Swafiyyah Bint Abdil-Muttwalib (رضي الله عنها)

 

Mwanamke Wa Mwanzo katika Uislam Kumuua Mshirikina

 

 Muhammad Faraj Salim As-Sa’y (Rahimahu Allaah)

 

Alhidaaya.com

 

 

 

 

Bibi Swafiyyah binti Abdul Muttalib (Radhiya Allaahu ''anhaa) shangazi lake Mtume wa Allaah (SwaAllaahu Allaahu 'alayhi wa Sallam) alikuwa mwingi wa hekima, hodari wa kuyapima mambo, shujaa na mkali. Hata wanaume walikuwa wakipanga na kupanguwa huku wakiwaza na kufikiri kabla ya kuamua kujadiliana au kupambana naye.

Anajulikana kuwa ni mwanamke wa mwanzo kumuua mshirikina kwa ajili ya kuwahami wanawake wenzake wa Kiislamu.

 

 

Nasaba Yake

 

Baba yake ni Abdul Muttalib bn Hashim babu yake Mtume wa Allaah (SwaAllaahu Allaahu 'alayhi wa Sallam) aliyekuwa kiongozi wa Makureshi mwenye kutiiwa. Mama yake Bi Swafiyyah ni Halah binti Wahab dada yake Aminah binti Wahab mama yake Mtume wa Allaah (SwaAllaahu Allaahu 'alayhi wa Sallam).

Mumewe wa mwanzo aliyefariki dunia akiwa naye alikuwa Al Haarith bin Harb ndugu yake Abu Sufyaan bin Harb mkuu wa kabila la Bani Umayyah.

Mume wake wa pili alikuwa Al ‘Awwaam bin Khuwaylid ndugu yake Bi Khadijah binti Khuwaylid (Radhiya Allaahu ''anhaa) mke wa mwanzo wa Mtume wa Allaah (SwaAllaahu Allaahu 'alayhi wa Sallam) na mama wa mwanzo wa Waislamu.

Mume wake wa pili Al ‘Awwaam bin Khuwaylid alipofariki dunia alimuacha akiwa na mtoto mdogo wa kiume Az Zubayr bin Al ‘Awwaam (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyesilimu pamoja na mama yake akiwa na umri wa miaka minane.

Az Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa sahibu mpenzi wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) aliyesema juu yake:

"Kila Mtume anaye sahibu, na sahibu yangu ni Az Zubayr."

Na akasema:

"Twalhah na Az Zubayr sahibu zangu Peponi."

 

 

Ulezi Wake

 

Bi Swafiyyah (Radhiya Allaahu 'anhaa) alimlea mwanawe Az Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhu) malezi magumu na ya shida. Mchezo wake ulikuwa ni kutupa mikuki, kuchonga mishale na kutengeneza pinde.

Alikuwa akimtia vishindo na kumpeleka sehemu zinazotisha na za hatari. Na anapoingiwa na hofu au uoga alikuwa akimpiga kipigo chenye kuumiza. Na kwa ajli hiyo watu wake walikuwa wakimlaumu.

Mmoja katika shangazi zake aliwahi kumuambia:

"Si hivyo anavyopigwa mtoto. Unampiga mfano wa mama anayemchukia mwanawe. Hicho si kipigo cha kumlea mtoto."

Bi Swafiyyah akamjibu kishairi akimuambia: "Anayesema namchukia hajasema kweli. Nampiga apate akili, ayashinde majeshi makali na afuzu kikweli."

 

 

Kusilimu Kwake

 

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) alipopewa utume, alitakiwa aanze kwa kuwaonya watu wake na kuwapa bishara njema, na kuwalingania. Aliwakusanya jamaa zake wanaotokana na tumbo Abdul Muttalib wanawake kwa wanaume, wadogo kwa wakubwa na kuwahutubia ifuatavyo:

"Ewe Fatima binti Muhammad. Ewe Swafiyyah binti Abdul Muttalib. Enyi wana wa Abdul Muttalib. Hakika mimi similiki chochote kwa ajli yenu mbele ya Allaah."

Kisha akawataka wamuamini Allaah Mmoja na kuamini ujumbe aliokuja nao.

