Jazaa Ya Waja Wema Na Neema Za Jannah

Jazaa Ya Waja Wema Na Neema Za Jannah

 

Alhidaaya.com

 

 

Tunapotoka katika msimu mtukufu wa utendaji  ‘ibaadah tele  kama Ramadhwaan au Hajj au kwa kila mja mwema, mtiifu, mwenye taqwa na mwenye kutenda matendo mengi yenye kumridhisha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa),  basi ataraji Rahma za Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kuingizwa Jannah ya Neema ambako humo ni kuishi milele kwa amani na furaha. Hivyo tujikumbushe Aayah ifuatayo tukufu inayobashiria kuhusu hiyo Jannah ili tuwe na matarajio ya kuzidi kuendelea katika taqwa, utiifu na kutenda mema hadi hapo tutakapokutana na Muumba wetu (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

   

 وَبَشِّرِ الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أَنَّ لَهُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ كُلَّمَا رُزِقُوا مِنْهَا مِن ثَمَرَةٍ رِّزْقًا ۙ قَالُوا هَـٰذَا الَّذِي رُزِقْنَا مِن قَبْلُ ۖ وَأُتُوا بِهِ مُتَشَابِهًا ۖ وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ ۖ وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٢٥﴾

Na wabashirie wale walioamini na wakatenda mema kwamba watapata Jannaat (bustani) zipitazo chini yake mito, kila watakaporuzukiwa humo katika matunda kuwa ni riziki husema: Haya ndiyo yale tuliyoruzukiwa kabla. Na wataletewa hali ya kuwa yanashabihiana, na watapata humo wake waliotakaswa, nao humo ni wenye kudumu.  [Al-Baqarah: 25]

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anatuelezea hali ya waja wema itakavyokuwa huko Jannah kwamba kutakuweko na mito inayopita chini yake, chemchemu zinazotiririka na Hadiyth ifuatayo inataja pia:

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه عن النبي صلى الله عليه وآله سلم قال (( أنهار الجنة تفجر تحت تلال أو من تحت جبال المسك ))  إبن أبي حاتم 1:87

Amehadithia Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Mito ya Jannah inachipuka kutoka chini ya vilima au majabali ya misk)) [Ibn Abiy Haatim 1:87]

 

Na pia katika Aayah hiyo tukufu, watu wa Jannah watakapoletewa matunda watakula, kisha wataletewa tena watashangaa kuwa yamefanana na yale waliyokwishakula, lakini kumbe ladha yake ni tofuati ingawa ni ya rangi ile ile.  

 

Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: "Hakuna kitu katika Jannah kinachofanana na cha duniani isipokuwa majina."

 

Na katika usimulizi mwingine: Ibn 'Abbaas (Radhwiya Allaahu 'anhumaa) amesema: "Majina pekee yaliyokuwa katika dunia hii na Jannah ndio yanafanana.” [Atw-Twabariy 1:392]

 

 

Na Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Amewasifu wake wa watu wa Jannah katika Qur-aan katika Aayah mbali mbali kuwa ni wake wenye macho meupe makubwa ya kupendeza (Huwr-Al-‘Ayan), na hapa Amewasifu pia kuwa ni wake waliosafika kabisa.

 وَلَهُمْ فِيهَا أَزْوَاجٌ مُّطَهَّرَةٌ  

na watapata humo wake waliotakaswa.”

 

Ibn Abi Twalhah ameeleza kwamba Ibn 'Abbaas (Radhwiya-Allaahu 'anhumaa) amesema, "Wametakasika kutokana na uchafu na unajisi" [At-Twabariy 1:295]. 

Mujaahid amesema, "Wametakasika kutokana na hedhi, kwenda haja kubwa na ndogo, kutema mate, shahawa (manii) na mimba."  [At-Twabariy 1:396]. 

 

Qataadah amesema, "Wametakasika kutokana na unajisi na madhambi." na katika usimulizi mwengine amesema "kutokana na hedhi na mimba." [Ibn Haatim 1:91]

 

وَهُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Nao humo ni wenye kudumu.” 

 

Ni kwamba, wataishi humo milele kwa furaha na amani bila ya tabu yoyote, wala maudhi au ugonjwa wala dhiki ya aina yoyote, bali hakutakuwepo tena mauti, ni maisha ya raha yasiyo na mwisho.

