'Aaishah (رضي الله عنها): Ndoa Changa Ya Mama Wa Waumini -2

Imetafsiriwa na Naaswir Haamid

 

 

Ndoa Za Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam) Kwa Ulinganifu

 

Kuyaweka yote haya kwenye ulinganifu – kwa matarajio na bila ya haya ya kujitetea – kitu cha mwanzo ambacho mtu lazima akitanabahi ni kwamba ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa ni mke wa tatu wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), sio wa mwanzo. Pamoja na hili, mke wa mwanzo na mke pekee wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa ni Mama Khadiyjah bint al-Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘Anha), ambaye alikuwa mkubwa zaidi yake kwa umri wa miaka kumi na tisa. Alimuoa Khadiyjah wakati akiwa na umri wa miaka arobaini na yeye akiwa na umri wa miaka ishirini na moja[1] – kipindi ambacho kinaweza kuitwa kuwa ni umri wa “kiini cha shahawa” wa mwanamme – na alibaki ndani ya ndoa PEKE yake hadi kifo chake.

Mara tu baada ya kifo cha Khadiyjah, ambapo alikuwa na umri wa miaka arobaini na sita[2], Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alioa mke wake wa pili Sawdah bint Zam’ah. Ilikuwa baada ya ndoa hii ya pili ambapo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuja kufunga ndoa na ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha). Alikuwa ni binti ya Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu), mmoja wa rafiki wa karibu mno na mfuasi wa kujitolea wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘Anhu), alikuwa ni miongoni mwa watu wa mwanzo waliobadili dini kwa kuingia kwenye Uislamu na alitaraji kugandisha mapenzi makubwa yaliyokuwapo baina yake na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa kuunganisha koo zao ndani ya ndoa.

 

Ndoa ya binti ya Abu Bakr, yaani ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) kwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ilifanyika ndani ya mwaka wa kumi na moja wa Utume, kipindi ambacho kilikuwa kiasi ya mwaka baada ya kumuoa Sawdah bint Zam’ah na kabla ya kufanya hijra (kuhama) yake kwenda al-Madiynah (Yathrib). Kama ilivyoelezwa hapo juu, ndoa pamoja na ‘Aaishah bint Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ilitimia kwa tendo la ndoa ndani ya Shawwaal, kipindi ambacho kimekuja baada ya miezi saba ya hijra ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kutoka Makkah kwenda al-Madiynah. Wakati wa ndoa yake kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha), Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa zaidi ya miaka hamsini.

 

Ni vyema ikabainishwa hapa kwamba ndoa ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) ilikuwa ni yenye furaha iliyochupa mpaka kwa pande zote, kama maandiko ya Hadiyth yanavyothibitisha. ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha), alikuwa ni mke wake kipenzi na bikira pekee ambaye amepata kuoa. Baada ya kuhama kwenda al-Madiynah, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alioa idadi inayohesabika ya wake wengine, matokeo yake kukamilisha idadi ya kumi na tano [3]ndani ya maisha yake.

 

Ingawa hatuna muda wa kwenda ndani zaidi kwa kila mmoja wao, (lakini) kila moja ya ndoa hii ilifanywa aidha kwa sababu za kisiasa, kuimarisha mfungamano wa ukoo au kusaidia mwanamke aliye na haja. Ni idadi kadhaa ya wake hao walikuwa ni wajane, wanawake walio wakubwa zaidi au waliotelekezwa, na hivyo walikuwa na haja ya maskani. Kwa kuongezea, itambuliwe kwamba mkusanyo huo huo wa Hadiyth za maandiko ya (Imaam) Muslim zinatueleza kwamba ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anha) alikuwa na umri wa miaka tisa tu wakati wa ndoa hiyo ya amri iliyotoka kwa Mungu:

 

 

Amesimulia ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha), Mjumbe wa Allaah alisema (kuniambia): “Umeoneshwa kwangu mara mbili ndani ya ndoto (zangu). Kuna mtu alikuwa akikubeba ndani ya kitambaa cha hariri na kuniambia: ‘Huyu ni mke wako.’ Nikakikufungua, na kumuangalia, ilikuwa ni wewe. Nilijiambia, ‘kama ndoto hii inatokana na Allaah, Ataifanya kuwa ni kweli.” (Swahiyh Al-Bukhaariy, Juzuu ya 7, Kitabu 62, Nambari 15).

 

Hivyo, kama ilivyo kila kitu anachofanya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kulikuwa na hekima nyuma yake na mafunzo ya kujifunza kutokana nacho. Kwa mfano hekima zilizo nyuma ya matokeo kama hayo, zinatudhihirishia uongofu kwa msingi wa ustaarabu wa mwanaadamu, kuharibu viwango maradufu vya wanafiki wasio waongofu kutokana na dini nyengine ambazo zinakejeli Uislamu na zaidi ya hayo. Lakini zaidi kuhusiana na mada hiyo fuatilia hapa chini...

 

 

 

 


[1] Kauli nyingi zinasema kuwa  Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimuoa Mama Khadiyjah (Radhiya Allaahu ‘anha) akiwa yeye ana miaka 25, na hivyo tofauti  kati yao ilikuwa ni miaka 15 na si 19. (Mfasiri)

[2] Kauli yenye nguvu kuunganisha na maelezo yaliyotangulia ni kuwa hapa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa na umri wa miaka 50. (Mfasiri)

[3] Mwandishi hapa kawajumuisha wake zake na wanawake wanne ambao ni masuriya na aliopewa zawadi ambao sheria ilimruhusu kuishi nao kama wake zake akiwemo Mama Mariyah Al-Qibtwiyah (Radhiya Allaahu ‘anha) aliyemzalia mwanawe Ibraahiym aliyefariki akiwa mdogo. (Mfasiri)

 

 

Itaendelea inshaAllaah...

 

 

Share