016-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Kufutwa Kisomo Nyuma Ya Imaam Katika Swalah Za Sauti, Na Kuwajibika Katika Swalah Za Kimya

 

 

KUFUTWA KISOMO NYUMA YA IMAAM KATIKA SWALAH ZA JAHRIYYAH (SWALAH ZA KUNYANYUA SAUTI)

 

Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ameruhusu kwa wale waliokuwa ma-amuma kuisoma Suratul-Faatihah nyuma ya Imaam katika Swalah za jahriyyah, na mara moja alikuwa (صلى الله عليه وآله وسلم), "Akiswali Alfajiri na kisomo kikawa kigumu kwake. Alipomaliza alisema: ((Labda mnasoma nyuma ya Imaam wenu!)). Tukasema: "Ndio hadhdhan[1] Ewe Mjumbe wa Allaah". Akasema: ((Basi Msifanye hivyo isipokuwa [kwa kusoma mmoja wenu] Ufunguo wa Kitabu, kwani hakuna Swalah kwa asiyeisoma))[2]

 

Kisha aliwakataza kusoma katika Swalah za jahriyyah kabisa, na hilo lilitokea wakati,

 

"Alipomaliza Swalah ambayo alikuwa akisoma kwa sauti [katika usimulizi (mmoja) ilikuwa Swalah ya Alfajiri] basi akauliza: ((Je, kuna (yeyote) aliyekuwa akisoma pamoja nami hivi sasa?)) Mtu mmoja akajibu: "Ndio, mimi Ewe Mjumbe wa Allaah". Akasema: ((Mimi Nasema: sasa kwa nini naingiliwa kati katika kisomo changu][3] [Abu Hurayrah alisema]: (Hivyo) watu wakaacha kusoma pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kila anapokuwa anasoma kwa sauti baada ya kusikia hivyo kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) [wakawa wanaendelea kusoma kimya kimya kila anapokuwa Imaam haisomi kwa sauti][4]

 

Pia Akaufanya (صلى الله عليه وآله وسلم) ukimya katika kisomo cha Imaam kuwa ni sehemu katika kukamilisha kumfuata Imaam, kwa kusema: ((Kwa hakika amewekwa Imaam ili apatwe kufuatwa, hivyo anapoleta takbiyr, na nyinyi leteni takbiyr, na anaposoma kaeni kimya))[5] kama alivyofanya kumsikiliza Imaam kuwa kunatosheleza na kisomo nyuma yake, kwa kusema (aliposema): ((Mwenye kuwa na Imaam, basi kisomo cha Imaam huyo ni kisomo chake))[6]. Hii inahusu Swalah za jahriyyah.

 

 

 

 

 

KUWAJIBIKA KUSOMA KATIKA SWALAH ZA SIRRIYYAH (SWALAH ZA KIMYA)

 

Ama katika Swalah za kimya kimya, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwaachilia waendelea kusoma humo. Jaabir alisema: "Tulikuwa tukisoma katika (Swalah ya) Adhuhuri na 'Aswr nyuma ya Imaam katika Rakaa mbili za mwanzo Suratul-Faatihah na Surah nyingine, na katika mbili za mwisho Suratul-Faatihah[7]

 

Lakini, alichukizwa kwa tashwishi na kubabaishwa, kwa kisomo chao pale aliposwali Adhuhuri na Maswahaba akauliza: ((Nani katika nyinyi aliyesoma: "Sabbihisma Rabbikal A’laa" [Suratul-A'laa, 87:1])). Mtu mmoja akajibu: "ni mimi" [sikuwa na kusudio lo lote lile kwa kuisoma ila kheri] Akasema: ((Nilijua kuwa kuna mtu anavutana na mimi kwayo))[8]

 

Na Katika Hadiyth nyingine: "Walikuwa wakisoma nyuma ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), hivyo akasema: ((Mmenibabaisha katika kisomo changu))[9]

 

Akasema: ((Anayeswali huwa ananongo’na na Mola wake, basi aangalie cha kumnongo’neza, wala msisome Qur-aan pamoja wote kwa sauti))[10] 

 

Pia alikuwa akisema: ((Atakayesoma herufi moja katika kitabu cha Allaah atapata hasanah (jema) moja, na kila hasanah moja ni sawa na thawabu kumi, (wala) sisemi 'Alif-Laam-Miym' ni herufi moja, bali Alif ni herufi moja na Laam ni herufi moja na Miym ni herufi moja)) [11]

 

 

[1] Hadhdhan:  kusoma haraka haraka, kwa kukimbilia au kuharakiza.

