020-Sifa Ya Swalah Ya Mtume (Swalla Allaahu 'Alayhi Wa Aalihi Wa Sallam): Ruhusa Ya Kusoma Al-Faatihah Pekee

 

RUHUSA YA KUSOMA AL-FAATIHAH PEKEE

 

Mu'aadh bin Jabal (رضي الله عنه) alikuwa akiswali 'Ishaa (ya mwisho) pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), kisha akirudi huwaswalisha wenzake. Usiku mmoja, aliporudi aliwaswalisha, na akaswali kijana mmoja katika watu wake [wa Banu Salamah aliyeitwa Sulaym], lakini (Swalah) ilipokuwa ndefu kwa yule kijana, [alijiondokea] na akaswali [pembezoni mwa Msikiti]. Kisha akatoka na kushika ungwe za ngamia wake na akajiondokea. Mu'aadh (رضي الله عنه) Alipomaliza kuswali alielezwa yaliyotokea, akasema: "Bila shaka ana baadhi ya unafiki! Nitamweleza Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alivyofanya". Na yule kijana naye akasema: "Nami nitamweleza Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alivyofanya". Kulipopambazuka, walikuja kwa Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), basi Mu'aadh akamweleza yale aliyoyafanya yule kijana. Kijana akasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Yeye hukaa na wewe muda mrefu, kisha anarudi na kuturefushia". Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema: ((Je, wewe ni mfitini ewe Mu'aadh?!)). Na akasema kumwambia yule kijana([1]): ((Vipi  unafanya unaposwali ewe mtoto wa ndugu yangu?)) Akamjibu: "Nasoma Kifungulio cha Kitabu, kisha namuomba Allaah Pepo, na najikinga Kwake kutokana na moto. Na hakika mimi sielewi dandanah([2]) yako wala dandanah ya Mu'aadh!" Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwambia: ((Hakika Mimi na Mu'aadh tuko katika hayo hayo mambo mawili, au mfano wake)).  Msimulizi alisema: "Yule Kijana akasema: "Lakini Mu'aadh ataelewa watakapokuja watu wakapewa habari kwamba adui wamefika". Msimulizi akasema: "(Hivyo) Adui wakaja na yule kijana akafa shahidi. Baada ya hapo, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema kumwambia Mu'aadh: ((Amefanya nini yule aliyejadiliana nami na wewe?)). Akasema: "Ewe Mjumbe wa Allaah! Amemsadikisha Allaah, nami sikuwa mkweli, amekufa shahidi".([3])

 





[1]  Asili ni 'Yule Kijana".  

[2] "Dandanah" ni mtu anaposema maneno kwa madaha na kusikiwa mvumo wa maneno yake lakini hayafahamiki. Ni karibu kidogo na kunong'ona. (An-Nihaayah)

[3]  Ibn Khuzaymah katika Swahiyh yake (1634) na Al-Bayhaqiy kwa isnaad Swahiyh. Na pahala penye ushahidi kutokana na Hadiyth pako katika Abu Daawuud (Namba 758, Swahiyh Abu Daawuud) na asili ya kisa chenyewe kipo katika as-Swahiyhayn (Al-Bukhaary na Muslim). Nyongeza ya mwanzoni iko katika usimulizi wa Muslim. Ya pili iko katika Ahmad (5/74), na ya tatu na ya nne katika Al-Bukhaary. Pia mlango wa hizi, ni Hadiyth iliyotolewa na Ibn 'Abbaas kwamba Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) aliswali Rakaa mbili ambazo hakusoma ndani yake isipokuwa Kifungulio cha Kitabu (Al-Faatihah) pekee". Imesimuliwa na Ahmad (1/282), Al-Haarith bin Abi Usaamah katika musnad yake (Uk. 38 kutoka zawaaiyd yake) na Al-Bayhaqiy (2/62) kwa isnaad dhwa'iyf. Nilikuwa nimesema kuwa Hadiyth hii ni nzuri katika chapa  zilizopita, kisha ikanibainikia kuwa nilikuwa nimekwenda kombo, kwa sababu Hadiyth  yenyewe inazunguka kwa Handhwalah Ad-Dawsiy ambaye anaeleweka kuwa ni dhaifu, na sielewi kwa nini sikuweza kugundua hili?! Huenda nilifikiri kuwa ni mtu mwengine. Hata hivyo, Sifa zote ni Zake Allaah Aliyeniongoza kuweza kufikia kutambua kosa langu, na ndio maana nikakimbilia kuisahihisha katika chapa. Kisha Allaah Akanisawazisha kwa kuniruzuku Hadiyth hii bora ya Mu'aadh ambayo inahusisha yaliyoashiriwa katika Hadiyth ya Ibn 'Abbaas. Sifa zote ni Zake Allaah Ambaye kwa Neema Zake yanatimia mema.

Share