 

Isitoshe, Jannah hiyo mchanga wake pia ni wa misk inayonukia vizuri, mawe yake ni ya lulu na johari, nyumba zake ni maqasri ya fakhari, viti vyake vya fakhari vilivyoinuka, matakia na mazulia yaliyotandikwa vizuri, vyombo vya dhahabu na fedha, nguo za hariri, matunda ya kila aina. Hadiyth zifuatazo zimethibitisha sifa za Jannah:

 

 

Mahema ya lulu:

 

عن أبي موسى رضي الله عنه : أنَّ النبيَّ صلى الله عليه وسلم  قال : (( إنَّ لِلمُؤْمِنِ فِي الجَنَّةِ لَخَيْمَةً مِنْ لُؤْلُؤَةٍ وَاحِدَةٍ مُجَوَّفَةٍ طُولُها في السَّمَاءِ سِتُّونَ مِيلاً . لِلمُؤْمِنِ فِيهَا أَهْلُونَ يَطُوفُ عَلَيْهِمُ المُؤْمِنُ فَلاَ يَرَى بَعْضُهُمْ بَعْضاً )) مُتَّفَقٌ عَلَيهِ

Abuu Muwsaa (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema : “Hakika, Muumini katika Jannah atakuwa na  hema la lulu ambalo liko mviringo, urefu wake ni maili sitiini kwenda juu. Muumini atakuwa na familia yake humo, Muumini atakuwa akiwazunguka humo nao hawaonani (jinsi lilivyo kubwa).”  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Kuna ambayo macho hayajapatapo kuona wala masikio kusikia, wala akili kuyawazia:

 

وعن سهل بن سعد رضي الله عنه ، قال : شَهِدْتُ مِنَ النبيّ صلى الله عليه وسلم مَجْلِساً وَصَفَ فِيهِ الجَنَّةَ حَتَّى انْتَهَى ، ثُمَّ قَالَ في آخِرِ حَدِيثِهِ : (( فيهَا مَا لاَ عَينٌ رَأَتْ ، وَلاَ أُذُنٌ سَمِعَتْ ، وَلاَ خَطَرَ عَلى قَلْبِ بَشَرٍ )) ثُمَّ قَرَأَ : [ تَتَجَافَى جُنُوبُهُمْ عَنِ المَضَاجِعِ ] إلى قوله تعالى : [ فَلاَ تَعْلَمُ نَفْسٌ مَا أُخْفِيَ لَهُمْ مِنْ قُرَّةِ أَعْيُنٍ ] [ السجدة: 16 - 17 ] . رواه البخاري

Sahl bin Sa’d (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesimulia:“Siku moja nilishuhudia kikao fulani cha Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Ambapo ndani yake aliisifu Jannah mpaka akamaliza. Mwisho wa mazungumzo yake alisema:“Ndani yake mna ambayo hayajaonekanapo na jicho lolote, wala hayajasikiwa na sikio lolote wala hayajawahi kufikiriwa na moyo wowote wa mwana Aadam,” Kisha akasoma: “Mbavu zao zinatengana na vitanda, wanamuomba Rabb wao kwa khofu na matumaini, na katika yale Tuliyowaruzuku wanatoa.  Basi nafsi yoyote haijui yaliyofichiwa katika yanayoburudisha macho. Ni jazaa kwa yale waliyokuwa wakiyatenda.” [As-Sajdah 17 – 18] [Al-Bukhaariy]

Watu wa Jannah watatakaswa na kila aina ya uchafu:

 

عن جابر رضي الله عنه، قَالَ : قَالَ رسولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم: (( يَأكُلُ أَهْلُ الجَنَّةِ فِيهَا ، وَيَشْرَبُونَ ، وَلاَ يَتَغَوَّطُونَ ، وَلاَ يَمْتَخِطُونَ ، وَلاَ يَبُولُونَ ، وَلكِنْ طَعَامُهُمْ ذَلِكَ جُشَاءٌ كَرَشْحِ المِسْكِ ، يُلْهَمُونَ التَّسْبِيحَ وَالتَّكْبِيرَ ، كَمَا يُلْهَمُونَ النَّفَسَ )) . رواه مسلم 

Imehadithiwa na Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhu) kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:  “Watu wa Jannah watakula humo, watakunywa, wala hawataenda haja kubwa, wala hawatatokwa kamasi, wala hawatakojoa, lakini chakula chao kitatoka kwa kuteuka na ikitoa harufu kama ya miski.  Watapewa ilhamu ya kumsabihi Allaah kama vile wanavyopewa ilhamu ya kupumua (bila ya shida)” [Muslim]

