”

 

 

  1. “Kwa hakika wale wanaoangusha sauti zao mbele ya Mtume wa Allaah, hao ndio Allaah Amezisafisha nyoyo zao kwa kumuogopa Allaah. Basi yatakuwa kwao maghfirah na thawabu kubwa (kabisa).”

 

Sura hii ya 106 kwa utaratibu wa kushushwa na tukio hili lililotokea siku nne (tatu wengine) kabla ya kufariki kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wafasiri wa Qur-aan wengine wanasema kuwa Aayah 1-3 za Surah ya 49 wanaonesha kutotokea kwa jambo hili kwani Suratul Hujuraat ilishushwa zamani kabla ya tukio la Karatasi.

 

Anasema Imam An-Nawawiy:

“Itikadi ya kila Muislam kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hawezi kusema neno la uongo wala hawezi kubadilisha yale aliyotakiwa kutufikishia ikiwa yu mgonjwa au mzima na afya yake. Na iwapo tushayajua hayo, basi inatubainikia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angekuwa ametumwa na Mola wake kutufikishia jambo, basi lazima atatufikishia akiwa anaumwa au akiwa na afya yake.

Na kwa ajili hiyo angekuwa ametumwa kutufikishia jambo la lazima ambalo baada yake hatutopotoka, basi hata Waislam wangekhitilafiana namna gani, lazima angelifikisha neno hilo., na hii inatokana na kauli Yake Subhaanahu wa Taala pale Aliposema:

“Wafikishie yale uliyofunuliwa”

Kama vile alivyokuwa hakuacha kuyafikisha aliyoteremshiwa kabla ya hapo juu ya inadi, mateso, inda na zogo alokuwa akifanyiwa na makafiri.

 

Baya kuliko yote yaliyokwishatajwa ni kumsingizia Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa amepoteza fahamu. Utume wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) umekoma tu pale alipofariki, kwa sababu yoyote ile, hali hii ingepelekea utata mkubwa katika Utume na ujumbe wake ndio maana makafiri wa ki-Quraysh walipomwita majnuni, Allaah Alilikanusha hilo. Hivyo Allaah Asingejipinga tena na kuruhusu Mtume hata kwa nukta moja awe majnuni. Hali inakuwa ngumu zaidi wakati usia huu unapohusishwa na ‘Aliy (Radhiya Allahu ‘anhu) na kudaiwa kuwa alikuwepo. Mtume alipofariki ‘Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu), Abbaas na Nduguze Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) walikaa katika nyumba ya Faatwimah bint Muhammad (Radhiya Allaahu 'anha) kupanga mashauri ya uongozi. Kama usia huu ungekuwepo basi tungemtegemea ‘Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) auwakilishe kwenye ukumbi wa mikutano wa Saqiyfah Bani Saa'idah ambapo Answaar na Muhaajiriyn walikuwa wanajadili juu ya jambo hilo hilo la uongozi wa dola baada ya kufa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Isitoshe katika siku aliyokufa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), al-Bukhaariy katika sura ya ugonjwa wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amenakili Hadiyth isemayo ‘Abbaas alimshika mkono ‘Aliy na kumwambia twende kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza kabla hajafa nani ashike nafasi ya uongozi baada yake, kama sisi ni warithi wa halali Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ataacha usia.  ‘Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) alijibu kuwa hutauliza swali hilo kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema hapana matumaini yote ya baadae yatatoweka. Hivyo ni dhahiri hakukuwa na usia wowote kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya nani atawale baada yake.

 

Lakini ni akili ya ajabu inayofikiria kuwa uongozi wa Kiislamu utokane na ukoo wa Mtume tu kwa sababu hili ni jambo geni katika historia ya Mtume. Hakuna Mtume yoyote aliyeusia nduguze ndiyo wawe viongozi wao wanapotawafu. Ingekuwa ni Sunnah yao pangekuwa na hoja ya kuelekeza.

