Kafiri Kakanyaga Msahafu Na Hajali, Waislamu Tuchukue Hatua Gani?

SWALI:

 

Huku Kahama kuna kafiri kaisigina masahafu (Quran) kwa kuikanyaga huku akitamba kuwa hawezi kudhurika na chochote je sisi Waislamu tuchukue hatua gani kwa mujibu wa sheria ya Kiislamu tukiwa katika nchi hii ya kitwaaghuti (daaru harbu)


Jibu:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kafiri aliyekanyaga Qur-aan. Hili ni jambo ambalo linatarajiwa kutoka kwa makafiri ambao wana chuki kubwa na kila wakati wanatafuta njia ya kufanya jambo moja au jingine dhidi ya Uislamu na Waislamu.

 

Mara nyingi sisi huwa tuna raghba za ziada na huwa tunafanya mambo ambayo yanaleta athari kinyume na inavyotarajiwa. Uislamu umetupatia njia ya kufanya katika kuondosha munkari kama huo au mwingine. Katika hali zote haitakiwi katika kwa kuondosha munkari huo ukaleta mwingine ambao ni mkubwa kuliko huo. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametupatia mwongozo pale aliposema:

"Yeyote katika nyinyi atakayeona munkari (jambo ovu) aubadilishe kwa mkono wake; na akiwa hawezi basi kwa ulimi wake; na akiwa hawezi basi achukie kwa moyo na huo ni udhaifu zaidi wa Imani" (Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaa'iy, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah). Katika hayo matatu unaweza kufanya lolote kwa mpangilio huo wa Hadiyth.

 

Pia ni vizuri kufuata njia za kisheria kufikisha malalamiko sehemu husika kuliko kuchukua sheria mkononi na hatimaye madhara yakawapata zaidi kuliko manufaa.

 

Na wakati huo pengine ni muhimu kwetu kuweza kuwaelezea wasiokuwa Waislamu kuhusu Qur-aan na jinsi kitabu chochote ambacho ni kitukufu hakifai kufanywa hivyo. Wafahamishwe kuwa kufanya hivyo ni ujinga mambo leo mbali na kuwa wanasema kuwa wamestaarabika. Huo ni wakati wa kuweza kuwaelezea kuhusu Uislamu na kuutangaza na kuyafikisha mafundisho yake kwa wengi wengine ambao huwa daima wanapata picha mbaya ya Uislam kwenye vyombo vya habari.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share