Aliyefariki Akihijiwa, Dhambi Zake Zitafutika Japo Hakuwahi Kutubia Alipokuwa Hai?

 

Aliyefariki Akihijiwa, Dhambi Zake Zitafutika Japo Hakuwahi Kutubia Alipokuwa Hai?

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Asalaam Alaykum Warahma tullah taala Wabarakatu

 

Nilikua nauliza kuwa nimewahi kusikia kuwa mtu ambaye anayekwenda Makka kuhiji na Hijjah yake ikakubalika akirudi huwa amefutiwa zambi zake zote na huwa kama mtoto mchanga (yaani hana zambi) sasa swali langu ni hivi:-  Je? Mtu ambaye aliasi sana kwa kufanya dhambi nyingi hapa duniani na akafa wakati hakuwahi kutubia zambi zake hizo. Je, mtu kama huyu akienda kuhijiwa makka na mtoto wake hizo zambi zake atafutiwa zote na atakuwa hana zambi?Naomba ufafanuzi juu ya hili wabillah tawfiq.

 

Asalaam Alaykumu Warahma tullahi Wabarakatu

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika hili ni swali zuri na maelezo uliyoyaeleza kuhusu kufutiwa dhambi kwa anayehiji Hijjah ni ya sawa kabisa, inatokana na Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iliyo sahihi kabisa. Hata hivyo, ni sikitiko kubwa sana kuwa zipo baadhi ya Hadiyth ambazo zimekosa kueleweka inavyostahiki.

 

 

Ukiacha aliyekufa ambaye anahijiwa, hata aliyehai anatakiwa baada ya Hijjah hiyo iliyokubaliwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) awe atajikita katika Uislamu wa sawa, awe na msimamo katika hilo mpaka aage dunia katika njia hiyo ya Uislamu. Mara nyingi watu huenda wakafanya Hijjah au hufanya kila mwaka kwa kumchezea shere Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Wanafanya vipi hilo? Wanafanya kwa kurudi katika maasiya baada ya Hijjah hivyo Hijjah zao hutuyakinishia kuwa hazikukubaliwa kabisa, kwani Ibadah inayokubaliwa inatakiwa imuweke mtendaji katika ‘amali njema daima dawamu.

 

 

Sasa ikiwa anayefanyiwa Hijjah alifanya madhambi makubwa au matendo ya kumtoa katika Uislamu, Hijjah hiyo haitamsaidia lolote wala chochote. Msingi mkubwa wa Uislamu ni kuwa lazima mwanaadamu atubie kwa madhambi yake kabla hajaaga dunia pamoja na kujirekebisha na kufanya mema na mazuri. Ikiwa hakufanya hivyo, Ibadah anazofanyiwa na wengine (jamaa zake) hazitomsaidia na chochote

 

 

Hivyo, tuswali wenyewe kabla ya kuswaliwa na tutubie wenyewe tusitarajie kufanyiwa toba na wengine.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share