Dhambi Za Kutowahudumia Wazazi Na Kuwafanyia Ihsaan

SWALI:

 

Asalam Aleikum

 

Nini hukmu ya mtoto ambaye ana nafasi katika maisha lakini hamuangalii kimaslahi mzazi wake wakati uwezo anao.

 

Kwa maana ingine hana CONTINUITY ya kumsaidia mzazi wake. Anamsaidia siku akipenda. Na wala hana kawaida ya kumjulia HALI hata kwenye simu. Vile vile naomba munipe ile hadithi ya sahaba wa mtume ambaye alishindwa kutoa shahada mpaka ilipodhihiri kuwa alimuudhi mama yake.

 

Wabillahi Taufiq

 


JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukran zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuwatendea wema wazazi. Ni utovu wa nidhamu na adabu kwa mtoto kutowatazama wala kuwatendea wema wazazi wake. Allaah Aliyetukuka Ameonyesha kuwa kuwatendea wema wazazi ni jambo kubwa sana hata Akalitaja baada tu ya kutomshirikisha Yeye, Anasema:

 

Na Mola wako Ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima. Na uwainamishie bawa la unyenyekevu kwa kuwaonea huruma. Na useme: Mola wangu! Warehemu kama walivyonilea utotoni” (17: 23 – 24).

 

Mtu ambaye atawakuta wazazi wake katika uzee kisha asiingie Peponi basi huyo amekhasirika vibaya sana. Watoto hata wakifanya nini hawawezi kulipa fadhila walizofanyiwa na wazazi wao ila wawakute kuwa ni watumwa wawanunue kisha wawaache huru. Ikiwa si hivyo basi hata ukafanya nini huwezi kurudisha ihsani uliyofanyiwa na mzazi, baba na mama. Na mama ana daraja kubwa zaidi. Faida ni kubwa kwa mtu kuwafanyia ihsani wazazi wake kama ilivyokuja katika Hadiyth ndefu ya wale watu watatu waliofungiwa katika pango na kila mmoja akataka msaada wa Allaah Aliyetukuka kwa kuomba kupitia kwa 'amali njema alizofanya. Na kwa wema aliowafanyia wazazi wake Allaah Aliyetukuka Akakubali na kuwapatia takhfifu na kuwafungulia pango hilo. [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na pia khasara ni kubwa maradufu kwa mtu kutowafanyia wema wazazi wake hapa duniani kabla ya Aakhirah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share