 

 

Chochote utakachotamani humo utakipata bila shida:

 

عن أبي هريرة رضي الله عنه : أنَّ رسولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم قال : (( إنَّ أدْنَى مَقْعَدِ أَحَدِكُمْ مِن الجَنَّةِ أنْ يَقُولَ لَهُ : تَمَنَّ ، فَيَتَمَنَّى وَيَتَمَنَّى فَيقُولُ لَهُ : هَلْ تَمَنَّيتَ ؟ فيقولُ : نَعَمْ ، فيقُولُ لَهُ : فَإنَّ لَكَ ما تَمَنَّيتَ وَمِثْلَهُ 

مَعَهُ )) . رواه مسلم

Abuu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika daraja ya chini mno ya mmoja wenu Jannah, ni kuwa Allaah Atamwambia “Tamani!” Atatamani kila atakalo. Allaah Atamuuliza: Umeshamaliza kutamani?” Atajibu: “Ndio.” Allaah Atamwambia: “Nimekupa ulichotamani na Nimekupa kama hicho.” [Muslim]

 

 

Wanawake wazuri (Huwrul-'Ayn walioandaliwa wanaume wa Jannah):

 

 

Zaidi ya neema hizo ni kwamba tutaonana naye Rabb wetu Mtukufu na kupata Radhi Zake kama alivyotuthibitishia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) katika Hadiyth:

 

 

Kuonana Naye Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) waziwazi:

 

عن جرير بن عبد الله رضي الله عنه، قال: كُنَّا عِندَ رَسُولِ اللهِ صلى الله عليه وسلم فَنَظَرَ إلَى القَمَرِ لَيْلَةَ البَدْرِ، وَقَالَ : (( إنَّكُمْ سَتَرَوْنَ رَبَّكُمْ عَيَاناً كما تَرَوْنَ هَذَا القَمَرَ ، لاَ تُضَامُونَ فِي رُؤْيَتِهِ )) متفق عليه

Jariyr bin Abdillaah  (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesimulia: “Tulikuwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akautizama mwezi usiku wa arbatashara, akatuambia: “Hakika mtamuona Rabb wenu wazi wazi kama mnavyouwona mwezi huu, hamtapata shida katika kumuona.” [Bukhari na Muslim]

 

وعن صُهيب رضي الله عنه: أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم قال : (( إذا دَخَلَ أهْلُ الجَنَّةِ الجَنَّةَ يَقُولُ اللهُ تَبَارَكَ وَتَعَالَى : تُريدُونَ شَيئاً أَزيدُكُمْ ؟ فَيقُولُونَ : ألَمْ تُبَيِّضْ وُجُوهَنَا ؟ ألَمْ تُدْخِلْنَا الجَنَّةَ وَتُنَجِّنَا مِنَ النَّارِ ؟ فَيَكْشِفُ الحِجَابَ ، فَمَا أُعْطُوا شَيْئاً أَحَبَّ إلَيْهِمْ مِنَ النَّظَرِ إلَى رَبِّهِمْ )).رواه مسلم .

Suhaib (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Watu wa Jannah watakapokuwa wameshaingia Jannah, Allaah ‘Azza wa Jalla Atawauliza: “Mnataka Niwazidishiye chochote?” Watasema: “Si Umezing’arisha nyuso zetu? Si Umetuingiza Jannah na Umetuepusha na moto?” Allaah ‘Azza wa Jalla Ataondoa pazia.  Basi watakuwa hakuna walichopewa kinachowapendeza mno kuliko kumtazama Rabb wao!” [Muslim] 

 

Kupata Radhi Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) za milele:

 

وعن أبي سعيد الخدري رضي الله عنه: أنَّ رسول الله صلى الله عليه وسلم قال : (( إنَّ الله  (عزّ وجلّ) يَقُولُ لأَهْلِ الجَنَّةِ : يَا أهْلَ الجَنَّةِ ، فَيقولُونَ : لَبَّيكَ رَبَّنَا وَسَعْدَيْكَ ، وَالخَيْرُ في يَديْكَ ، فَيقُولُ : هَلْ رَضِيتُم ؟ فَيقُولُونَ : وَمَا لَنَا لاَ نَرْضَى يَا رَبَّنَا وَقَدْ أَعْطَيْتَنَا مَا لَمْ تُعْطِ أحداً مِنْ خَلْقِكَ ، فَيقُولُ : ألاَ أُعْطِيكُمْ أفْضَلَ مِنْ ذلِكَ ؟ فَيقُولُونَ : وَأيُّ شَيءٍ أفْضَلُ مِنْ ذلِكَ ؟ فَيقُولُ : أُحِلُّ عَلَيكُمْ رِضْوَانِي فَلاَ أسْخَطُ عَلَيْكُمْ بَعْدَهُ أبَداً )) . متفق عليه 

