Mume Anamuingilia Akiwa Hedhini Aoge Ghuslu La Janabah Au Aoge Akimaliza Hedhi?

SWALI LA KWANZA:

Mume wangu ana tabia ya kuniingilia wakati nikiwa katika siku zangu kwani huwa nachelewa kumaliza huwa nachukua siku saba yeye anaziona nyingi, nini hukmu yake na huwa nashindwa sijui nikoge josho gani na wakati gani, kama nikoge janaba au nikimaliza hedhi nikoge vyote viwili?
 

SWALI  LA PILI:

Assalaam alaykum, ninavyoelewa kuwa Qur'an imetueleza kuwa tusiwakaribie pindi wake zetu wanapokuwa katika siku zao za Hedhi. Lakini vipi anapokuwa katika siku hizo na yeye anajisikia kuingiliwa na kukutaka hata utumie mkono    ili kumuondolea hamu iliyomjaa kwa wakati huo je ina juzu kwa mume kumkamilishia mkewe matakwa yake hayo katika kipindi hiki?. Kama jawabu hairuhusiwi naomba maelezo kwanini?.

Kama jawabu ndio naweza kumkamilishia basi naomba kujua pia yafuatayo:

Nini hikma ya kutumika neno "tusiwakaribie"  huenda tusifanye mapenzi yoyote yale kama kuchezeana na kumaliziana haja bila kufunja sheria zake Allah(SW)

Pia kuna itikadi zetu za kibinadamu kuwa unapofanya mapenzi naye hata kwa kutumia mkono katika kipindi hicho cha Hedhi basi ni kutiana NUKSI NA MABALAA kimaisha. Je kuna ukweli wowote unaoandamana na kauli kama hizi kama aya, hadithi au kisa chochote wakati wa Mtume(S.A.W)

Wabillahi taufiiq

 

 

 


 

 

AlhamduliLlaah - Himdi Na Sifa Zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

JIBU LA SWALI LA KWANZA:

Shukrani sana kwa muulizaji kuhusu swali hili nyeti. Na hakika hii inatuonyesha jinsi gani tunavyokwenda kombo kabisa na mafundisho ya Dini yetu. Ni makosa kwa mwanaume kumuingilia mkewe wakati yupo katika damu ya mwezi au katika damu ya nifasi (ya uzazi) kwa nasw ya Qur’an na Hadiyth. Allah  Anasema:

“Na wanakuuliza kuhusu hedhi. Waambie huo ni uchafu (ugonjwa). Basi jitengeni na mwanamke wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watwahirike. Wakisha twahirika basi waendeeni Alivyokuamrisheni Allaah. hakika Allah Huwapenda wanaotubu na Huwapenda wanaojisafisha”  (2: 222).

Aya hii ipo wazi kuwa mwanamke haifai kuingiliwa wakati huo na atakayefanya, amefanya jambo la dhambi na inabidi atubie kwa Allah kwa kutolirudia kosa hilo.

Utafiti wa kisayansi umethibitisha kuwa wakati huo mwanzo mwanamke anakuwa ni kama mgonjwa na kumuingilia kunamuumiza na ni madhara kwa mume  na mke mwenyewe, kwani vidudu huenda vikaingia na mwanamke akakosa kuzaa kabisa na pengine mume mwenyewe kupata ugonjwa kwani damu huwa imebeba vidudu vingi.

Siku saba sio nyingi ikiwa ana subira nasi tumeamriwa kuwa na subira na hakuna haja ya kufanya haraka kisha kukawa na madhara makubwa kwa mmoja wenu au nyote wawili. Tofauti na Dini nyinginezo ambazo zinawakataza wanandoa kulala kitanda kimoja na kula pamoja, Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha kuwa mume anaweza kukumbatiana na mkewe, kulala kitanda kimoja, kumpiga busu na kumshika shika ikiwa ana hamu kubwa isipokuwa kufanya tendo la ndoa.

Kwa ufupi, Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)    amesema unaweza kufanya na mkeo kila kitu isipokuwa kumuingilia.

Inabidi dada yetu amueke chini mumewe na ampatie nasaha mumewe ili asirudie jambo hilo ambalo limekatazwa na waweze kufanya mambo mengine ila kuingiliana.

Na ikiwa ameingiliwa kwa sababu hana Swalah anaweza kuoga josho moja tu anapoingia katika Twahaarah yake au akipenda kuoga josho la janaba atafanya hivyo na kisha akiingia katika Twahaarah yake ataoga tena, na hii ya pili ni nzuri zaidi.    

 JIBU LA SWALI LA PILI: 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) :

((يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْمَحِيضِ قُلْ هُوَ أَذًى فَاعْتَزِلُواْ النِّسَاء فِي الْمَحِيضِ وَلاَ تَقْرَبُوهُنَّ حَتَّىَ يَطْهُرْنَ فَإِذَا تَطَهَّرْنَ فَأْتُوهُنَّ مِنْ حَيْثُ أَمَرَكُمُ اللّهُ إِنَّ اللّهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ))

((Na wanakuuliza juu ya hedhi. Waambie, huo ni uchafu. Basi jitengeni na wanawake wakati wa hedhi. Wala msiwaingilie mpaka watahirike. Wakisha tahirika basi waendeeni Alivyokuamrisheni  Allah. Hakika Allah Huwapenda wanaotubu na huwapenda wanaojisafisha)) [Al-Baqarah:222]

Maana ‘tusiwakaribie’ ni kutofanya nao tendo la ndowa.

 Si kama wanavyofanya baadhi ya watu kwa kutokula nao au kulala nao kitanda kimoja na mengineyo.  Na sio sahihi kuweka itikadi hiyo kuwa kunatokea balaa na nuksi katika hiyo ya mwanamke, hizo ni kauli za kijahiliyyah haitupasi kuzifuata.

 Kwa muktadha huo inajuza kwa mume kumtoshelezea mkewe matakwa yake ya kumpunguzia matamanio ya kimwili katika siku za hedhi, kwa ushahidi wa hadith ifuatayo:

Amesimulia Bibi Aisha "Alikuwa Mtume [Salallahu alaihi wasalam] akiniamuru nijifunge vizuri nguo yangu kiunoni kisha akinikumbatia hata nikiwa katika hedhi"

 Hii inaonesha pia sehemu zingine za mwili zilikuwa wazi wakati akimkumbatia.  

Pia katika hadith nyingine iliyosimuliwa na Muslim ikifafanuwa aya ya 222 ya surat Baqara, walimuuliza Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  ipi kinachoruhusiwa mume kwa mkewe anapokuwa katika? Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akajibu "Fanyeni kila kitu ila tendo la ndowa" kwa maana hiyo inajuzu yote yatakayoweza kumstarehesha mke kwa njiya za halali kwa wakati huo wa hedhi

Na Allah Anajua zaidi

 

Share