Kuoa Mkristo Inafaa Japokuwa Sharti Za Ndoa Zimekamilika?

 

SWALI:

JE KAMA SHARTI ZA NDOA ZIKAFUATWA YAANI WALII AKAWA SHEKHE, MASHAHIDI WAWILI, MAHARI, KUKUBALI MUOLEWAJI NA MUOAJI, NA NDOA IKAFANYIKA NYUMBANI KWA MUOAJI BILA YA MKE KUBADILI DINI YAKE YA KIKRISTO JE NDOA ITAKUBALIKA?

 


 

JIBU:

AlhamduliLLaah - Sifa njema zote Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kuoa Mkristo. Hakika ni kuwa wapo wengi wasioelewa kuhusu mas-ala ya ndoa baina ya mwanamume Muislamu na mwanamke wa Kitabu. Allaah Aliyetukuka Ametoa ruhusa kwa mwanamume wa Kiislamu kumuoa mwanamke wa Kitabu (Mkristo au Myahudi). Hata hivyo Allaah Aliyetukuka hakuliacha jambo hilo bila ya kuliekea masharti. Ikiwa masharti hayo yaliyowekwa yatakuwa ni yenye kutimizwa basi kutakuwa hakuna tatizo. Aayah inayohusiana na hilo ni ile ya Suratul Maa’idah (5): 5,

Leo mmehalalishiwa vyote vizuri, na pia chakula cha waliopewa Kitabu ni halali kwenu na chakula chenu ni halali kwao. Na wanawake Waumini Muhswanaat na wale Muhswanaat waliopewa Kitabu kabla yenu ikiwa mtawapatia ujira (mahari) wao kuwataka kwa ndoa wala sio kuweka wazi zinaa wala kuwachukua kama vimada kwa siri”. Neno Muhswanaat lina maana ya wanawake wema watwaharifu waliojiweka mbali na uzinzi. Na ibara za mbele zinamaanisha kuwa wanawake hawa wasiwe ni wale wenye kufanya zinaa kwa siri au dhahiri.

 

Ikiwa Mkristo ana sifa hizo basi unaweza kumuoa baada ya kutimiza na hayo masharti mengine ya ndoa. Mbali na kwamba ruhusa hii imetolewa inatakiwa Muislamu awe ni mwenye kujiuliza: Ikiwa kila mwanamme Muislamu anaoa mwanamke wa Kikristo, je hawa wasichana wetu wa Kiislamu wataolewa na nani? Kwa sababu sisi kwa kutotilia maanani hilo leo katika sehemu nyingi wasichana wa Kiislamu wanachukuliwa na Wakristo.

Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo marefu muhimu kuhusu mas-ala haya:

 

Kuoa Wanawake wa Kitabu (Wakrito Na Mayahudi)

 

Nani Ahlul-Kitaab Na Wanawake Gani Tumeruhusiwa Kuwaoa?

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share