Kamtoroka Mume Kwa Sababu Anampiga, Nini Haki Yake Kuhusu Mahari Ambayo Hakulipwa Mwanawe?

SWALI:

 

Assalam Aleikum. Mimi nimeolewa miaka mitatu na nusu na nina mtoto   mmoja. Mimi na mume wangu tunaishi pamoja na familia yake. Lakini hatukuweza kusikizana nao. Ilifika wakati hadi mume wangu akanipiga. Niliweza kutorakea nyumbani kwetu maana ni mbali. Lakini mume wangu amekataa kuja nyumbani kutoa pole kwa yale aliyoyatenda na wazazi wangu wanadai aje kwanza. Nilimuacha mwanangu huko kwa vile sina uwezo kama wao. Wao ni tajiri na mimi sina utajiri. Mume wangu ameweza kunipimia wakati kama sitarudi nyumbani ataniandikia talaka yangu.

 

Hajalipa mahari yangu bado Je Kuna haki gani kwangu.

 

  1. Kwa mtoto wangu

  2. Kwangu mimi mwenyewe.

Naomba usaidizi tafadhali


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako, dada yetu kuhusu kupigwa na mumeo. Haya ni mashtaka ya upande mmoja na inakuwa ni vigumu sana kuweza kuamua kwa uadilifu lakini tutajaribu kugusia mambo mengi pamoja na kukuuliza maswali ili tuweze kukusaidia kwa njia ambayo ni nzuri zaidi.

Mwanzo inaonyesha kulingana na ibara ya swali lako ni kuwa mume ni tajiri kuliko familia yenu. Je, ulikubali kuolewa naye kwa sababu ya utajiri wake au nasaba yake? Ikiwa ulimkubali kwa msingi huo utakuwa umekosea sana kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuusia kwa kutumbia:

 

Akikujilieni ambaye mmeridhia Dini na maadili yake, mwozesheni kwani mkitofanya hivyo kutakuwa na fitina na uharibifu mkubwa” (at-Tirmidhiy).

 

Kisha umefanya kosa la kukimbia kutoka katika nyumba yako. Hukueleza kwa kina sababu nyengine iliyokufanya ufanye hivyo (yaani kutoroka nyumbani kwako). Je, alikupiga mara hiyo hiyo moja au ni ada yake kukupiga? Je, ikiwa alikupiga siku hiyo moja tu, ulifanya kosa lolote? Tufahamu kuwa mume hafai kumpiga mkewe kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

Si bora miongoni mwenu mwenye kumpiga mkewe”.

 

Lakini kosa hilo limetokea hujapata nafasi ya wewe kukimbia kutoka nyumbani kwako.

Kosa hilo lingeweza kurekebishwa kwako wewe kuzungumza na mumeo baada ya kitendo hicho na kutazama nani aliyekosa kusameheana na kuendelea na maisha. Kama umeona labda tatizo hilo linatokana na kukaa katika nyumba pamoja na familia yake mgejadiliana kwa njia nzuri na kuangalia ufumbuzi ulio na maslahi kwa kila mmoja kati yenu. Kunapotokea tatizo tumepatiwa ufumbuzi mzuri lakini mara nyingi huwa hatutaki. Lile ambalo tungekushauri sasa usiwe mkakamavu wala kutaka makubwa bali funga safari na babako au jamaa yako wa karibu urudi nyumbani na mulizungumze tatizo hilo ukiwepo wewe, mumeo, babako au jamaa yako na babake mume au mwakilishi kutoka upande wake. Hii ni kwa kauli ya Allaah Aliyetukuka:

 

Na mkichelea kutakuwapo mfarakano baina ya mke na mume basi pelekeni muamuzi kutokana na jamaa za mume, na muamuzi kutokana na jamaa za mke. Wakitaka mapatano Allaah Atawawezesha. Hakika Allaah ni Mjuzi Mwenye khabari” (4: 35).

 

Ama kuhusu mahari ni haki yako na ulikuwa upatiwe kuanzia mwanzo lakini huku kukimbia kwako ndiko kunaleta utata. Je, unataka kujiachisha au humtaki tena mumeo au unatakaje? Kwa ajili ya hayo ambayo hukutueleza inabidi kuhusu hilo uipeleke kesi yako kwa Qaadhi ili aweze kuamua kesi yako hiyo. Ama haki yake kwa mtoto ni babake kumtazama kwa mahitaji yake yote – mavazi, matibabu, malazi, kumsomesha na mengineo. Na ikiwa mtoto atakuwa kwako pia itabidi baba amtimizie mahitaji hayo yote.

 

Tunamomba Allaah Aliyetukuka Awaondolee matatizo hayo na Awarudishe tena katika ndoa.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share