Zakaatul-Fitwr Inafaa Kwa Ajili Ya Kusaidia Matibatu Ya Yatima?

 

Zakaatul-Fitwr Inafaa Kwa Ajili Ya Kusaidia Matibatu Ya Yatima?  

 

 www.alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Je, tunaweza kumsaidia matibabu mtoto Yatima ambaye ni mgonjwa sana kwa kumkusanyia Zakaah zetu za Fitr?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza inapasa tufahamu tofauti baina ya aina mbili za Zakaah; Zakaatul-Maal ambayo ni nguzo katika nguzo tano za Kiislam. Na Zakatul-Fitwr ambayo ni zakaah inayotolewa baada ya Swawm ya Ramadhwaan kwa ajili ya kuitwaharisha  Swawm ya mfungaji.

 

1-Zakaah Ya nguzo tano ya Kiislamu (Zakaatul-Maal):

Ni Zakaah ya mali anayomiliki mtu inayofikia mwaka wa Kiislam (hawl) bila ya kutumika.

 

Anayewajibika Kutoa:

Mwenye kumiliki mali ya aina mbalimbali ambayo tayari ishafikia Niswaab kama ilivyo hapa chini.

 

Mali Inayotolewa:

Mali zinazopasa kulipiwa Zakaah ni dhahabu, fedha, pesa, mifugo ya wanyama; (ngamia, ng'ombe, kondoo, mbuzi). Vinavyotaka ardhini kama mazao (nafaka, mchele, maharage, mtama, mahindi, n.k.)  na mali iliyofukiwa.

 

Muda Wake:

Muda wa kulipwa Zakaah ni baada ya mwaka mmoja wa Kiislam, yaani mpaka mali hizo zipitiwe na mwaka mzima ndipo zilipiwe. Lakini kwa Zakaah ya mazao, muda wake unategemea uvunaji wake, ikiwa mazao yamevunwa zaidi ya mara moja kwa mwaka basi Zakaah hiyo inabidi itolewa pale mazao yanapovunwa.

 

Wanaostahiki Kupewa:

Ni aina ya watu wanane kama walivyotajwa katika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((إِنَّمَا الصَّدَقَاتُ لِلْفُقَرَاء وَالْمَسَاكِينِ وَالْعَامِلِينَ عَلَيْهَا وَالْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِي الرِّقَابِ وَالْغَارِمِينَ وَفِي سَبِيلِ اللّهِ وَابْنِ السَّبِيلِ فَرِيضَةً مِّنَ اللّهِ وَاللّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ))

((Wakupewa sadaka (Zakaah) ni mafakiri, masikini, wanaozitumikia, wa kutiwa nguvu nyoyo zao, katika kukomboa watumwa, wenye madeni, katika Njia ya Allaah na wasafiri. Huu ni wajibu uliofaridhiwa na Allaah. Na Allaah ni Mjuzi Mwenye hikma) [At-Tawbah: 60].

 

Ama kuhusu Zakaah ya Fitwr ni kama ifuatavyo:

 

2-Zakaatul-Fitwr:

Ni Zakaah inayotolewa baada ya kumalizika Ramadhwaan kwa ajili ya kumsafisha (kumtwaharisha) mwenye kufunga kutokana na maneno ya upuuzi na machafu, kwa kuwalisha masikini

 

Anayewajibika Kutoa:

Waislamu wote, mtumwa na na aliye huru, mwanamke na mwanamume, kijana na mzee, kwa anayemiliki chakula cha siku moja.

