Mafunzo Kutoka Katika Hijrah

 

Mafunzo Kutoka Katika Hijrah

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa’iy (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

Ndugu zangu Waislam, katika kalenda ya Hijri (Kalenda ya Kiislam) imeanza, na kwa ajili hiyo tutajikumbusha kidogo juu ya umuhimu wa siku hizi kwa ajili ya kuelewa umuhimu wake na kwa ajili ya kujifunza angalau machache juu ya Hijrah ya Nabiy wetu mtukufu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba wake watukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

Mwaka jana katika mnasaba huu, tulisoma namna gani tukio la Hijrah lilivyokuwa muhimu kupita matukio yote yaliyopata kutokea katika historia ya Kiislam, na hii ni kwa sababu kutokana na Hijrah, taifa la mwanzo la Kiislam liliweza kuundwa, na Waislamu wakaweza kuweka miguu yao juu ya ardhi, madhubuti kwa ajili ya kuisimamisha dini yao, kuilinda itikadi yako, na kuweza kuieneza ulimwenguni kote.

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Waislamu wa mwanzo waliokuwa wachache sana, wakiongozwa na Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan na ‘Aliy (Radhwiya Allaahu ‘anhum), walihiari kuhatarisha maisha yao, kupoteza mali zao, milki zao pamoja na kila walichokuwa nacho kwa ajili ya kutaka radhi za Rabb wao Subhaanahu wa Ta’aalaa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:

 

مُّحَمَّدٌ رَّسُولُ اللَّـهِ ۚ وَالَّذِينَ مَعَهُ أَشِدَّاءُ عَلَى الْكُفَّارِ رُحَمَاءُ بَيْنَهُمْ ۖ تَرَاهُمْ رُكَّعًا سُجَّدًا يَبْتَغُونَ فَضْلًا مِّنَ اللَّـهِ وَرِضْوَانًا ۖ

Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ni Rasuli wa Allaah. Na wale walio pamoja naye ni wakali zaidi dhidi ya makafiri; wanahurumiana baina yao. Utawaona wakirukuu na wakisujudu wakitafuta fadhila na radhi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa). [Al-Fath: 29]

 

Tukasema kuwa kwa ajili ya umuhimu wake, ndiyo maana Waislam walikubaliana kuianzisha Kalenda ya Hijrah ya Kiislam kuanzia mwaka huo.

 

Siku tukufu ambayo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akifuatana na Sahibu yake Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu), walihama kutoka Makkah kwenda Madiynah, wakitanguliwa na kufuatiliwa na Swahaba watukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhum).

 

Waislamu ambao wakati huo walikuwa wachache sana, walipata mtihani mkubwa kutokana na mateso waliyopata pamoja na kudharauliwa na kunyanyaswa na makafiri wa Makkah. Lakini mara baada ya kutakiwa na Nabiy wao (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuihama nchi yao hiyo na kwenda Madiynah, wakaanza kukumbana na mtihani mwingine. Mtihani wa kuiacha nchi yao, nchi waliyozaliwa na kulelewa na kucheza juu ya mchanga wake. Iliwabidi waiache nchi hiyo pamoja na kuacha nyuma mali zao, nyumba zao na kila walichomiliki isipokuwa vichache sana walivyoweza kuvibeba katika safari ndefu iliyojaa kila aina ya hatari na mashaka. Walikuwa tayari kupambana na yote hayo kwa ajili ya utiifu wao kwa Rabb wao na kwa ajili ya kuinusuru na kuiendeleza dini yao.

 

Kwa vile wengi wao walitoka nyakati za usiku kwa kujificha wakihofia maisha yao, iliwabidi waache vitu vyao vingi vilivyokuwa vizito na vengine vya thamani, ili waweze kukimbia kwa wepesi na haraka na ili wasalimike na mateso ya Maquraysh. Waliacha vyote hivyo nyuma yao na kuianza safari ndefu iliyowawezesha kufika kwa ndugu zao waliokuwa wakiwasubiri kwa hamu na shauku kubwa sana huko Madiynah ili washirikiane nao katika kuiendeleza mbele dini yao hii tukufu na mpya.