Abuu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhwiya Allaahu 'anhu) amesema: “Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah ('Azza wa Jalla) atawaambia watu wa Jannah: “Enyi watu wa Jannah.” Wataitikia: “Labbayka Rabb wetu, Utukufu ni Wako na Kheri imo Mkononi Mwako.” Atawauliza: “Mmeridhika?” Watajibu: “Kwa nini tusiridhike ee Rabb wetu ilhali Umetupa ambayo Hukumpa yeyote katika viumbe Vyako!” Allaah atawauliza: “Je, niwape kilicho bora kuliko hicho Nilichowapa? Watasema “Ni kitu gani kilicho bora kuliko hicho?” Allaah atawaambia: “Nimewateremshia Radhi Yangu Sitawakasirikia milele baada ya leo.” [Bukhari na Muslim]

 

Baadhi ya Aayaat zinazotaja sifa za Jannah:

 

 

Hakuna kuchukiana, nyoyo zitaondoshwa mafundo, hakuna machofu wa tabu:

 

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿٤٥﴾ ادْخُلُوهَا بِسَلَامٍ آمِنِينَ﴿٤٦﴾ وَنَزَعْنَا مَا فِي صُدُورِهِم مِّنْ غِلٍّ إِخْوَانًا عَلَىٰ سُرُرٍ مُّتَقَابِلِينَ﴿٤٧﴾ لَا يَمَسُّهُمْ فِيهَا نَصَبٌ وَمَا هُم مِّنْهَا بِمُخْرَجِينَ﴿٤٨﴾

Hakika wenye taqwa watakuwa katika Jannaat na chemchemu. (Wataambiwa): Ingieni humo kwa salama mkiwa katika amani. Na Tutaondosha mafundo ya kinyongo yaliyomo vifuani mwao, wakiwa ndugu, juu ya makochi yaliyoinuliwa wakikabiliana. Hautowagusa humo uchovu nao humo hawatotolewa. [Al-Hijr: 45-48]

 

 

Vyombo watakavyotumia watu wa Jannah na matunda kila aina:

 

 يَا عِبَادِ لَا خَوْفٌ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ وَلَا أَنتُمْ تَحْزَنُونَ﴿٦٨﴾ الَّذِينَ آمَنُوا بِآيَاتِنَا وَكَانُوا مُسْلِمِينَ﴿٦٩﴾ ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ﴿٧٠﴾ يُطَافُ عَلَيْهِم بِصِحَافٍ مِّن ذَهَبٍ وَأَكْوَابٍ ۖ وَفِيهَا مَا تَشْتَهِيهِ الْأَنفُسُ وَتَلَذُّ الْأَعْيُنُ ۖ وَأَنتُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴿٧١﴾ وَتِلْكَ الْجَنَّةُ الَّتِي أُورِثْتُمُوهَا بِمَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ﴿٧٢﴾ لَكُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ كَثِيرَةٌ مِّنْهَا تَأْكُلُونَ﴿٧٣﴾

 

Enyi waja Wangu! Hakuna khofu juu yenu leo, na wala nyinyi hamtohuzunika. Ambao wameamini Aayaat Zetu na wakawa Waislamu. Ingieni Jannah nyinyi na wake zenu mfurahishwe. Watapitishiwa sahani za dhahabu na bilauri, na humo mna yale yanayotamani nafsi na ya kuburidisha macho, nanyi humo ni wenye kudumu. Na hiyo ni Jannah ambayo mmerithishwa kwa yale mliyokuwa mkitenda. Mtapata humo matunda mengi mtakayokuwa mnakula. [Az-Zukhruf: 68-73]

 

Huwr Al-‘Ayn (Wake Wazuri Wa Jannah wenye macho makubwa ya kupendeza) na mazuri mengineyo:

 

