Kuhifadhi Mabaki Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Swahaba Inafaa?

Kuhifadhi Mabaki Ya Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) Na Swahaba Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalamu alaikum warahmatulahi wabarakatuhu.Kwanza nawashukuru sana kwa kutuelimisha na kutunufaisha na in shaa Allah Allaah awazidishie nguvu na imani ya kuendeleza kazi hii muhimu mnayoifanya. Swali langu ni je, inakubalika kuhifadhi vyombo vya zamani kama seif ya maswahaba au nguo ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au footprint yake kama ilivyo katika Museum in Istanbul? Kwa sababu nimewaona watu kwa T.V wakibusu na kulia machozi. Nauliza kwa sababu nadhania watu watazipa umuhimu na baadaye kujikuta wakimshirisha Allaah bila kujua.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunakushukuru kwa Swali lako hilo muhimu ambalo lina hatari ya kumharibia Muislamu 'Aqiydah yake kwa kutukuza vitu na kuingia katika shirk.

 

 

Kuna uzushi mwingi siku hizi kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha vitu vinavyodaiwa kuwa ni vya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na vya Swahaba. Na kama ulivyoona kuwa vinaonyeshwa hata katika televisheni.

 

 

Kwanza hakuna uthibitisho kuwa hivyo vitu vilivyohifadhiwa kuwa ni kweli vina uhusiano na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) au vya Swahaba. Uthibitisho lazima upatikane kwa ushahidi sahihi, bila ya hivyo basi bila shaka ni uzushi ambao haumpasi Muislamu kufuata, kwani hakumpatii Muislamu faida yoyote katika Dini yake au kumzidishia elimu katika vitu hivyo. Badala ya kupoteza muda wake Muislamu katika mambo kama hayo yasiyomfaa bali yanayaweza kumletea madhara katika 'amali zake, ni bora kuutumia muda wake kwa kujishughulisha na mengi yaliyo sahihi yatakayomjengea Aakhirah yake.

 

 

Ikiwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipinga kutukuzwa na kusifiwa akiwa hai, iweje leo hii watu wazushe vitu na kudai ni vyake na kisha kuvitukuza na kuviadhimisha? Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema:

 

((لا تطروني كما أطرت النصارى المسيح ابن مريم، إنما أنا عبد، فقولوا: عبد الله ورسوله))  متفق عليه

((Msinitukuze Kama Manaswara walivyomtukuza Masiyh mwana wa Maryam, hakika mimi na mja kwa hiyo semeni mja wa Allaah na Rasuli Wake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Tunaona leo kwenye baadhi ya Misikiti kuna picha ya unaodaiwa unyayo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), picha za jino lake, unywele wa ndevu yake n.k. Na hao wanaoweka hizo picha wakidai wanamtukuza na kumpenda, utakuta hata hawafuati maamrisho yake na Sunnah zake. Wameweka picha ya unywele wa ndevu zake, hapo hapo wenyewe hawafugi ndevu! Sasa ni mapenzi gani wanayoyaonyesha kwa Nabiy (Swalla Allahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama ni wakweli?

  

Vile vile kutukuza vitu hivyo na kuvibusu na kujipangusia kwavyo kutaka kupata baraka, ni jambo ambalo linampelekea Muislamu katika shirki. Tuchukue mfano wa 'Umar (Radhwiya Allaahu 'anhu) alivyokuwa na khofu ya kulibusu Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) lilioko katika Ka'bah alipolifikia wakati akifanya Twawaaf alisema:

 

"إني أعلم أنك حجر لا تضر ولا تنفع ولولا أني رأيت النبي صلى الله عليه وسلم يقبلك ما قبلتك"   البخاري

"Mimi nafahamu kuwa wewe ni jiwe tu ambalo halinufaishi wala kumdhuru mtu, na ingekuwa sikumona Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anakubusu basi nisingekubusu". [Al-Bukhaariy]

 

Na madam hakuna uthibitisho kuwa Swahaba walikuwa wakivitukuza vitu vya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) basi haimpasi Muislamu kuambatanisha utukufu wa chochote ili asije kuingia katika shirki.

 

 

Shirki kama hiyo imedhihirika hadi katika Masjid ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ambako Hujaji na wenye kufanya 'Umrah wanaonekana wakigusa na kupapasa kaburi la Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)  na makaburi ya Swahaba na kujipangusa mwilini kwa kudhani kuwa wanapata nafuu au utukufu au baraka zao. Vile vile wengine huligusa Ka'bah na kulipapasa, na hata kung'ang'ana kwenye kuta zake hadi kwamba wanasabisha zahma, madhara na dhiki sehemu hiyo ya kufanya Twawaaf kwa Waislamu wengine. Hakika hili ni jambo lisilokuweko katika Shariy’ah yetu na ni jambo ovu kabisa ambalo linamharibia Muislam 'Aqiydah yake. Na ni jambo la asasi kuwa na 'Aqiydah iliyo safi kabisa isiyoambatana na uzushi na shirki, kwani shirki ni dhambi ambayo hasamehewi  kabisa mja pindi akifariki katika hali hiyo kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

 

إِنَّ اللَّـهَ لَا يَغْفِرُ أَن يُشْرَكَ بِهِ وَيَغْفِرُ مَا دُونَ ذَٰلِكَ لِمَن يَشَاءُ ۚ وَمَن يُشْرِكْ بِاللَّـهِ فَقَدِ افْتَرَىٰ إِثْمًا عَظِيمًا ﴿٤٨﴾

Hakika Allaah Haghufurii kushirikishwa; lakini Anaghufuria yasiyokuwa hayo kwa Amtakae. Na yeyote atakayemshirikisha Allaah basi kwa yakini amezua dhambi kuu.  [An-Nisaa:48]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share