 

Anasema Ibn Kathiyr katika Al-Bidaayah wan Nihaayah kuwa:

 

"Katika mwaka wa kumi na sita na inasemekana katika mwaka wa kumi na saba wa Ukhalifa wa ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Waislam walikubaliana kuianzisha Kalenda yao, kutokana na matatizo yaliyokuwa yakitokea mara kwa mara baina yao wakati watu wakiandikiana mikataba ya madeni au ya aina nyengine.

 

Waarabu walikuwa wanayohesabu ya miezi yao, lakini hawakuwa na hesabu ya miaka, na kwa ajili hiyo wengine walikuwa wakitumia kalenda za Kifursi na wengine za Kirumi na wengine wakitumia matukio ya wakati wa ujahilia.

 

‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipowataka Waislam kutoa rai zao kuhusu jambo hilo, wengine wakapendekeza ianzie mwaka aliozaliwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na wengine wakapendekeza ianzie pale alipopewa Utume na wengine wakapendekeza siku aliyokufa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Lakini Khalifa wa Waislam ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akapendelea rai zilizosema kuwa ianzie siku ile ya Hijrah na wengi wakakubaliana naye.

 

Kwa vile mwezi wa Al-Muharram ndio mwezi wa mwanzo wa Kiarabu, wakakubaliana kuhesabu kuanzia mwezi huo."

 

Ufuata ni mpangilio wa Miezi ya Kiislam:

 

Al-Muharram (Mfunguo nne)

 

Swafar

 

Rabiy’ul Awwal (Mfunguo sita)

 

Rabiy’uth Thaaniy

 

Jumaadal Awwal

 

Jumaadath Thaaniy

 

Rajab

 

Sha’abaan

 

Ramadhaan

 

Shawwaal

 

Dhul Qa'dah (Mfunguo pili)

 

Dhul Hijjah (Mfunguo tatu)

 

Baada ya kutoa dalili mbali mbali, Mwanachuoni Ibn Kathiyr katika kitabu chake hicho mashuhuri kiitwacho Al-Bidaayah wan Nihaayah akamaliza kwa kusema:

 

"Nimekuelezeeni kwa ushahidi wa kutosha ulioandamana na isnadi zake na njia zake kutoka katika Siyrah ya ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na AlhamduliLlaah na kusudi langu ni kuwa wao (Swahaba) walikubaliana wote kwa Ijmai kuianzisha Kalenda ya Kiislam kuanzia Mwaka wa Hijrah na wakakubaliana kuufanya mwezi wa mwanzo uwe mwezi wa Al-Muharram na hii pia ni kauli za Maimaam wote waliobaki".

 

Ama kuhusu rai ya Imaam Maalik, Ibn Kathiyr ameandika yafuatayo:

 

"Amesema As-Suhayliy na wengineo kuwa Imaam Malik amesema kwamba mwanzo wa Mwaka wa Kiislam ungeanzia mwezi wa Rabiy’ul-Awwal (na si Al-Muharram), kwa sababu mwezi huo ndio aliohama ndani yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na akaegemea ushahidi wake katika kauli ya Allaah Subhanahu wa Ta’aalaa pale Aliposema:

 

لَا تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا ۚ لَّمَسْجِدٌ أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَىٰ مِنْ أَوَّلِ يَوْمٍ أَحَقُّ أَن تَقُومَ فِيهِ ۚ 

Usisimame humo abadani. Bila shaka Msikiti ulioasisiwa juu ya taqwa tokea siku ya kwanza unastahiki zaidi usimame humo. [At-Tawbah: 108]

 

(Kusudi la 'Siku ya mwanzo' katika Aayah hii, ni siku ile Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipowasili Madiynah).

 

"Bila shaka kauli ya Imaam Malik ndio inayonasibiana, lakini (Swahaba kabla yake) walikwishakubaliana kuwa Mwaka wa Kiislam uanzie Mwaka aliohama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ndani yake (Mwaka wa Al-Hijrah), na wakakubaliana Mwezi wa mwanzo uwe mwezi wa Al-Muharram ili wasibabaike. Wa-AAllaahu Ta’aalaa A’alam”.

