Njia 10 Za Kuukaribisha Vizuri Mwezi Mtukufu Wa Ramadhwaan

 

Njia 10 Za Kuukaribisha Vizuri Mwezi Mtukufu Wa Ramadhwaan

 

Alhidaaya.com

 

Inatupasa tumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) kwa kutupa umri tukiwa katika Uislamu na Iymaan hadi kutufikisha tena kukaribia Mwezi mtukufu wa Ramadhwaan. Na hii ni fursa nyingine Anayotupa Allaah Ta’aala katika maisha yetu kushuhudia mwezi huu na kupata fadhila zake.  

 

Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa):    

 

 يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا كُتِبَ عَلَيْكُمُ الصِّيَامُ كَمَا كُتِبَ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِكُمْ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٨٣﴾

Enyi walioamini! Mmefaridhishwa Swiyaam kama ilivyofaridhishwa kwa walio kabla yenu mpate kuwa na taqwa.

أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۚ

(Swiyaam ni) Siku za kuhesabika[Al-Baqarah: 183-184]

 

Hii ni neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'alaa) Ambaye Ametujaalia kuwa na miezi iliyo bora kuliko miezi mingine au siku bora au masaa bora kuliko mengine, ambazo thawabu zake za mema yanayotendeka humo huwa ni zaidi ya nyakati nyingine. Mfano wake, (na Allaah Ana Mifano bora kabisa kulikoni ya yote) ni kama kunapokuwa na mauzo yaliyopunguzwa bei dukani (sale), ambayo kawaida yake huwekwa kwa muda mdogo tu maalum.  Na muda huu mtu huweza kununua vitu vingi kwa malipo kidogo tu. Basi Ramadhwaan ni mwezi mmoja tu, lakini malipo yake huwa ni mengi kuliko hata malipo ya miezi yote mingine.  Ikiwa mtu atatimiza Swawm yake inavyopaswa na kufanya mema mengi, na akawa katika twaa'ah (utiifu) kamili, taqwa na kuomba maghfirah, basi Muislamu hutoka katika mwezi huu akiwa amechuma thawabu tele na ameghufuriwa madhambi yake.

 

Amesema Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

  ((من صام رمضان إيماناً واحتساباً، غفر له ما تقدم من ذنبه)) أخرجه البخاري ومسلم  

((Atakayefunga Ramadhwaan kwa iymaan na kutaraji malipo, ataghufuriwa madhambi yake yaliyotangulia)) [Al-Bukhaariy na Muslim] 

 

Ramadhwaan ni mwezi ambao tunatimiza fardhi mojawapo ya Kiislamu. Ni mwezi uliojaa baraka, kheri na Rahmah za Allaah (Subhaanahu wa Ta’alaa). Kila Muislamu inampasa aukaribishe mwezi huu kwa furaha na matumaini kamili.

 

Zifuatazo ni njia kumi za kujitayarisha kuukaribisha mwezi wa Ramadhwaan na kupata manufaa makubwa pindi utakapotimiza:

 

 

1- Du'aa

Anza kwa kuomba Du'aa kwamba mwezi huu ukufikie wakati umo katika hali ya siha nzuri na usalama hata uweze Swawm na kufanya ‘ibaadah zako kwa hamu kubwa na wepesi.  

 

 

2-Mazoezi katika mwezi wa Sha'baan  

 

Funga Sunnah nyingi katika mwezi wa Sha'baan, soma Qur-aan Juzuu moja kila siku au chini yake au zaidi yake, amka usiku uswali japo Rakaa mbili, kisha zidisha kidogo kidogo hadi inapoingia Ramadhwaan uwe tayari umeshapata mazoezi mazuri.

 

 

 

3- Shukurani Na Furaha

 

Mshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kukupa uhai na siha hata uifikie Ramadhwaan nyingine.  Imaam An-Nawawy alisema, kwamba shukurani inapasa kwa kila jambo jema unalojaaliwa kubwa au dogo na vile vile shukurani inapasa kwa kila jambo baya Analokuepusha nalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).  Kwa hivyo fanya 'Sajdatush-Shukr' [Sajda ya kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)] kwa neema hii tukufu.  

 

 

Furahia kukufikia mwezi wa Ramadhwaan kama unavyomfurahikia mgeni mpenzi anapokuja kwako na kumuandalia mazuri yote.  Maswahaba (Radhwiya Allaahu ‘anhum), walikuwa wakiamkiana unapoingia mwezi wa Ramadhwaan na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akisema hivi anapowabashiria khabari nzuri za mwezi wa Ramadhwaan:

 

((جاءكم شهر مبارك افترض عليكم صيامه تفتح فيه أبواب الجنة وتغلق فيه أبواب  الجحيم وتغل فيه الشياطين  فيه ليلة خير من ألف شهر من حرم خيرها فقد حرم)) رواه أحمد 

((Umekujieni mwezi wa Ramadhwaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni fardh, milango ya Jannah hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na mashaytaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu.  Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri])) [Ahmad]

 

 

4-Jipangie wakati na weka maazimio

 

 

Ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wanafurahia kuingia mwezi wa Ramadhwaan kwa kujiandaa kupanga mambo ya kidunia badala ya mambo ya Aakhirah.  Wengi hukimbilia kwenda sokoni kununua nguo za 'Iyd, na kufurahikia vipindi vya Ramadhwaan katika televisheni ambavyo sio vya dini kama 'misalsal' (vipindi vya televisheni vinavyoendelea), na pia kuanza kukusanya video za filamu, mipira, na mambo ya kupotezea muda usiku wa Ramadhwaan. Pia wengine kunua karata, dhumna, meza ya mchezo wa keram kwa maandalizi ya vipumbazo na vipoteza muda katika mchana wa Ramadhwaan ili wasiihisi Swawm au kuupeleka muda haraka kama wanavyoamini wao. Badala ya kufanya maandalizi ya kununua misahafu ya ziada, kanda za mawaidha, Qur-aan, kukusanya video za mawaidha na mafunzo mbalimbali ya Dini, vitabu vya Dini kwa lugha wanayoifahamu kwa wepesi na kadhalika.

 

 

Huu ni mwezi wa kufanya ‘ibaadah na fursa ya kujichumia mema mengi yamfaayo mtu Aakhirah. Kwa hiyo ndugu Waislamu, tujitahidi kuutumia wakati wetu wote bila ya kupoteza hata dakika moja, na muhimu sana kujipangia mapema wakati wako kama ifuatavyo:

 

 

 • Ni bora kujipangia nyakati zote za mwezi mzima vipi utatumia muda wako wa mchana na usiku. Weka maazimio ya dhati kuchukua fursa kamili ya wakati wote wa mwezi huu.

 

 • Weka mpango maalum wa kazi zako hata uweze kuswali kwa wakati kila kipindi, kusoma Qur-aan, kula daku na mengineyo kama tutakavyotaja hapa chini.

 

 • Kama ni mwanafunzi na kama ulikuwa ukisoma usiku, lala mapema, kisha uamke uswali Qiyaamul-Layl na usome masomo yako baada ya hapo.

 

 • Anza mpango wako kwa siku chache na kama unahitaji kurekebisha kuboresha nidhaam yako fanya hivyo uweze kujua nidhaam ipi itakayowafikiana na hali yako. 

  

5- Tawbah na Maghfirah      

 

Omba Tawbatun-Naswuwhaa (toba ya kikwelikweli) kwa Rabb wako na waombe msamaha wale uliowakosea. Kufanya hivi kutanufaisha zaidi Swawm na Swalaah zako na pia kukupa iymaan kuwa huna haki ya mtu.

 

 

6- Jifunze Fiqhi ya Swawm

 

Jifunze elimu ya mambo yanayohusu Swawm (Fiqhi ya Swawm), hiyo ni muhimu ili usije kufanya jambo la kuharibu Swawm yako.  Jifunze Swawm kama aliyokuwa akiifunga Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  ndio mfano bora kabisa wa kuufuata.

 

Swawm haifunguliwi kwa kula na kunywa tu, bali pia ni kujiepusha na maneno mabaya na kufanya mambo mabaya kama kusengenya, kutukana, kugombana. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 ((من لم يدع قول الزور والعمل به والجهل فليس لله حاجة في أن يدع  طعامه وشرابه)) البخاري   

 

((Yeyote asiyeacha kusema maneno mabaya? Na vitendo vibaya basi hana haja kuacha chakula chake na maji)) [Al-Bukhaariy]

 

 

7- Jitayarishe kuchuma mema mengi  

 

 

 • Mwezi wa Ramadhwaan ni mwezi wa ukarimu, huruma, rahma na mapenzi.

 

 • Panga kabisa na kuweka kiwango fulani cha kutoa swadaqah na kutoa kwa maskini, anzia kwanza kwa ndugu na jamaa.

 

 • Kama inakupasa kutoa Zakaah, na umependa iwe katika mwezi wa Ramadhwaan fanya hima uitimize fardhi hii pia.

 

 • Weka 'azma ya kufuturisha kwa kualika ndugu, jamaa, jirani na marafiki kwani kumfuturisha mtu ni thawabu.

 

                                

قال صلى الله عليه وسلم : (( من فطر صائماً كان له مثل أجره غير أنه لا ينقص من  أجر الصائم شيء)) أخرجه أحمد والنسائي وصححه الألباني

Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alahyi wa aalihi wa sallam) ((Atakayemfutarisha aliyefunga, atapata ujira kama ujira wake bila ya kupungua chochote katika ujira wa yule aliyefunga)) [Ahmad, An-Nasaaiy na kasahihisha Imaam Al-Albaaniy]

 

 • Kama unaye jirani asiye Muislamu, mjulishe kuhusu Ramadhwaan, faida na fadhila zake. Hii ni njia na fursa mojawapo ya kufanya da'wah kwa jirani yako.

 

 

8- Hitimisha Qur-aan, Hifadhi Na Jifunze Tarjama Na Tafsiyr. 