إِنَّ الْمُتَّقِينَ فِي مَقَامٍ أَمِينٍ﴿٥١﴾ فِي جَنَّاتٍ وَعُيُونٍ﴿٥٢﴾ يَلْبَسُونَ مِن سُندُسٍ وَإِسْتَبْرَقٍ مُّتَقَابِلِينَ﴿٥٣﴾ كَذَٰلِكَ وَزَوَّجْنَاهُم بِحُورٍ عِينٍ﴿٥٤﴾ يَدْعُونَ فِيهَا بِكُلِّ فَاكِهَةٍ آمِنِينَ﴿٥٥﴾لَايَذُوقُونَ فِيهَا الْمَوْتَ إِلَّا الْمَوْتَةَ الْأُولَىٰ ۖ وَوَقَاهُمْ عَذَابَ الْجَحِيمِ﴿٥٦﴾ فَضْلًا مِّن رَّبِّكَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ﴿٥٧﴾

Hakika wenye taqwa wako katika mahali pa amani. Katika Jannaat na chemchemu. Watavaa hariri laini na hariri nzito nyororo wakiwa wamekabiliana. Hivyo ndivyo!  Na Tutawaozesha mahuri (wanawake wa Jannah) wenye macho ya kupendeza. Wataagiza humo kila aina ya matunda wakiwa katika amani. Hawatoonja humo mauti isipokuwa mauti yale ya awali na (Allaah) Atawakinga na adhabu ya moto uwakao vikali mno. Ni fadhila kutoka kwa Rabb wako.  Huko ndiko kufuzu adhimu. [Ad-Dukhaan: 51-57]

 

 

Vinywaji vya watu wa Jannah, na mengineyo mazuri:

 

 إِنَّ الْأَبْرَارَ لَفِي نَعِيمٍ ﴿٢٢﴾ عَلَى الْأَرَائِكِ يَنظُرُونَ ﴿٢٣﴾تَعْرِفُ فِي وُجُوهِهِمْ نَضْرَةَ النَّعِيمِ ﴿٢٤﴾يُسْقَوْنَ مِن رَّحِيقٍ مَّخْتُومٍ ﴿٢٥﴾خِتَامُهُ مِسْكٌۚ وَفِي ذَٰلِكَ فَلْيَتَنَافَسِ الْمُتَنَافِسُونَ ﴿٢٦﴾وَمِزَاجُهُ مِن تَسْنِيمٍ ﴿٢٧﴾عَيْنًا يَشْرَبُ بِهَا الْمُقَرَّبُونَ ﴿٢٨﴾

Hakika Waumini watendao wema kwa wingi  bila shaka watakuwa kwenye neema (taanasa, furaha n.k). Kwenye makochi ya fakhari wakitazama. Utatambua nyuso zao kwa nuru ya neema (taanasa, furaha). Watanyweshwa kinywaji safi na bora kabisa cha mvinyo kilichozibwa. Mwisho wake ni miski. Na katika hayo basi washindane wenye kushindana … Na mchanganyiko wake ni kutokana na Tasniym. Ni chemchemu watakayokunywa humo watakaokurubishwa (kwa Allaah). [Al-Mutwaffifiyn:22 - 28]

 

Amani na maamkizi kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾

Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi.

 

هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾

Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea.

 

 

لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾

Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba.

 

سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾

 “Salaamun!” Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye kurehemu.     [Yaasiyn: 55-58]

 

Basi nani asiyetamani Jannah baada ya kutambua neema na starehe zilizomo humo?  Bila shaka kila mmoja wetu ataitamani na kuomba aipate.  Lakini kuipata Jannah sio kwa wepesi ila baada ya juhudi ya kuendelea kuwa katika utiifu na taqwa na kufanya matendo mema kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) mara nyingi Anapoitaja Jannah Humalizia kwa Kauli Yake:

 

نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ

Ni ujira mwema ulioje huo wa watendao.

 

Kama ilivyo katika Aayah:

 

 وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ لَنُبَوِّئَنَّهُم مِّنَ الْجَنَّةِ غُرَفًا تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ خَالِدِينَ فِيهَا ۚ نِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ ﴿٥٨﴾

 Na wale walioamini na wakatenda mema, bila shaka Tutawawekea makazi ya ghorofa katika Jannah, yapitayo chini yake mito, ni wenye kudumu humo. Uzuri ulioje ujira wa watendao. [Al-'Ankabuwt:58]

 

 

Basi ni kujitahidi kufanya mema ili kulipwa ujira mzuri huo wa Jannah yenye neemah tele.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Atujaaliye miongoni mwa Waumini Atakaowaingiza Jannah, kwani Yeye ni Mkarimu, Mpole na Mwingi wa Rehma.  Aamiyn.

 

 

 

Share