 

Hivi ndivyo alivyomaliza Imaam Al-Haafidh Ibn Kathiyr (Rahimahu Allaah).

 

Safari za jangwani zilikuwa zikiwatoa jasho majabari na mashujaa wakubwa wa wakati ule wanaosafiri wakiwa katika amani, kwa hivyo munaweza kukisia hatari za namna gani zilizokuwa zikimkabili Rasuli wa (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyeondoka akiwa na sahibu yake Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu) huku wakiwa wanasakwa na makafiri waliokwishaamua kuwa lazima auliwe, wakatangaza zawadi ya ngamia mia moja kwa yeyote atakayeweza kumkamata Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa hai au amekwishakufa.

 

Hawezi kuyakisia haya ila yule aliyewahi kuuonja moto wake.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwahi kulikata jangwa lile alipokuwa mdogo akiwa amefuatana na mama yake siku ile walipokwenda Madiynah kwa ajili ya kulizuru kaburi la baba yake, kisha akarudi Makkah peke yake kwa sababu mama yake alifariki dunia alipowasili Madiynah. Lakini safari hii Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) analikata tena jangwa hilo hilo akiwa na umri uliopindukia miaka hamsini pamoja na Sahibu yake Asw-Swiddiyq (Radhwiya Allaahu ‘anhu), si kwa ajili ya matembezi wala kwa ajili ya biashara, bali kwa ajili ya kuuendeleza ujumbe aliokuja nao.

 

Anasafiri ili aweze kuusimamisha ujumbe huo juu ya ardhi ya Yathrib (Madiynah), na kuiweka mizizi yake hapo baada ya kung'olewa katika mji wa Makkah.

 

Aliondoka Makkah kuelekea Madiynah akiwa na yakini kupita mtu yeyote yule kuwa Rabb wake Atamnusuru na kuidhihirisha dini Yake, na alikuwa na uhakika pia kuwa Rabb wake atamrudisha tena Makkah.

 

Allaah Alikwishamwambia:

فَإِنَّكَ بِأَعْيُنِنَا ۖ 

Kwani hakika wewe uko chini ya Macho Yetu. [Atw-Twuwr: 48]

 

Na Akasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ الَّذِي فَرَضَ عَلَيْكَ الْقُرْآنَ لَرَادُّكَ إِلَىٰ مَعَادٍ ۚ 

Hakika Yule Aliyekufaridhishia Qur-aan (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم,) bila shaka Atakurudisha mahali pa marejeo. [Al-Qaswasw: 85]

 

Mwenendo Wa Rusuli ('Alayhim-Salaam)

 

Kutokana na Hijrah hii Nabiy wetu mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atakuwa ametimiza Sunnah ya Rusuli wenzake waliomtangulia, kwani Rusuli yote ('Alayhim-salaam) kuanzia Nabii Ibraahiym mpaka kufikia kwa ‘Iysa (‘Alayhis-salaam), wote waliihama miji yao waliyozaliwa, wakateswa na kusubiri ili wawe mfano mwema kwa watu wao.

 

Na hii ndiyo maana Waraqah bin Nawfal siku ile alimwambia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Yalaiti ningeliishi mpaka siku ile watu wako watakapokutowa katika nchi yako".

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amesema:

 

وَقَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِرُسُلِهِمْ لَنُخْرِجَنَّكُم مِّنْ أَرْضِنَا أَوْ لَتَعُودُنَّ فِي مِلَّتِنَا ۖ 

Wakasema wale waliokufuru kuwaambia Rusuli wao: Bila shaka tutakutoeni katika ardhi yetu, au mtarudi kwa hakika katika mila zetu. [Ibraahiym: 13]

 

Tofauti Ya Kuhama Kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Na Kuhama Kwa ‘Umar Bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

"Inaweza kumpitikia mtu kutaka kufananisha baina ya kuhama kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kuhama kwa ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), akajiuliza:

 

"Kwa nini ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akahama mchana tena mbele ya watu bila kuogopa, huku akiwabishia makafiri pale alipowaendea na kuwaambia:

 

‘Zimedhalilika nyuso zenu, zimedhalilika nyuso zenu, yeyote kati yenu anayetaka mamake ampoteze na wanawe wawe mayatima na mkewe awe kizuka, basi na akutane nami nyuma ya bonde hili.’

