Zingatio: Upanga Ulio Mkali

 

Zingatio: Upanga Ulio Mkali

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kwa kila pumzi tunayovuta basi ni kasoro ya kupungua maisha na ni dalili ya kulisogelea kaburi. Pumzi zetu ndio tofauti ya anayeishi na aliyefariki. Wao walikuwa kama sisi, na sisi tulikuwa kama wao.

 

Muda wetu wa kuishi hapa duniani ni mfano wa kila mwanaadamu kupatiwa kigae; kinapoanguka na kuvunjika, ndio uhai wake umekatika.

 

Waislamu walio wengi wamejiweka mbali na nuru ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kuzidharau fadhila na neema Zake kwetu. Ni wachache wanaokumbuka na kuzishukuru neema hizi.

 

Wala hakuna haja ya kutafuta darubini kuona shughuli za maisha hapa ulimwenguni zinavyotiririka kutoka kilele cha mlima wa Ibilisi. Theluji inayotoka hapa ndio wimbo wa wengi na anasa za wale waliopumbazika na dunia hii.

 

Hata hivyo, ni kichache mno anachokipulizia Ibilisi, mengi tunayafanya na kuyavumbua sisi wenyewe. Ibilisi anabakia kushabikia tu. Ummah huu umejaa vituko hadi Ibilisi kuiga mifano kutoka kwetu badala ya yeye kiongozi wa maasi kutuvumbulia njia za kuasi.

 

Kwa hakika hakuna thamani kubwa aliyopatiwa mwanaadamu kuliko wakati. Kuutumia vyema ndio sababu ya hata wengine kufikia Uprofesa na baadhi kukosa mtoto na maji ya moto (duniani na Aakhirah).

 

Wakati kwa mwenye akili sio wa kuupuuza na kwake hana "passing time" kwa kujishughulisha na ratiba za mipira. Hao ni wale waliouelewa wakati. Wakaandika juzuu za vitabu hadi kutufikia sisi. Katu hakuwa mpotezaji muda miongone mwa wakongwe kama Imaam Al-Bukhariy wala Imaam Shaafi'iy wala Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah, Ibn Kathiyr, An-Nawawiy na wala wa karibuni kama Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy na wengineo. Hizo ndio nyendo za kuziiga kwani zimetoka kwa muasisi wa kuuchunga wakati na si mwengine bali ni kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Maisha yetu ni wakati na ujana ndio njia ya kasi kabisa ya kuukata huo wakati. Naye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba binaadamu hataingia Jannah hadi aulizwe namna alivyoutumia wakati wake hapa duniani:

 

 

“Miguu ya mja haitaruhusiwa kuingia (Jannah) Siku ya Malipo mpaka aulizwe mambo manne: Uhai wake au maisha yake aliishije, ujana wake aliutumiaje, mali yake aliichumaje na aliitumiaje na elimu yake nayo aliitumia vipi [at-Tirmidhiy].

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pia ametutaka kutumia wakati wetu wa ujana, wenye afya, mali, faragha na maisha kabla ya uzee, maradhi, ufukara, mishughuliko na kifo:

 

 

"Chukua faida ya mambo matano (5) kabla ya matano (5): ujana wako kabla ya uzee wako, afya yako kabla ya maradhi yako, mali yako kabla ya ufukara wako, faragha yako kabla ya wakati utakaoshughulishwa na mambo mbali mbali, na maisha yako kabla ya kifo chako." [Al-Haakim]

 

Wasomi na wataalamu tofauti wamejaribu kueleza kuhusu wakati. Hata Waarabu wana msemo: الوقت كا لصيف إن لم تقطعه قطعك Yaani "wakati ni kama upanga, kama hujaukata utakukata." Wakati ni sawa na kushikilia upanga ambao upo nje ya ala yake na unalazimika kuutumia. Hivyo, ni mawili; ama uutumie vyema kwa kuukatia au uutumie vibaya ukukate.

 

Wangapi na wangapi wamekemea vijana kupoteza muda hadi kuacha faradhi ya kutafuta elimu! Kuidharau faradhi ya kuisaka elimu ndio mwanzo wa kupotoka; kwani elimu ndio awlaa (bora) kuliko ibada yoyote. Hata kumpwekesha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) hutaweza kwa kuikosa vilivyo elimu.

 

Sisi ndio tunaopotoeza muda hadi tukatekwa na kuvamiwa bila ya kujihami. Sisi ndio tumekuwa tambara bovu la kanyagio la Marekani na marafiki zake. Tuamkeni na tuache mzaha kwa kutumia vyema kila sekunde yetu katika maisha haya mafupi. Na silaha ya mwanzo kabisa ni kuacha laghai kwa kutafuta elimu sahihi ya Kiislamu.

 

 

Share