Amemrudia Mke Aliyeritadi Na Ambaye Alikuwa Akimhubiria Aingie Ukiristo

SWALI:

 

Assalaam aleykum.

 

Jamaa yangu alimsilimisha mwanamke akamuoa. Bahati mbaya wakaachana na yule mwanamke akasema kwa kutamka kuwa amerudi dini yake ya Ukristo baada ya kuachwa manake yeye alisilimu kwa kutaka kukaa na huyu bwana tu. Akawa anamletea huyu bwana makala za kumhubiria ili nae aingie ukristo. Baadae yule mwanamke akasema hajarudi dini yake ile ilikuwa ni kumfanya huyu bwana amrudie tu. Na huyu bwana amemuoa tena. Jee nini hukumu yake?


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu kwa swali lako kuhusu kumrudia mke aliyeritadi baada ya kumuacha.

 

Suala hili la kuoa mke au kuolewa na mume aliyesilimu na baada ya hapo ikafanywa Nikaah huwa yapo matatizo mengine. Tumetahadharisha sana suala hilo kwani baada ya ndoa huwa kunapatikana matatizo mengi sana kwa kuwa ndoa yenyewe haina ikhlaasw inayotakiwa katika Ibadah ya aina yoyote ile.

 

Ni nasaha kwa sote tufuate maagizo ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika kuchagua mchumba. Miongoni mwa maagizo ni kutafuta mke aliyeshika Dini na mwenye maadili mema. Mwanamke amesilimu leo na kesho kuolewa Dini yake imejulikana wakati gani? Shida zinazopatikana zinakuwa nyingi zisizokuwa na hesabu ya aina yoyote ile. Inatakiwa tuwe waangalifu sana katika uchaguzi wa mchumba ili tusiwe tunafanya kazi ya bure. Ni nasaha yetu ya dhati kuwa kabla ya kumuoa msichana kama huyo afunzwe Dini kwa muda usiopungua mwaka ili kuweza kupima Dini yake na ukakamavu wake katika kufuata Dini hii ya Kiislamu. Baada ya hapo unaweza kuchukua uamuzi muafaka baada ya kuswali Swalah ya Istikhaarah.

 

Wengi wanachukua ruhusa iliyotolewa kuwaoa wanawake wa Kiyahudi na Kikristo, lakini hata hivyo Allaah Aliyetukuka Ameweka sharti muhimu sana kabla ya sisi kuchukua hatua hiyo nyeti. Sharti lililowekwa ni wanawake hao wawe wema na bila kufanya nao uzinzi kabla ya kuingia nao katika ndoa ya halali. Mbali na hilo ni muhimu tuzibe paa zetu kwani wanawake wetu wataolewa na nani ikiwa kila mmoja kwa maslahi yake anaoa Mkristo.

 

Ikiwa mwanamke huyo baada ya kupatiwa talaka aliritadi hakutakuwa na ndoa baina yao mpaka arudi katika Uislamu kwa ajili ya kutaka Dini na sio kuolewa. Hivyo kama wamerudiana basi waachane haraka hadi mwanamke asilimu kikweli kisha huyo mwanamke kama anautaka Uislam kikweli, basi aanze kwanza kupewa mafunzo ya Uislam maana yaonyesha kuwa huyo mke hakupatiwa mafunzo ya Dini hapo kabla. Inatakiwa kwa wakati huu apatiwe vitabu kuhusu Uislamu awe ni mwenye kusoma apate ufahamu mzuri na kusomeshwa kabla ya kurudiwa. Ikiwa kweli atarudi katika Dini kwa kuomba msamaha na kujirekebisha pamoja na kusoma Uislamu kutakuwa hakuna tatizo lolote la wanandoa hao kurudiana.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share