 

Wakati Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alihama kwa kificho bila kumjuulisha mtu. Mtu anaweza kujiuliza:

 

"Hivyo ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) anaweza kuwa shujaa kuliko Nabiy?

 

Jibu lake litakuwa:

 

"Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) au Muislam yeyote yule, hukmu yao ni tofauti na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani matendo ya mtu yeyote yule awe ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) au mwengine yanahesabiwa katika dini kuwa ni matendo yake mwenyewe binafsi, na kwamba si hoja inayoweza kusimama katika dini kama yalivyo matendo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kwani mtu mwingine asiyekuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaweza kutumia njia zozote zile azitakazo anazoziona kuwa ni mnasaba kwake, ama Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yeye matendo yake ni Shari’ah, na hii maana yake ni kuwa matendo yake yote yanayohusiana na dini yanahesabiwa kuwa ni Shari’ah kwetu, na kwa ajili hiyo Mafundisho yake (Sunnah zake) yakawa ni asili ya pili ya Shari’ah, yakiwemo matendo yake, maneno yake, sifa zake na yale yaliyofanywa mbele yake na akayakubali.

 

Lau kama Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) angefanya kama alivyofanya ‘Umar bin Al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu), baadhi ya watu wangedhania kuwa hivyo ndivyo anavyowajibikiwa kila Muislam kufanya, na kwamba haina haja mtu kuchukua tahadhari wala kuogopa pale anapokuwa katika hatari.

 

Baada Ya Kuhamia Madiynah

 

Tuliona huko nyuma kuwa mara baada ya kuwasili mjini Madiynah, jambo la mwanzo alilofanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni kufungisha udugu baina ya watu wa Makkah na watu wa Madiynah, na jambo la pili ni kuujenga Msikiti uliokuwa mfano wa Chuo Kikuu kilichokuwa kikifundisha Imani, udugu, umoja, ushujaa, fiqhi pamoja na tabia na mwenendo mwema, na kutokana na hayo Chuo hicho kikaweza kutoa mashujaa walioweza kuzifungua nchi nyingi pamoja na nyoyo nyingi.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Akiwa Madiynah

 

Anasema Shaykh Abu Bakr Al-Jazairiy:

 

"Hakika ya miaka yote kumi na tatu aliloishi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pale Makkah tokea alipopewa utume mpaka siku ile aliyohama kwenda Madiynah, yote ilikuwa ni maumivu na machozi na huzuni. Hakupata kufurahi hata kwa muda wa saa moja au kustarehe angalau kwa siku moja.

 

Ama miaka kumi aliloishi Madiynah, yote ilikuwa ni miaka ya Jihaad iliyokamatana. Hakupata hata siku moja kukaa bure wala kustarehe. Hata maisha; kwake yalikuwa magumu, hakupata hata siku moja kushiba mkate au tende wala hata kula vizuri mara mbili katika siku moja.

 

Naam, ingawaje kwa siku alizoishi Madiynah zilikuwa ni siku za kuchomoza, lakini siku nyingi katika hizo zilikuwa ni za kuunguza".

 

Kusilimu Kwa ‘Abdullaah Bin Salaam (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Mara baada ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwasili mji wa Madiynah alikuja kwake ‘Abdullaah bin Salaam (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kuzitamka shahada mbili.

 

Akasema:

 

"Nashuhudia kuwa hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Allaah na kwamba wewe ni Rasuli wa Allaah na kwamba uliyokuja nayo ni haki. Ee Rasuli wa Allaah, Mayahudi ni watu waongo, wanajua kuwa mimi ni bwana wao na mwana wa bwana wao na wanajuwa pia kuwa mimi ni ‘Aalim wao na mwana wa ‘Aalim wao, kwa hivyo nakuomba (uniache nijifiche, kisha) uwaite na uwaulize juu yangu kabla ya kuwajulisha juu ya kusilimu kwangu, kwani wakijua kuwa nimesilimu watasema juu yangu yale nisiyokuwa nayo".

