Kamlipia Aliyefariki Pesa Alizochukua Bila Idhini Ya Mwenye Mali?

SWALI:

 

Asalam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatu, Jambo la mwanzo ni kuwashukuruni sana kwa kutuelimisha kwa kupitia kwenye mtandao, Suali langu ni kutaka kujua namna ya kumlipia madeni aliyefariki hii inatokana na aliyefarikii sehemu aliyokua akifanya kazi alichukua pesa taslim bila ya ridhaa ya mwenyewe na suala hili mke wake alikuwa akilielewa vizuri baada ya mume kufariki mke akenda alipokuwa akifanya kazi mume aliyefariki na kutaka kumlipia bila ya kujua ni kiasi gani wakakubaliana kuwa amlipie kwa kiasi fulani ikiwa kasoro atamsamehe na ikiwa zaidi mke atamsamehe mwenye mali suala langu ni hili kuwa inafaa kwa vile tumekamilisha malipo tuliyokubaliana tunaomba jawabu kwa manufaa ya waislamu wote Asalam Alaikum


 

JIBU:

 

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu wizi wa mtu ambaye wakati huu ni aliyefariki. Hakika ni kuwa mtu huyo alikuwa na makosa makubwa na hatujui mkewe baada ya kujua hilo alichukua hatua gani kumrekebisha. Je, alizungumza na mumewe? Mazungumzo hayo yalitoa natija gani? Je alikubali kosa lake na akataka kujirekebisha au vipi?

 

Kisheria ni kuwa mume alikuwa apatiwe adhabu hapa hapa duniani kwa kosa hilo na ikiwa hakupata hapa basi atapata Siku ya Qiyaama kutegemea na nia yake katika kurekebisha kosa hilo. Sasa kwa kuwa tayari ashaaga dunia na hapa hakupata adhabu yoyote huenda akapatiwa huko. Bila shaka kama tunavyojua kuwa yapo masharti kwa mtu kukubaliwa toba yake. Wanazuoni wameweka masharti MANNE kama kosa linaingiliana na haki ya nwanadamu. Hakika ni kuwa masharti haya yametokana na Aayah za Qur-aan na Sunnah za Bwana Mtume Muhammad (Swalla Allaah ‘alayhi wa sallam). Katika hayo masharti ni kuwa mtu aombe msamaha kwa yule aliyemkosea. Kwa kuwa yeye alichukua mali ya watu bila ruhusa ilikuwa atake msamaha na kuilipa kabla ya kuaga dunia.

 

Kwa kuwa hilo lishapita bila ya yeye kufanya hivyo nanyi mkawa ni wenye kufanya juhudi kulipa alichoiba, Allaah Aliyetukuka huenda akawaangalia kwa jicho la huruma na kumsamehe.

 

Hakika ni kuwa Yeye Allaah ni Mwingi wa kusamehe na Mwenye huruma kubwa sana. Kwa hivyo, nyinyi endeleeni kumuombea na Allaah Aliyetukuka Atawatakabalia hilo. Wala msikate tamaa katika hilo kwani Muislamu hakati tamaa na Rehema ya Allaah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share