Lakini hata kama ingekuwa hivyo tungetegemea watoto wa kiume wa Mitume wangekuwa hai ili kukamilisha mpango huo. Matumaini ya ukoo wa Mtume kuwa ndio ungeongoza, yanapotea ukizingatia hali ya ukoo wake alipofariki haikuruhusu wapate uongozi. ‘Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa na miaka thelathini hivi. ‘Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa na miaka kumi na tatu au kumi na nne, mwingine ambae ndiye angemfuata ni Abu Sufiyaan aliyesilimu mwaka wa 8 Hijriyah (Mwaka wa Fathu Makkah) hivyo ni dhahiri pamoja na kuwa ukoo wa Mtume ulikaa kujadili uongozi, sawa, walikuwa na haki hiyo kama Waislamu wengine na walipaswa wajitokeze, lakini kukaa kama ukoo wa Mtume haikuwa sahihi.

 

Inashangaza zaidi katika ule utaratibu wa kuahidiana waliojipangia Hasan na Mu’aawiyah (Radhiya Allaahu 'anhuma) kuwa Mu’aawiyah atajapokupa Ukhalifa uende kwa mdogo wake Husayn (Radhiya Allaahu 'anhu), hasa kwa vile ni mjukuu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini vilevile kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angeacha usia kuwa awe fulani ingekuwaje baada ya yule fulani kufa? Kwa kuwa Mtume hawakilishwi katika Utume wake na uteuzi wake ungekuwa na ukomo kwa yule aliyemteua tu, wakati dola na watu vipo daima hadi siku ya mwisho isingewezekana kwa Mtume kuacha usia. Ni hivyo hivyo kwa ukoo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) una ukomo, ingefikia mahali ingebaki historia tu kama ilivyo leo watu wanajiita masharifu kwa kisingizio kuwa wana ukoo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwa kuwa ukoo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ungekoma kama koo nyingine zilizoishi hapa duniani zimetoweka na kwa kuwa dola ingeendelea kuwepo hadi mwisho wa dunia basi asingefanya usia kwa mtu yoyote kayika ukoo wake.

 

Katika Uislamu ukoo huhesabiwa kwa mwanaume, udugu kwa mfano wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na ‘Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) haumfanyi ‘Aliy (Radhiya Allaahu 'anhu) awe na damu ya Utume hivyo ahusike na Utume, hivi sio kweli na hili ni maarufu. Pengine kwa kujua hivi ndiyo sababu ya kutoachwa hai mtoto yeyote wa kiume wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Watoto wa Faatwimah bint Muhammad kwa msingi huu ni kweli Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni babu yao wa kikeni lakini ukoo wao unahesabiwa kwa babu yao wa kiumeni. Vile vile dola ya Kiislamu ni ya dunia nzima, ni mawazo butu kudhania na kushikilia kuwa ukoo wa Mtume ambao kimsingi haupo ungeweza kugawanywa duniani kote na kuendesha dola mbalimbali za Kiislamu. Udhaifu huu pamoja na maaelezo yaliyotangulia yamefanya iwe vigumu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ameacha usia unaohusu ukoo wake au mwingine yoyote. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuacha usia wa nani awe kiongozi baada ya kufariki kwake kwa sababu aliwaachia Waislamu wateue na kuchagua kiongozi wao kwa kutumia vipaji vyao kupitia maamuzi yanayohusu Uislamu wao. Katika uhai wake Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwafundisha Waislamu kuhusu uongozi katika dola ya Kiislamu, lakini utawala na Ukhalifa ni wa watu wote. Hakuna mwenye haki ya kuzuia mwingine kutawala kama Aayah ya 55 ya Sura ya 24 inavyobainisha:

 

“Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na wakatenda mema, ya kwamba atawafanya Makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya Makhalifa wa kabla yao, na kwa yakini Atawasimamishia Dini yao Aliyowapendelea, na Atawabadilishia amani baada ya khofu yao. Wawe wananiabudu Mimi, wala wasinishirikishe na chochote. Na wataokufuru baada ya hayo, basi hao ndio wapotovu.”

 

Allaah Amewaahidi wale walioamini miongoni mwenu na kufanya vitendo vizuri, atawafanya Makhalifa katika ardhi kama alivyowafanya wale kabla yao. (24:55).

 

 

Ukiachilia mbali dondoo kuwa uongozi ni wa watu wote, Mtume vile vile amefundisha maana, umuhimu na hali ya kutawala kuwa madaraka, milki, hukumu au uwezo mtu alionao katika ardhi na vilivyomo amepewa na Allaah (Subhaanahu Wa Ta’ala). Nafsi yake hapa duniani ni mdhaminiwa tu, sio mtawala wa hivyo, hana madaraka ya kutawala atakavyo, amuwakilishe Muumba na atawale kufuatana na maagizo yake:

 

Na hakika tumekuwekeni katika ardhi, na tumekujaalieni humo njia za kupatia maisha. Ni kuchache kushukuru kwenu. (7:10).