 

Wakasema mara tatu:

 

"Sisi hatujui"

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

 

“Ana daraja gani kwenu ‘Abdullaah bin Salaam?”

 

Wakasema:

 

"Yule ni bwana wetu na mwana wa bwana wetu, na ‘Aalim kutupita sote na mwana wa ‘aalim kutupita sote".

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

 

“Munaonaje akisilimu?”

 

Wakasema:

 

"Haiwezekani hata siku moja akasilimu"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza hivyo mara tatu, kisha akasema:

 

“Ee ‘Abdullaah bin Salaam, watokee.”

 

Akawatokea na kusema:

 

"Enyi Mayahudi, mcheni Allaah kwani naapa kwa yule ambaye hapana anayepaswa kuabudiwa isipokuwa Yeye, mnajua vizuri kuwa huyu ni Rasuli wa Allaah na kwamba amekuja na haki".

 

Wakasema:

 

"Muongo! wewe si bwana wetu wala si ‘Aalim wetu".

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaamrisha watolewe nje.

 

[Imepokewa na Al-Bukhaariy]

 

Mwenye Kumtii Nabiy (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Atakuwa Pamoja Naye

 

Swahaba wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na hususan watu wa Madiynah walikuwa wakimpenda Nabiy wao (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kupita kiasi, na walikuwa tayari wakati wote kuzitanguliza roho zao na nafsi zao kwa ajili ya kumlinda Nabiy wao mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na yale aliyokuja nayo. Ni wao waliohatarisha maisha yao hapo mwanzo walipomfuata Nabiy wao mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huko Makkah katika usiku ule wa hatari na kumpa ahadi ya kumnusuru na kumlinda ikiwa atahamia kwao Madiynah. Kisha wakafungamana naye kwa siri mahali panapoitwa Al-’Aqabah katika mafungamano yaliyokokuja kujulikana baadaye kama 'Fungamano la ‘Aqabah' (la mwanzo na la pili).

 

Watu wa Madiynah waliitimiza ahadi yao hiyo ya kumlinda Nabiy wao (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na kuwalinda Waislam wote waliohamia kwao na kuwasaidia kwa hali na mali. Na pale Allaah Subhaanahu Wa Ta’aalaa Alipoiteremsha kauli Yake:

 أُذِنَ لِلَّذِينَ يُقَاتَلُونَ بِأَنَّهُمْ ظُلِمُوا ۚ وَإِنَّ اللَّـهَ عَلَىٰ نَصْرِهِمْ لَقَدِيرٌ ﴿٣٩﴾الَّذِينَ أُخْرِجُوا مِن دِيَارِهِم بِغَيْرِ حَقٍّ إِلَّا أَن يَقُولُوا رَبُّنَا اللَّـهُ ۗ 

Wameruhusiwa (kupigana) kwa wale wanaopigwa kwa kuwa wamedhulumiwa. Na kwamba Allaah bila shaka ni Muweza wa kuwanusuru. Ambao wametolewa majumbani mwao bila ya haki isipokuwa kwa kuwa wanasema: Rabb wetu ni Allaah. [Al-Hajj: 39-40]

 

Watu wa Madiynah wakaingia katika mapambano mbali mbali na majeshi ya makafiri mpaka pale Allaah alipowawezesha Waislamu kuuteka mji wa Makkah na kuyabomoa masanamu yaliyokuwepo ndani ya Al-Ka’abah na kuidhihirisha Haki na kuiangamiza Baatwil.

 

Hadiyth ifuatayo inatuwezesha kuihisi angalau kwa uhaba ladha ya namna Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum) na hasa watu wa Madiynah walivyokuwa wakimpenda na kumuenzi na kumthamini Nabiy wao mtukufu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na namna gani walivyokuwa tayari kujitolea kwa hali na mali kumtii Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imetolewa na Imaam Al-Bukhaariy na Muslim na Atw-Twabaraaniy na wengineo kuwa mara baada ya kumalizika vita vya kuuteka mji wa Makkah, Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) aliwakusanya mateka na kuwauliza:

 

“Mnadhani nitakufanyeni nini?”

