Khadiyjah Bint Khuwaylid (رضي الله عنها)

 

 

Haliymah ‘Abdullaah

 

 

Khadiyjah bint Khuwaylid bin Asad bin ‘Abdil-‘Uzza bin Qusway bin Kilaab Al-Qurayshiyah Al-Asadiyah aliyekuwa akijulikana kama At-Twaahirah (msafi), alizaliwa katika nyumba ya utukufu na heshima kabla ya mwaka wa tembo kwa miaka kumi na tano, akalelewa malezi mazuri akawa mwanamke mwema mwenye akili na adabu jambo lililomjaalia kuwa mashuhuri na kupelekea macho yote ya wanaume wenye vyeo katika jamii yake yamuelekee.

 

Aliolewa na Abu Haalah bin Zurarah At-Tamiymiy akamzalia Haalah na Hind alipofariki Abu Haalah aliolewa na ‘Atiyq bin ‘Aaidhw bin ‘Abdillaah Al-Makhzuumiy akakaa naye muda kisha wakaachana.

 

Wakajitokeza watukufu wengi wa ki-Quraysh lakini aliamua kusimamia malezi ya wanae na biashara zake Kwani alikuwa tajiri mwenye mali anaajiri wanaume katika biashara zake na kuwalipa, ilipomfikia habari ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) kabla ya utume kwa aliyosifika nayo katika ukweli, amana na tabia nzuri alimuajiri na kumtuma Shaam na kijana wake aitwae Maysarah.

 

Akakubali Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akasafiri na Allaah Akamuwafikisha katika biashara hii akarudi na faida kubwa akajua Bi Khadiyjah kwamba huyu mwanaume sio kama wengine akaanza kujiuliza je, kijana huyu atakubali kumuoa mama aliyefikia miaka arobaini? Jamii itamfikiriaje naye amewakataa wengi?

 

Alipokuwa katika lindi la mawazo akaingia rafiki yake Nafiysah bint Manbah na akaweza kumdodosa mpaka akamueleza linalomsumbua, naye akamtuliza na kumweleza kuwa yeye ni mwenye cheo, mali, uzuri wanaume wote wanampigania hivyo asijali naye atamsaidia.

 

Akatoka kwake na kuelekea kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akaanza mas-ala kwa akili na kumuuliza:

Kitu gani kinakuzuia kuoa ewe Muhammad?

Akajibu sina mkononi cha kuolea… akatabasamu huku akisema:

Je, ukitoshelezeka na kuitwa katika mali, uzuri, utukufu, usawa (kafaa-ah) utakubali? Akajibu kwa kuuliza ni nani? Akajibu kwa haraka ni Bi Khadiyjah bint Khuwaylid.

Akasema ikiwa atawafiki, basi nami nimekubali.

Akarudi haraka kumpa bishara rafiki yake. Na Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akawaeleza ‘Ami zake kuhusu kumuoa Bi Khadiyjah, Akaenda Abu Twaalib na Hamzah kwa ‘Ami yake Khadiyjah ‘Amru bin Asad wakamposea na kutoa mahari.

 

Akahudhuria katika sherehe Haliymah Sa’adiyah (mnyonyeshaji wa Mtume Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) wakamzawadia mbuzi arobaini wakati wa kurejea.

 

Wakaishi maisha mazuri ya furaha na heshima na wakaajaliwa kupata watoto sita (Al-Qaasim, ‘Abdullaah, Zaynab, Ruqayyah, Ummu Kulthuum, na Faatwimah) na neema ikawa inazidi akawa Bi Khadiyjah mke mwema mtiifu mwenye mapenzi hakumdharau mumewe kwa kuwa na mali tofauti na leo baadhi ya wanawake wanapokuwa na cheo au mali hawatimizi wajibu wao na wanakuwa na kiburi.

 

Alipofikia Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) miaka arobaini alipenda kujitenga na watu na kufanya ibada mwezi mzima katika pango akichukua chakula na wakati mwengine akiletewa na Bi Khadiyjah ambaye hakudhikika na kupenda kwake kukaa pangoni, alikaa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) katika ibada hii kiasi Alichojaaliwa na Allaah kisha akamshukia Malaika Jibriyl (‘Alayhis Salaam) na kumpa bishara ya Utume katika pango la Hiraa katika mwezi wa Ramadhaan, akatetemeka na kuogopa kwa kumuona Malaika huku akimbana na kumtaka asome akasema mimi sijui kusoma akasema:

“Soma kwa jina la Mola wako…” kisha akasoma Surah ya mwanzo kushuka  ambayo ni Iqraa alipoachiwa alifanya haraka kurudi nyumbani huku akisema “nifunikeni, nifunikeni”.

