Imaam Akiomba Du’aa Anapokuwa Katika Mimbari Inapasa Kunyanyua Mikono?

 

Imaam Akiomba Du’aa Anapokuwa Katika Mimbari Inapasa Kunyanyua Mikono?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Ikiwa imamu yuwatoa dua kwa jumla hatufai kuomba kwa matumbo ya mikono yetu twafaa tuitikie amin basi bila ya kunyanyua mikono? Sababu inasemwa kuwa  ile huwa ni dua ya jumla na haipaswi kunyanyua mikono. Je hivi ni sawa.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Swali lako haliko wazi na dhahiri kama inavyohitajika ili tuweze kukujibu kama inavyotakiwa. Hili huwa linatupatia usumbufu kwani inabidi tuanze kufikiria ulikuwa unataka kuuliza lini.

 

Tunawaomba waulizaji maswali waulize maswali yalio wazi ili kusiwe na usumbufu wa kuyarudisha kwa waulizaji kwa ajili ya kupata ufafanuzi.

 

 

Inaonekana kama muulizaji anauliza kuhusu du'aa anayotoa Imaam wakati yuko juu ya mimbari katika Swalaah ya Ijumaa. Inafaa tufahamu kuwa Imaam kutoa du'aa wakati huo ni Sunnah kwa sababu ya kufanya hivyo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Hii ni kwa mujibu wa Hadiyth ya Sahl bin Sa'd (Radhwiya Allaahu 'anhu) aliyesema: "Sikumuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akinyanyua mikono yake kabisa akiwa anaomba juu ya mimbar wala sehemu nyengine, lakini nilimuona akisema hivi, na akaashiria kwa kidogo chake cha shahada" [Abu Daawuwd].

 

Hivyo Imaam aweza kuomba du'aa ndani ya khutbah bila kunyoosha mikono yake na Maamuma ni hivyo hivyo waweza kuitikia ndani ya nyoyo zao bila kunyoosha mikono yao.

 

Ama ikiwa ni baada ya Swalaah za kawaida basi Sunnah ni kuwa Imaam haleti du'aa na Maamuma wakaitikia,  bali kila mmoja atasoma uradi uliofundishwa katika mafunzo Swahiyh ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘layhi wa aalihi wa sallam) na kisha baada ya kuswali Swalaah ya Sunnah mtu anaweza kumuomba Allaah ('Azza wa Jalla)   kwa anachotaka kipekee.

 

 

Na sehemu bora kabisa za kuomba du’aa tulishataja katika majibu mengine, nazo sehemu hizo ni katika wakati mtu anaposujudu ndani ya Swalaah, au wakati anapomaliza At-Tashahhud na kabla hajatoa salaam.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share