[2] Al-Bukhaariy katika kijarida, Abu Daawuud na Ahmad. At-Tirmidhy na Ad-Daaraqutwniy wamesema ni nzuri.

[3] Amesema al-Khattabiy: maana yake ameingilia kisomo changu, pia yawezekana ikawa ushindani kwa maana ya kushirikiana na kubadilishana, na maana ya pili ndio iliyokusudiwa hapa kwa sababu ya kuacha Swahabah (رضي الله عنهم) kusoma moja kwa moja, na kama ingelikuwa kusudio ni maana ya kwanza, basi wesingeliacha kusoma, lakini inaonyesha kuwa ni kuingilia kati tu kama ilivyodhihiri.

[4] Maalik, Humaydy, Al-Bukhaariy katika kijarida chake, Abu Daawuud na Mahaamaliy (6/139/1) At-Tirmidhiy amesema ni nzuri, Abu Haatim Ar-Raaziy, Ibn Hibbaan na Ibn Qayyim wamesema kuwa ni Swahiyh, na hadiyth yenye kuipa nguvu –shaahid- katika Hadiyth ya ‘Umar ambayo mwisho wake: sasa kwa nini nashindaniwa Qur-aan?! Haimtoshelezeshi mmoja wenu kisoma cha Imaam wake?! Kwa hakika amewekwa Imaam ili apatwe kufuatwa, basi ataposoma kaeni kimya. Imepokewa na al-Bayhaaqiy katika kitabu ulazima wa kisomo katika Swalah, kama ilivyo katika al-Jaami’ al-Kabiyr (3/344/2)

[5] Ibn Abi Shaybah (1/97/1), Abu Daawuud, Muslim, Abu 'Awaanah na al-Ruwayaaniy katika musnad yake, (24/119/1). Imetolewa katika Al-Irwaa (332,394).   

[6] Ibn Abi Shaybah (1/97/1), Ad-Daraaqutwniy, Ibn maajah, At-Twahaawiy na Ahmad kutoka njia mbali mbali, musnad na mursal. Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema kuwa ina nguvu kama katika Al-Furuu' ya Ibn 'Abdil-Haadiy (48/2). Al-Buswayriy amesema kuwa baadhi ya isnaad zake kuwa ni Swahiyh. Nimeijadili Hadiyth hii kwa kirefu na kuzitafiti njia zake (mbali mbali) za usimulizi katika maandishi kisha katika Al-Irwaa Al-Ghaliyl (Namba. 500)

[7] Ibn Maajah kwa isnaad Swahiyh. Imetolewa katika Al-Irwaa (506)   

[8] Muslim, Abu 'Awaanah na Siraaj.

[9] Al-Bukhaariy katika makala yake, Ahmad na Siraaj kwa isnaad nzuri.

[10] Maalik na al-Bukhaariy katika Af'aal al-'Ibaad kwa isnaad Swahiyh.

 

TANBIHI:

Rai ya uthabiti wa kusoma nyuma ya Imaam katika Swalah za Sirriyah na sio za Jahriyyah, imetolewa na Imaam Ash-Shaafi'y mwanzo, na Muhammad mwanafunzi wa Abu Haniyfah katika usimulizi kutoka kwake ambao umependelewa (zaidi) na Shaykh 'Aliy al-Qaariy na baadhi ya Mashaykh (wengine) wa madhehebu. Pia (ulikuwa) ni msimamo wa Imaam Az-Zuhriy, Maalik, Ibn Al-Mubaarak, Ahmad bin Hanbal, na kundi la Muhaddithiyn na wengineo, na ni mapendeleo ya Shaykhul-Islaam Ibn Taymiyyah.

[11] At-Trimidhiy na Ibn Maajah kwa isnaad Swahiyh. Imesimuliwa pia na Aajuriy katika Aadaab Hamalat al-Qur-aan. Ama Hadiyth: "Mwenye kusoma nyuma ya Imaam mdomo wake utajazwa moto" ni Hadiyth ya uzushi (mawdhwuu) na hii imelezewa katika Silsilat al-Ahaadiyth Adh-Dhwa'iyfah (Namba. 569) Taz. Kiambatisho 5.

Share