Nimeoa Mwezi Wa Pili Lakini Mke Hataki Kuingia Katika Kitendo Cha Ndoa

SWALI:

Asalaam Alaykum,

Kwanza napenda kumshukuru ALLAH, kwa kukupeni ujasiri kuanzisha hii website ambayo inawasadia waislamu, kutatua matatizo yao katika kuzifuata vyema sheria za KIISLAM.

Huu ni mwezi wa pili sasa tangu nioe, lakini sijaweza kufanya tendo la ndoa na mke wangu, kila ninapotaka kufanya, anakuwa hataki, na anaogopa, na sitaki kumlazimisha kabisa, nipo namvumilia, lakini sasa maji yamefika shingoni, anasema tuite wazee, lakini mimi siwezi kuita wazee, nilimwambia tukae mpaka tutakapoweza kufanya (tendo la ndoa) lakini sasa ni muda mrefu (miezi miwili) bado hataki kufanya tendo la ndoa, na mimi naona aibu kwenda kuwazungumzia wazee jambo hili, je nifanyeje? 

 


JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako hilo kuhusu mke kukataa kuingiliwa katika kitendo cha ndoa. Ama kuhusu hilo huenda ya kuwa yapo mengi ambayo hukutueleza ambayo yangetupatia sisi fursa na nafasi nzuri ya kuweza kukusaidia kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo hayo machache uliyotuambia tunaweza kukuuliza na majibu ya kutoka kwako yakatusaidia kukusaidia wewe.

Mwanzo ni kuwa si jambo la kawaida kwa msichana wakati anapokwisha kuolewa kukataa jimai ila kunapokuwepo na sababu. Na hizi hapa chini huenda zikawa ni miongoni mwazo:

1.      Huenda hakupata kutoka kwa wazazi malezi ya kijinsiya na jinsi kumtekelezea mume haki zake.

2.      Huenda ameingishwa hofu ya kuwa kitendo hicho ni cha dharubu na msichana hupata shida pamoja na kutokwa na damu na kuumia.

3.      Huenda ikawa pia hujamchukua kwa upole hivyo hisia zake zikaenda katika yale aliyoyasikia.

4.      Huenda msichana hakutaki lakini amelazimishwa na wazazi pamoja na kutolewa radhi ikiwa hatakubali.

5.      Huenda ikawa msichana ametembea na mvulana mwengine kabla ya harusi, hivyo anaogopa aibu na hataki kuwavunja wazazi wake.

6.      Huenda akawa ametahiriwa kabisa, kwani kufanywa hivyo kunaondoa matamanio ya mwanamke.

Hizi ni baadhi ya sababu ambazo humfanya msichana akatae tendo la ndoa. Katika maelezo hayo lau tutapata baadhi ya majibu kutoka kwako hata wewe mwenyewe kujijibu itakupatia ufumbuzi mzuri sana na kutatua kitendawili hicho. Nukta ya kwanza, wewe kama mume unamjuaje msichana huyo? Je, msichana ni yule aliyeshika Dini kuanzia mwanzo au ni vipi? Ikiwa umepata maelezo muruwa kutoa shaka hiyo inabidi tuende katika nukta ya pili.

Je, msichana kwa ridha yake amekutaka au amelazimishwa kuingia katika ndoa hiyo? Ikiwa amelazimishwa na labda ana mpenzi mwengine mtasumbuana na ni afadhali utake mahari yako yarudishwe ili upate kutafuta mke mwengine. Na ikiwa msichana mwenyewe hakupata malezi ya kijinsia au amepata lakini kwa kiwango kidogo itabidi sasa wewe ndio ucheze duru hiyo ya kumuelimisha pole pole na kwa ulaini kuhusu hilo. Pia unaweza kumpatia vitabu vya Kiislam kama kitabu hiki:

Zawadi Kwa Wanandoa

kuhusu penzi la ndoa afahamu kuwa ni jambo la kimaumbile wala hakuna shida yoyote anayopata msichana katika hilo.

Umueleze ni kwa ajili ya kufanya hivyo ndio sisi tumezaliwa na hatuna budi kufuata kanuni alizoweka Muumba ili kizazi cha wanadamu kipate kuendelea. Mchukue kwa utaratibu kwa maelezo ambayo ni kama unamuelezea mtoto mdogo. Jaribu sana kumtoa hofu na kumuelezea kuwa hakuna tatizo lolote na kuwa habari hizo ni porojo tupu. Jipambe usiku mnapoingia chumbani kwa kuoga na kujipaka manukato, huenda naye akapata hisia za kukutamani pia 

Tatizo linakuja ikiwa ametahiriwa kabisa kwani hata akiwa atakubali kufanya tendo la ndoa huwa hana raha.

Ikiwa umefanya yote hayo na hakuna natija yoyote ile iliyo nzuri kutakuwa hapana budi isipokuwa kuwaita wazazi wake ni kuwaeleza kwani hutaweza kuishi maisha katika hali hiyo. Na katika suala hilo hakuna hayaa kwani kuona hayaa ndio utazidi kuumia, tena kwa kiasi kikubwa sana.

Tunakutakia kila la kheri na Allaah Aliyetukuka Akuondolee tatizo hilo na muishi na mkeo kwa wema, ihsani na fanaka.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share