Wakakubali miongoni mwao waliokubali na wakakanusha waliokanusha kwa upotofu wao. Na Bi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ''anhaa) alikuwa miongoni mwa kundi la mwanzo kumuamini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) na kumsadiki.

 

 

Hijra Yake

 

 

Kwa hivyo Bi Swafiyyah (Radhiya Allaahu 'anhaa) pamoja na mwanawe Al Zubair bin Al ‘Awwaam (Radhiya Allaahu 'anhu) wakawa miongoni mwa kundi la mwanzo kujiunga na msafara huu ulioieneza nuru kila pembe ya dunia, na wakapata tabu nyingi kama walivyopata tabu wenzao wote waliotangulia kuingia katika dini hii tukufu tokea siku za mwanzo.

Makureshi waliwaonjesha Waislamu kila aina ya mateso na adhabu, mpaka pale Allaah (Subhanahu wa Ta'aalaa) alipomtaka Mtume wake (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) aondoke Makkah yeye pamoja na wafuasi wake na kuhamia Madinah. Na hapo ndipo Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ''anhaa) alipoitikia mwito huo kuuhama na kuuacha nyuma mji anaoupenda, Makkah, na kuacha nyuma kila anachokipenda katika mji ule mtukufu na kila kinachomkubusha utoto wake na ujana wake.

 

 

Jihaad Yake

 

 

Juu ya kuwa umri wake ulikaribia miaka sitini, lakini Bibi huyu mtukufu (Radhiya Allaahu ''anhaa) alikuwa na misimamo madhubuti isiyosahaulika mbele ya adui wa Allaah katika kupigana Jihaad.

Alikuwa akitoka pamoja na wanawake wenzake kuwasaidia Waislamu wanaopigana Jihaad kwa kuwapelekea maji na kuwachongea mikuki na mishale pamoja na kutengeneza pinde zinapokatika. Wakati huo huo akiwa karibu na vita aliweza kupata habari za mtoto wa ndugu yake Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa Ssallam) anapokuwa vitani pamoja na habari za ndugu yake Hamzah bin Abdul Muttalib (Radhiya Allaahu anhu) na pia habari za mwanawe Az Zubayr bin Al ‘Awwaam (Radhiya Allaahu 'anhu) na juu ya yote hayo aliweza kujuwa juu ya maendeleo ya vita vinavyopiganwa kwa ajili ya kuinusuru dini ya Allaah.

Na siku ile alipowaona Waislamu wakikimbia vitani huku majeshi ya makafiri yakikaribia kumfikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) na kumuua, Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ''anhaa) aliruka kama simba jike anavyoruka anapowaona wanawe wakishambuliwa. Akamnyang'anya mkuki mmoja wa waliokuwa wakikimbia uwanja wa vita, akaanza kuelekea mbele kuwakabili maadui huku akiwatolea ukali Waislamu akiwaambia:

"Ole wenu! Mnashindwa kusimama na Mtume wa Allaah?

Na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) alipomuona akielekea katika uwanja wa vita aliogopa asije akamuona ndugu yake Hamzah (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyeuliwa na mwili wake kukatwa katwa vibaya. Akamuambia mwanawe Az Zubayr:

"Mzuwie mama yako ewe Zubayr, mzuie mwanamke ewe Zubayr."

Az Zubayr (Radhiya Allaahu 'anhu) akamuendea na kumuambia:

"Rudi ewe mama yangu, rudi."

Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu 'anhaa) akasema:

"Nipishe huko."

Akasema:

"Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) anakuamrisha urudi."

Akauliza:

"Kwa nini? Nimekwishapata habari kuwa ndugu yangu ameuliwa na kukatwa katwa vibaya. Yote hayo kwa ajili ya Allaah."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) akasema:

"Muache apite ewe Zubayr."

Akamruhusu.

Baada ya vita kumalizika Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ''anhaa) alisimama mbele ya maiti ya ndugu yake Hamzah (Radhiya Allaahu 'anhu) huku akiuangalia mwili wake uliokatwakatwa vibaya huku akimuombea maghfira na kusema:

"Yote haya kwa ajli ya Allaah. Nimeridhika na kile alichokitaka Allaah kiwe, na ninategemea malipo mema kutoka Kwake InshaaAllaah."