 

Bi Khadiyjah alipojua kisa chote alimwambia usiogope Allaah Hawezi kukutupa Kwani wewe unaunga undugu, unakaribisha wageni na kuwasaidia wenye matatizo. Ukatulia moyo wa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wasallam) akarudi katika hali ya kawaida, hakuishia hapa mke huyu mwenye akili na hikma bali alimuendea mtoto wa ‘Ami yake Waraqah bin Nawfal na kumsimulia yaliyompata Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akasema:

 

“Hakika aliyemuona ni Naamuus (Jibriyl) aliyekuwa anamshukia Nabii Muusa na ‘Iysa naye ni Nabii wa Ummah huu mwambie awe thabiti…”

 

Akawa Bi Khadiyjah ni wa mwanzo katika waliomuamini akawa pembeni yake anamtetea na kumpa moyo anamsaidia ikawa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) hapatwi na huzuni au matatizo ila akirudi nyumbani anapata faraja na huku Aayah za Qur-aan zikiendelea kushuka.

 

1. Ewe uliyejigubika! 

 

2. Simama uonye!

 

3. Na Mola wako Mlezi mtukuze!

 

4. Na nguo zako, zisafishe. 

 

5. Na yaliyo machafu yahame!

 

6. Wala usitoe kwa kutaraji kuzidishiwa. 

 

7. Na kwa ajili ya Mola wako Mlezi, subiri! 

 

Al-Muddaththir: 1-7

 

 

Kuanzia wakati huo yakabadilika maisha ya Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akaanza maisha mapya yaliyojaa baraka na yenye mashaka vilevile, akampa habari mke wake mwenye imani kwamba wakati wa kulala na raha umekwisha.

 

Akaanza Bi Khadiyjah kulingania Uislam pamoja na mumewe bega kwa bega. Akawafisha Allaah wanawe wa kiume Al-Qaasim na ‘Abdullaah udogoni naye akiwa mwenye subira na kutaraji thawabu kwa Allaah na akamuona shahiydah wa kwanza katika Uislam Summayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) akiwa katika taabu ya mauti mpaka alipochomwa mkuki na kufa.

 

Akamuaga mwanae Ruqayyah (Radhiya Allaahu ‘anha) mke wa ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipoelekea Uhabeshi (Ethiopia) kukimbia maudhi ya Maquraysh.

 

Akashuhudia matatizo mengi na yanayompata Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) katika kulingania haki na kushikamana nayo huku akimjibu ‘Ami yake kwa maneno haya ambayo ameyasimulia Ibn Hishaam katika Siyrah yake,

 

“WaLlaahi ewe ‘Ami yangu lau wangeweka jua katika mkono wangu wa kulia na mwezi kushoto ili niache hili jambo siwezi kuacha mpaka adhihirishe Allaah au niangamie…” Siyratun-Nabawiyah Ibn Hishaam.

 

ingawa wanachuoni wa Hadiyth wamesema maneno hayo kutoka kwa Ya’aquub bin ‘Utbah bin Mughiyrah hayana usahihi ingawa Ibn Hishaam kayaweka kwenye Siyrah yake.

 

Na hivyo ndivyo alivyokuwa Bi Khadiyjah katika kumthibitisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Maquraysh walipowawekea vikwazo vya kisiasa, kiuchumi, kijamii hakusita kusimama na Waislamu katika Shi’ibiy Abiy Twaalib miaka mitatu huku akiacha nyumba yake, alijitolea mali yake yote huku akiwa na miaka sitini na tano.

 

Baada ya kuisha vikwazo kwa miezi sita alifariki Abu Twaalib kisha akafuatia Mujaahidah Muhtasibah As-Sayidat Quraysh Atw-Twaahirah (Khadiyjah bint Khuwaylid (Radhiya Allaahu ‘anha)) kabla ya hijra kwa miaka mitatu.

 

Ikafuatia matatizo baada ya kifo cha Bi Khadiyjah kwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) Kwani alikuwa waziri wa kweli katika Uislam.

 

Na hivyo ikaondoka nafsi iliyotulia kwenda kwa Mola ilipofikia ajali yake baada ya kuacha mfano mwema katika njia ya Da’awah, mke mwema aliyetoa katika njia ya kumridhisha Allaah akapewa bishara njema ya nyumba peponi.

 

Kwa hilo alikuwa Mtume (Swalla Allahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

 

“Bora ya wanawake Maryam bint ‘Imraan, bora ya wanawake Khadiyjah bint Khuwaylid”.

 

 

Ee Mola Mridhie Khadiyjah bint Khuwaylid mke mkweli, Muuminah, aliyeipigania Dini kwa kila alichomiliki duniani.

 

Share