 

 

Jipangie wakati uweze kuhitimisha Qur-aan kwani Ramadhwaan ndio mwezi ulioteremshwa Qur-aan na hivi ndivyo alivyokuwa akifanya Jibriyl (‘alayhis-salaam) kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  kusoma naye Qur-aan yote:

 

 عن ابن عباس رضي الله عنهما قال: "كان رسول الله صلى الله عليه وسلم أجود الناس، وكان أجود ما يكون في رمضان حين يلقاه جبريل، وكان يلقاه في كل ليلة من رمضان فيدارسه القرآن؛    رواه البخاري

 

Kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhwiya-Allaahu ‘anhumaa)  kwamba: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) alikuwa ni mbora (mwenye matendo mema) wa watu, lakini alikuwa mbora  zaidi katika Ramadhwaan kwa sababu Jibriyl alikuwa akimjia kila usiku wa Ramadhwaan akimfundisha Qur-aan))  [Al-Bukhaariy]

 

 

Hadiyth hii inatufundisha yafuatayo:

 

 

 • Kusoma Qur-aan katika Ramadhwaan;

 

 • Kukutana kwa ajili hiyo;

 

 • Kupima hifdh yako ya Qur-aan kwa kukaa na Mwalimu au mwenye elimu nzuri ya Qur-aan kwa kukusikiliza au kukufundisha;

 

 • Kuongeza juhudi za kusoma Qur-aan zaidi katika mwezi wa Ramadhwaan:

 

 

Katika muda wa masaa 24 weka saa moja au mbili iwe khaswa ya Qur-aan kusoma na kujifunza maana ya maneno ya Rabb wako uonje ladha ya Qur-aan. Vile vile jitahidi kujiwekea wakati wa kuhifadhi japo Suwrah ndogondogo ili ukitoka katika Ramadhwaan uwe una Suwrah zaidi za kusoma katika Swalaah zako. 

 

 

 

9-Mdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Kila Mara

 

 

Usiache ulimi wako na moyo wako kuwa mtupu bila ya kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  kila wakati kila mahali. Huku unafanya kazi zako za jikoni, fanya Adkhaar za Tasbiyh (Subhaana Allaah), Tahliyl (Laa ilaaha illa-Allaah), Tahmiyd (AlhamduliLLaah), Takbiyr (Allaahu Akbar) na Adhkaar nyenginezo zilizothibiti katika Sunnah. Kufanya hivi utajichumia thawabu maradufu, kwa kutimiza wajib wako na kuongezea kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na juu ya hivyo kuongeza baraka katika kazi zako:

 

 

 

10- Darsa

 

Hudhuria Darsa katika mwezi huu au soma vitabu vya Dini, au sikiliza mawaidha.  Jambo hili ni muhimu sana kwani kusikiliza mawaidha ni njia muhimu na bora kabisa katika kuzidisha iymaan na elimu ya Dini yako. 

 

Kwa hakika unahitaji saa tu kuweza kutimiza jambo hili muhimu kila siku.  Kama huwezi kuhudhuria msikitini, Alhamdulillah, ALHIDAAYA  imejaa  mawaidha ya kusikiliza.  Tumia muda wako hata wakati unafanya kazi zako za nyumba na za jikoni huku unasikiliza mawaidha. Kwa hiyo badala ya kutazama televisheni na kusikiliza muziki jambo ambalo ni haraam ni bora utazame na kusikiliza mawaidha ujipatie manufaa, thawabu na kuongeza elimu yako. Kumbuka kwamba kama vile mwili unavyohitajia chakula, hali kadhalika moyo na nafsi zinahitaji chakula chake nacho ni kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kila aina ya kumdhukuru, na mawaidha na darsa za Dini ni mojawapo ya chakula kizuri kabisa cha kutakasa moyo na nafsi kwa kuzijaza iymaan na mapenzi ya Allaah ('Azza wa Jalla).

 

Kwa kumalizia, tunasema: 

 

 

Fungua Ukurasa mpya katika maisha yako  

 

Baada ya kuweza kuyatimiza hayo yote, basi hali yako ya iymaan itakuwa ni bora kabisa na utakuwa umejibadilisha na kuwa mtu tofauti na ulivyo.  Kwa hivyo weka maazimio ya kuendelea hata baada ya Ramadhwaan kuwa katika twaa'ah (utiifu) na ‘ibaadah kwa wingi, na kuendeleza Qiyaamul-Layl (Kisimamo cha usiku), kusoma Qur-aan japo kidogo kila siku, na iwe umefungua ukursa mpya wa maisha yako na kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa)  Akuendeleze katika hali hii.

 

 

Tunachukua Fursa hii ya kuwaombeeni Ramadhwaan yenye baraka na kheri nyingi, tutoke katika mwezi huu tukiwa tumesafishwa madhambi yetu yote, na wenye kubeba thawabu nyingi ziwe nzito katika Miyzaan ya Hasanaat (mizani ya 'amali njema) Siku ya Qiyaamah. 

 

اللَّهُمَّ تَقَبَّلْ مِنَّا وَ مِنْكُم  

 

Ee Allaah Tutaqabalie sisi na nyinyi.

 

 

 

 

 

Share