Huu ulikuwa msimamo wa Bibi Swafiyyah binti Abdul Muttalib (Radhiya Allaahu ''anhaa) siku ya vita vya Uhud.

 

 

Vita Vya Khandaq

 

 

Ama msimamo wake siku ya vita vya Khandaq ndani yake mna kisa chenye kusisimua sana.

Kawaida ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) ilikuwa kila anapokwenda vitani akiwaweka wanawake na watoto na wazee na vilema ndani ya ngome akihofia mtu asiwaendee kinyume akawazungukia na kuwateka.

Siku ya vita vya Khandaq aliwaweka wake zake na shangazi zake pamoja na wanawake wengine wa Kiislamu ndani ya ngome ya Hassan bin Thaabit (Radhiya Allaahu 'anhu) aliyeirithi kutoka kwa baba yake. Na ngome hii ilikuwa madhubuti zaidi. Haivunjiki kwa urahisi wala haiingiliki kwa wepesi. Na Waislamu walipokuwa wameshughulika na vita wakipambana na Makureshi na wanaowaunga mkono, waliwasahau wake na watoto wao kwa kujishughulisha na maadui  hao.

Alfajiri ilipoanza kuingia, na waliomo ndani ya ngome walikuwa bado wamelala, Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ‘'anhaa) aliyekuwa yu macho wakati huo aliona mfano wa mwili ukitaharuki huku na kule ndani ya ngome yao. Akausogelea mwili ule kimya na pole pole mpaka alipoukaribia akaona kuwa ni Myahudi aliyefanikiwa kuingia ndani ya ngome. Alimfuata huku na kule bila Myahudi kuhisi, na hatimaye Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ‘'anhaa) alitambua kuwa huyo ni mpelelezi aliyetumwa na Mayahudi kuja kupeleleza iwapo ndani ya ngome mna wanaume wenye kuilinda au ni ngome iliyojaa wanawake iliyoachwa bila ya ulinzi.

Bibi Swafiyyah (Radhiya Allaahu ‘'anhaa) akawa anajiuliza:

"Hawa Mayahudi wa Bani Quraydhah ndio walioivunja ahadi iliyokuwepo baina yao na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) kisha wakajiunga na Makureshi dhidi ya Waislamu. Na hivi sasa hapana mwanamume hata mmoja wa kutuhami, kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘'alayhi wa sallam) pamoja na Waislamu wote wapo vitani. Akiweza adui wa Allaah huyu kuwafikia watu wake na kuwajulisha kuwa humu ndani tumo wanawake watupu, watatuteka. Na hilo litakuwa ni balaa kubwa kwa Waislamu."

Hapo hapo akaamua kujifunga uzuri kitambaa usoni na kuzibana vizuri nguo mwilini mwake, kisha akaokota gongo na kuanza kumnyemelea adui yule wa Allaah kwa tahadhari mpaka alipomkaribia sana. Alipokuwa na uhakika kuwa keshamkaribia vya kutosha na kumkalia vizuri, akanyanyua gongo lake juu na kuliangusha kwa nguvu zake zote, akampiga nalo kichwani na kumuangusha chini. Akaendelea kumpiga mpaka alipomuona hawezi tena kuvuta pumzi, kisha akatoa kisu chake na kumkata kichwa kisha akakichukua kichwa na kukitupa juu ya paa, kikabiringitia na kuangukia mbele ya Mayahudi waliokuwa nje wakimsubiri mwenzao.

Walipokiona kichwa cha mwenzao kimekatwa wakasema:

"Tulijuwa sisi kuwa Muhammad hawezi kuwaacha wanawake na watoto peke yao bila ya ulinzi madhubuti wa wanaume."

 

 

Kufariki Kwake

 

 

Allaah awe radhi naye Bibi Swafiyyah. Alikuwa shujaa na jasiri kikweli, na historia imekwishaandika kuwa yeye ni mwanamke wa mwanzo kumuua mshirikina kwa ajili ya dini ya Islamu.

 

Alifariki dunia wakati wa ukhalifa wa ‘Umar bin Khattaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) akiwa na umri wa miaka sabini na tatu, Na ‘Umar (Radhiya AAllaahu ‘anhu) ndiye aliyeongoza Swalah ya jeneza, na akazikwa bibi huyo katika makaburi ya Al Baqi'y.

 

 

 

Share