 

Wakajibu:

 

‘Utatufanyia kila la kheri, ewe ndugu mwema na mwana wa ndugu mwema.’

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

 

“Nendeni, nyote nimekuacheni huru.”

 

Karibu mateka wote hao wakasilimu kwa hiari yao na kujiunga na jeshi la Kiislamu lililoondoka hapo Makkah kuelekea mji wa Hunayn kwa ajili ya kupambana na majeshi ya watu wa Huwzan waliokuwa njiani kuelekea Makkah kuwashambulia Waislam.

 

Imepokelewa kutoka kwa ‘Abdullaah bin Zayd (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa baada ya Waislam kushinda katika vita vya Hunayn, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwagawia ngawira iliyopatikana katika vita hivyo watu wa Makkah tu hasa wale waliosilimu hivi karibuni kwa ajili ya kuwalainisha nyoyo zao, na watu wa Madiynah hawakupewa chochote.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alijuwa kuwa watu wa Madiynah hawakufurahi kwa sababu na wao pia walitegemea kupewa chochote katika ngawira ile kama walivyopewa wenzao watu wa Makkah.

 

Alipojulishwa juu ya hayo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akawaita watu wa Madiynah na kuwahutubia, akasema:

 

“Nini haya maneno niliyosikia kuwa mlikuwa mkiyasema?”

 

Viongozi wao wakasema:

 

"Ama wakubwa wetu hawakusema lolote, isipokuwa watu wengine wanasema; "Allaah Amghufirie Nabiy wake, anawapa Maquraysh ngawira kwa mamia na sisi hatupi chochote wakati damu zao bado hata hazijakauka juu ya panga zetu?"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

 

“Mmekasirika kwa sababu ya faida ndogo tu ya kidunia enyi watu wa Madiynah? Mimi nimewapa hawa kwa sababu wao ndio kwanza wametoka katika ukafiri na kuingia katika Uislam ili niwalainishe nyoyo zao, nikakuacheni nyinyi kwa kuutegemea Uislam wenu. Enyi watu wa Madiynah! Si niliwakuta mmepotoka Allaah Akakuongozeni kupitia kwangu? Na nikawakuta masikini na Allaah Akakutajirisheni kupitia kwangu? Mmegawanyika na Allaah Akakuunganisheni kupitia kwangu? Mafakiri na Allaah Akakuneemesheni kupitia kwangu?”

 

Walikuwa kila wanapoulizwa wakijibu:

 

"Allaah Ametufanyia ihsani zaidi na Nabiy Wake ametufanyia Ihsani zaidi"

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawauliza:

 

“Mbona hamnijibu?”

 

Wakasema:

 

"Tukujibu nini ee Rasuli wa Allaah?"

 

Akasema:

 

“Kama mngenijibu kwa maneno mengine zaidi ya haya mngekuwa mnasema kweli. Mngetaka, mngeweza kusema; "Na wewe pia ulikuja kwetu ukiwa umefukuzwa na watu wako na sisi tukakupokea, umekadhibishwa na sisi tukakusadiki. Ulikuja peke yako umo hatarini na sisi tukakunusuru, na tukayakubali yale watu wako waliyoyakataa. Kisha mkawa mnanihesabia mema yote mliyonitendea.”

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akawaambia:

 

“Hamridhiki wakati wenzenu wanaondoka wakiwa na ngamia na kondoo na nyinyi mtaondoka mkiwa na Rasuli wa Allaah mpaka makwenu? Watu wa Madiynah (Al-Answaar) ni mfano wa nguo iliyokamatana na ngozi na waliobaki ni mfano wa guo la juu, Enyi watu wa Madiynah! Si Allaah Amekuiteni majina mazuri mazuri (kama vile) 'Answaar wa Allaah' na 'Answaar wa Nabiy Wake?' Naapa kwa Yule ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake, lau kama nisingehajiri basi ningelikuwa mmoja kati ya watu wa Madiynah, na lau kama watu wote watafuata njia zao katika mabonde na mitaa, na watu wa Madiynah watafuata njia nyingine, basi mimi ningefuata njia ya watu Madiynah. Allaah Warehemu ma-Answaar (watu wa Madiynah) na wana wa Answaar na wajukuu wa Answaar.”

