Nikipokea Zaidi Ya Nilivyokopesha Itakuwa Ni Riba?

SWALI:

 

Assalam Alaikum;

 

Kama nimemkopesha mtu halafu siku ya kurudisha akaniregeshea zaidi ya nilivyomkopa bila ya mimi kumwambia kuwa nataka anilipe na interest, Au saa ile ya kumkopa aniambie kuwa akirudisha atanilipe zaidi ya ninavyompa kwa hiari yake, nikipokea itakuwa ni haram kwangu.

Wassalam.

 


JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu nyongeza unayopata kwa mdeni wako.

 

Riba kwa kawaida inajulikana na kila mmoja na haina utata wowote. Riba ina maana ya ziada anayopewa mdeni anapolipwa deni lakekwa mapatano waliyopatana kuanzia awali ya mkopo. Mfano ni mtu anakukopesha shilingi au dola 1000 ukirudisha deni hilo utalipa 1050 ikiwa utakuwa nazo au laa. Huu ni mkataba ambao mnapatana kwayo baina ya pande mbili ima kwa maandishi au kwa mdomo.

 

Uislamu umeharamisha unyama na ubepari huu ambao nia yake ni kuzidi kumdhoofisha masikini na kumfanya tajiri awe tajiri. Sheria na kanuni za Uislamu zina ubinadamu na utu na zinajali sana maslahi ya kila mwanadamu na hasa mnyonge. Ndio Khaliyfah wa kwanza, Abu Bakr asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu 'anhu) alisema katika hotuba yake ya kwanza: "Dhaifu kwangu atakuwa na nguvu mpaka nimpatie haki yake". Kunapokuwa na usaidizi kama huo basi jamii na dola hiyo ni lazima itapata ufanisi wa hali ya juu.

 

Tukirudi katika swali lako ni kuwa umemkopesha nduguyo na hakukuwa na mapatano yoyote ya haramu kama kumwambia ukirudisha ulete zaidi pesa kadhaa. Katika hali hiyo uliyosema hakuna ubaya wowote wa kuchukua nyongeza hiyo kwani ameitoa kwa hiari yake bila wewe kuitaka au kuiuliza, lakini ni bora uhakikishe naye kuwa wewe hukuitaka nyongeza hiyo na pia uhakikishe kuwa yeye yu radhi kuitoa hiiyo nyongeza.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share