Zilzalah (Tetemeko La Ardhi) Na Mafunzo Tunayopata

Zilzalah (Tetemeko La Ardhi) Na Mafunzo Tunayopata

Alhidaaya.com

 

 

Maisha ya dunia sio chochote bali ni starehe ya muda tu na yaweza kukatika ghafla bila ya kuletewa taarifa. Tunaamka tukilala tukiwa ni wenye kusindikiza wazee bali hata vijana wangali wakiwa na umri mdogo kwenye malazi ya milele ya maisha ya Barzakh.

 

Zipo njia nyingi za kukatika maisha haya kama vile ajali, maradhi na mauaji. Hata hivyo, kuna aina nyingine ambayo kwa karne mbili hizi zilizopita, imepamba moto. Ni hii ardhi yetu tunayoringa nayo kushindwa kabisa kuhimili madhambi yetu yaliyopindukia mipaka. Hapo tunaona kimbunga, zilzazala (tetemeko la ardhi), kiwango cha juu cha joto au baridi kali na kadhalika.

 

Ardhi ya China ni mfano mzuri wa kuwazindua ndugu zetu wa Kiislam. Hakika kuna mengi ya kujifunza kwa Waislam kutokana na tetemeko lililotokea tarehe 12 Mei, 2008 huko China.  Maisha ya watu zaidi ya elfu yalipotea ghafla bila ya matarajio. Maelfu walipoteza viungo ambavyo kina dada wakivipigia mnada bure kabisa. Maelfu ya matajiri waliokuwa wakitakabbar kwa utajiri, siha na neema aliyowapa Allaah ('Azza wa Jalla)  waliondoka kwa wepesi kabisa. Mamilioni ya maisha ya watu yalibadilika ghafla ndani ya kipindi kisichozidi nusu saa... Allaahu Akbar! Yapo wapi macho ya Waislam kutanabahi kiumbe hichi kinachoitwa ardhi kushindwa kuhimili madhambi ya wana Adam?!

 

Majanga haya hayajaacha kuganduka kwa China ingawa ina idadi kubwa ya wananchi wake kuwa sio Waislam. Juu ya kwamba wamekuwa na ubin Aadam na moyo wa kusaidia haraka, hata kwa wale waliokuwa hawana uwezo, nao wamejitolea kusaidia. Sisi Waislam leo uwezo tunao, badala ya kusaidiana tunaleta jeuri ya neema tuliopewa.

 

Ni funzo kwa Waislam kuwa Maneno ya Allaah ('Azza wa Jalla)hayaanguki abadan, kuwa siku za mwisho kutakuwa na majanga mengi, vifo vitatokea vingi kwa pamoja na mengineyo: Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

ظَهَرَ الْفَسَادُ فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ بِمَا كَسَبَتْ أَيْدِي النَّاسِ لِيُذِيقَهُم بَعْضَ الَّذِي عَمِلُوا لَعَلَّهُمْ يَرْجِعُونَ ﴿٤١﴾

Ufisadi umedhihiri katika nchi kavu na baharini kwa sababu ya yale yaliyochuma mikono ya watu ili (Allaah) Awaonjeshe baadhi ya waliyoyatenda ili wapate kurejea. [Ar-Ruwm 30: 41]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amekwishabainisha kuwa maafa yatakuwa ni mengi karibu na Qiyaamah pindi aliposema:

 

“Saa (Qiyaamah) haitosimama hadi elimu ifutwe, wakati kukimbia kwa kasi, zilzala (tetemeko la ardhi) kuzidi kwa wing, fitnah nyingi kudhihirika na al-Harj kuengezeka.” Ikaulizwa, “Ee Rasuli wa Allaah, nini hiyo al-Harj?” Akasema, “Al-Qatl, al-Qatl (mauaji).” [Imaam Ahmad]

 

Na kwa vile maneno ya Allaah ('Azza wa Jalla)    pamoja na Rasuli Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni ya haki; tujue kuwa mitihani hii ipo, na bila ya shaka kila tuliloahidiwa litatokea, ikiwemo Qiyaamah chenyewe. Kwa mantiki hiyo; tunatakiwa tustaghfiru na tujiweke tayari na kifo wakati wowote.

 

Hakuna mwenye miadi na Malakul-Mawt (Malaika mtoaji roho). Yeye anakuja ule wakati anaopangiwa na Allaah ('Azza wa Jalla) aje kuzichukua roho zetu. Wachina wale waliokufa kwa mpigo hakuna hata mmoja aliyejuwa kama siku ile ilikuwa ni siku yake ya kuaga dunia hadi kwamba apange kustarehe starehe ya mwisho duniani, au apange kukinga mauti.  Laiti ghayb ingejulikana na viumbe, bas serikali ya China ingekuwa na uwezo wa kuwahamisha watu wake kutoka kwenye eneo la tukio la zilzalah kabla maharibiko hayajatokea.

 

Hivyo hii iwe ni funzo na zingatio kwa wale wanaosema: "Acha nienjoy, mie kijana, bado damu inachemka kotokoto!” Waliokufa katika maafa walikuwemo vijana waliochemkwa na damu mpaka zikatokota kwa afya njema na uzuri. Na wale walionekana na maumbo madogo, hawakuwa ni mbilikimo (watu wafupi), bali ni watoto wadogo kuonesha kwamba kifo au maafa hayachagui umri.

 

Hili jambo pia liwaguse wenye uwezo wanaogoma kuhiji, wakisema kuwa watakwenda baadae watakapokuwa na umri mkubwa. Pengine katika mamilioni ya watu hao waliofariki, walikuweko ambao walikuwa na mawazo kama hayo lakini matamanio yao yameishia siku hiyo ya zilzala.  Na hiyo ni khiyana kwa Allaah ('Azza wa Jalla)   ambayo tunamfanyia, kwa vile Ametupa  uwezo na tunautumia kinyume na malengo ya Dini. Jambo hili liwe funzo pia kwa wale  wanawake wanaosema “Nitavaa vazi la hijaab baadaye acha nionyeshe uzuri wangu sasa!”    

 

Ni mengi tunayojifunza kutokana na zilzala za ardhi. Watu wengi waliopoteza viungo ambavo sisi tunavyo na badala ya kumshukuru Rabb  wetu, hatuinami kumnyenyekea kuswali mpaka mauti yatufikie kisha tubakie kuwa katika khasara na majuto ya kutamani kusujudu lakini wapi! Imeshawapita fursa hiyo. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

يَوْمَ يُكْشَفُ عَن سَاقٍ وَيُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ فَلَا يَسْتَطِيعُونَ﴿٤٢﴾ خَاشِعَةً أَبْصَارُهُمْ تَرْهَقُهُمْ ذِلَّةٌ ۖ وَقَدْ كَانُوا يُدْعَوْنَ إِلَى السُّجُودِ وَهُمْ سَالِمُونَ﴿٤٣﴾

Siku utakapofunuliwa Muundi na wataitwa kusujudu lakini hawatoweza. Macho yao yatainama chini, udhalilifu utawafunika. Na hali walikuwa wakiitwa wasujudu (kuswali duniani) walipokuwa wazima wa afya. [Al-Qalam: 42 – 43]

 

 

 

 

 

 

 

Share