 

Anasema Ibn Is-haaq aliyoisimulia sehemu ya mwisho ya Hadiyth hii kuwa:

 

"Waliohudhuria wakaanza kulia kwa kwikwi mpaka ndevu zao zikarowa, wakasema:

 

"Tumeridhika na Allaah kuwa Rabb wetu na Rasuli Wake kuwa sehemu yetu."

 

Kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaondoka na wao wakatawanyika.

 

Sehemu ya mwisho ya Hadiyth hii imepokelewa kwa njia ya Imaam Ahmad peke yake na kusimuliwa na Ibn Is-haaq.

 

Ndugu zangu Waislam, anayetaka kuwa pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba wake watukufu (Radhwiya Allaahu ‘anhum) siku ya Qiyaamah, lazima awe mtiifu wa maamrisho aliyokuja nayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Imepokelewa na Atw-Twabaraaniy na Ibn Mardawiya na Abu Na’iym kutoka kwa Mama wa Waumini ‘Aaishah bint Abi Bakr (Radhwiya Allaahu anhum) kuwa: Siku moja mtu mmoja alimwendea Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na kumwambia:

 

"Ee Rasuli wa Allaah, kwa hakika mimi nakupenda kuliko ninavyoipenda nafsi yangu na kuliko ninavyowapenda wanangu. Ninapokuwa nyumbani basi nikikukumbuka tu, siwezi kustahamili tena, lazima nije nikutazame. Lakini kila ninapokumbuka kuwa siku moja mimi nitakufa na wewe utakufa, kisha nikakumbuka kwamba wewe daraja yako itakuwa juu pamoja na Rusuli, na mimi nikiingia Jannah naogopa (daraja yangu haitokuwa ya juu kama yako) nisiweze kukuona tena huko".

 

Katika riwaya nyingine:

 

"Swahaba yule aliyekuwa katika watu wa Madiynah alilia sana, na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipomuuliza:

 

“Nini kinachokuliza?”

 

Akamjibu:

 

"Kila ninapokumbuka kuwa wewe daraja yako itakuwa ya juu pamoja na Rusuli, na mimi nikiingia Jannah naogopa (daraja yangu haitokuwa ya juu kama yako) na sitoweza kukuona tena huko".

 

Kabla Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kumjibu Swahaba yule (Radhwiya Allaahu ‘anhu), Jibriyl (‘Alayhis-salaam) aliteremka na kauli ya Allaah isemayo:

 

وَمَن يُطِعِ اللَّـهَ وَالرَّسُولَ فَأُولَـٰئِكَ مَعَ الَّذِينَ أَنْعَمَ اللَّـهُ عَلَيْهِم مِّنَ النَّبِيِّينَ وَالصِّدِّيقِينَ وَالشُّهَدَاءِ وَالصَّالِحِينَ ۚ وَحَسُنَ أُولَـٰئِكَ رَفِيقًا ﴿٦٩﴾ 

Na atakayemtii Allaah na Rasuli, basi hao watakuwa pamoja na wale Allaah Aliowaneemesha miongoni mwa Manabii na Swiddiqiyna na Mashuhadaa na Swalihina, na uzuri ulioje kuwa pamoja na hao. [An-Nisaa: 69]

 

Yaani atakayefanya yale aliyoamrishwa na Rabb wake na Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na akayaacha yale alokatazwa na Rabb wake na aliokatazwa na Rasuli wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), basi Allaah Atamuingiza katika Jannah yake na atakuwa pamoja na Rusuli na Swiddiqiyn na Mashahidi na Swaalihiyn (watu wema).

 

Share