 

Wakasema: Tumeudhiwa kabla hujatufikia, na baada ya wewe kutujia! Musa akasema: Huenda Mola wenu Mlezi akamhiliki adui wenu, na akakufanyeni nyinyi ndio wa kufuatia kushika nchi, ili atazame mtavyo kuja tenda nyinyi. (7:129).

 

Na kumbukeni Alivyokufanyeni wa kushika pahala pa A'adi na Akakuwekeni vizuri katika nchi, mnajenga majumba ya fakhari katika nyanda Zake, na mnachonga majumba katika milima. Basi zikumbukeni neema za Allaah wala msitende uovu katika nchi kwa ufisadi. (7:74).

 

Taifa lolote lenye mamlaka juu ya sehemu ya ardhi ni kaimu wa Allaah:

Yeye ndiye Aliyekufanyeni manaibu katika ardhi. Na anayekufuru, basi kufuru yake ni juu yake; na kufuru za makafiri haziwazidishii kwa Mola wao Mlezi ila kuchukiwa. Wala kufuru za makafiri haziwazidishii ila khasara. (35:39).

 

Kwa hakika Tuliwatuma Mitume wetu kwa dalili waziwazi, na tukateremsha Kitabu pamoja nao na Mizani, ili watu wasimamie uadilifu, ...(57:25).  

 

Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa makusudi hakuacha uteuzi wowote wa nani ashike uongozi baada ya kufariki kwake kwa kuwa ameacha mafunzo ya kudumu ya namna ya kupata viongozi, watu wachague wenyewe kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu.

 

Na hivyo, wale wanaodai kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataliwa kuandikwa wasia wake, wasia wanaodhania hao wenye malengo yao binafsi - Mashia-, malengo ya kuwatukuza hao wanaodai ni Maimaam wao, kuwa kuzuiwa kwake kuletewa kalamu na karatasi, ndiko kulikosababisha kutoacha wasia wa kuwa nani awe Imaam au Khalifa baada yake, ni taawili potofu isiyokubaliana na nukulu (Qur-aan na Sunnah), wala kukubaliana na akili. Katika nukulu hakuna popote pale penye kuashiria kwa uwazi wala kwa uficho kuwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ameeleza kuwa ‘Aliy au yeyote katika jamaa zake kuwa awe ni Khalifa baada yake. Na kiakili, kutokana na kisa hicho, kinawasuta hapo au hilo pote lenye kudai hayo. Kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) maadam alikuwa ana uwezo wa kuzungumza hadi kuitisha kalamu na karatasi, basi asingeshindwa kueleza kwa maneno yake waziwazi huo wasia wake. Na kama angeeleza basi ungenukuliwa kwetu na wale waliohudhuria tukio hilo na haswa jamaa zake wa karibu wanaodaiwa kuwa ndio walengwa wa wasia huo!

 

Halikadhalika madai hayo yao hao wadai ni madai yenye lengo la kumfanya kama Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakujua jinsi ya kuacha wasia, na kwamba maadam kakosa pa kuandika basi na wasia usingeweza kutoka! Hayo ni madai ya kumdhalilisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa upande mwengine na kutaka kuwadanganya Waislam wasiojua Taariykh na wasiofuatilizia historia kwa kina. Na pia ni madai ya kulenga kuwatuhumu Maswahaba (Radhiya Allaahu 'anhum) kuwa wanaweza kuzuia Wahy.

 

Kisa hiki, ni moja ya mambo yanayotumiwa na baadhi ya watu wanaojidai ni Waislam wenye nia ya kuleta mpasuko na mgawanyo katika Uislam na kutia shaka katika Iymaan za Waislam. Lenye kusikitisha, Waislam wasiofuatilizia Taariykh kwa kina na wale wasiojishughulisha kusoma, wameingia kwenye mitego hiyo ya hao wavurugaji na kujikuta nao wamekuwa wanafuata na kubeba bendera hiyo ilihali hawajui inawakilisha nini.

 

Share