 

Mali Inayotolewa:

 

Ni chakula ambacho kinachotumika katika mji huo ikiwa ni mchele, tende, zabibu, shayiri (ngano) n.k. Usimulizi ufuatayo ni dalili:

Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) amesema: “Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya kutoka swaa’ (pishi moja kilo 2 ½ - 3) ya tende au swaa’ ya shayiri (ngano) kuwa ni Zakaatul-Fitwr iliyowajibika kwa Waislamu wote, mtumwa, aliye huru, mwanamke na mwanamume, kijana na mzee, na akaamrisha kwamba itolewe kabla ya watu kwenda kuswali (Swalaatul’Iyd)” [Al-Bukhaariy]

Vile vile,

Abu Sa’iydil-Khudhriyy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema: ‘Tulikuwa tukilipa Zakaatul-Fitwr swaa’ (pishi moja) moja ya chakula au swaa’ ya shayiri (ambacho ndicho kilichokuwa chakula chao zama hizo) au swaa’ ya tende au swaa’ ya aqit (mtindi mkavu) au swaa’ ya zabibu” [Al-Bukhaariy]

 

Muda Wake: 

Muda wake ni kuanzia jua linapozama siku ya mwisho ya Ramadhwaan ambayo ni usiku wa mwanzo wa mwezi wa Shawwaal na unamalizikia na Swalah ya 'Iyd.

 

Wanaostahiki Kupewa:

Zakaatul-Fitwr inapaswa kupewa maskini Waislamu katika nchi au mji ambao inatolewa kutokana na dalili ifuatayo:

Kutoka kwa Abuu Daawuwd kutoka kwa Ibn 'Abbaas (Radhiya Allaahu 'anhumaa) ambaye amesema: "Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ameamrisha Zakaatul-Fitwr ilipwe Ramadhwaan kuwalisha masikini”

 

Lakini ikiwa hawapatakani masikini ndipo inapofaa kupelekwa nchi nyiginezo ambako kuna masikini na hapa ndipo inapobidi kutumwa fedha badala ya chakula.

 

 

Kutokana na maelezo hayo, ni dhahiri kwamba kuna tofauti kubwa baina ya Zakaah hizi mbili, na tunaona kwamba zote hazikutajwa kuwa apewe yatima ingawa katika Zakaah ya Mali ikiwa Yatima ni masikini mwenye kuhitaji ataangukia katika waliotajwa kwenye Aayah hiyo Namba 60 ya Suratut-Tawbah, iliyotaja aina ya watu wanane. Na katika hali hii Zakaatul-Maal ingelifaa kutolewa kwa ajili yake.

 

Lakini Swali hapa ni kuhusu Zakaatul-Fitwr ambayo haikutajwa kabisa kupewa Yatima, ingawa ikiwa Yatima huyo ni maskin basi yafaa kumpa Zakaatul Fitwr kwani atakuwa kachukua nafasi ya maskini ambae anastahiki kupewa Zakaatul Fitwr, na kisha asili ya kinachopasa  kutolewa  ni chakula na sio fedha.  Kwa hiyo haifai kutoa Zakaatul-Fitwr kwa ajili hiyo. Zaakatul-Fitwr itolewe  mbali kama ipasavyo ili itimizwe na ipewe haki yake kama yalivyo maamrisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) katika usimulizi tuliotaja juu.

 

Kumhudumia Yatima, kumtazama kwa hali na mali ni jambo linalopasa bali limesisitizwa sana katika Qur-aan na Sunnah, na fadhila na thawabu zake ni kubwa mno. Ni wajibu wa Waislamu kumsaidia Yatima huyo ambaye tayari juu ya kuwa ni Yatima, anahitaji msaada ya matibabu. Hivyo basi inapasa kumsaidia kutokana na sadaka za mwenye kupenda kufanya kheri. Na mwezi huu wa Ramadhwaan umejaa fadhila na thawabu kwa kutoa sadaka, hivyo Waislamu wajitahidi kutoa sadaka zao kumsaidia Yatima huyo ambaye anahitaji kuhudumiwa pamoja na matibabu yake.     

 

 

Tafadhali  bonyeza viungo vifuatavyo upate faida nyenginezo kuhusu hukmu za Zakaatul-Fitwr

Fataawaa: Za Zakaatul-Fitwr

Fataawaa: Mukhtasari Wa Fataawaa Za Zakaatul-Fitwr

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share