Wamesema Uongo Serikalini Kuwa Hawakuoana Wapate Pesa, Je Watoto Wao Ni Halaal?

SWALI:

 

Sheikh jee inafaa kha mwanamke kwenda serikalini na kusemaeye hana mume na hivyo kushughulikiwa na serikali kwa mambo yote. wakati mwanamke huyu ameolewa kwa sheria zote za kiislaam? Vile vile mume mtu akiulizwa na yeye hujibu huyu si mke wangu pengine husema huyu ni ndugu yangu au jirani angu. wanapopata mtoto husema nimezaa na boy friend wangu na amenikimbia. Jee sheigh ndoa hii bado inakuwepo? Jee watoto wanakuwa halali? Naomba msaada wako kwanihaya ni maisha ya wengi tuliopo kwenye hizi nchi za ulaya.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza ningependa kuziusia nafsi zetu na nafsi ya kila mwenye kuamini Allaah na Siku ya mwisho kuwa ni vyema kushikamana na ushauri wa Allaah wa kututaka tuwe pamoja na wasema kweli ili tupate kufaidika na yaliyoandaliwa wasema kweli, kwani wasema kweli watatu kwa kusema kweli tu walikubaliwa tawbah zao Allaah anasema:

 

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na kuweni pamoja na wakweli” At-Tawbah: 119.

 

Katika Uislamu uongo au kusema uongo hakukubaliwi isipokuwa katika sehemu maalumu, kwani uongo unampelekea mtu kuwa mtu wa motoni kama ilivyothibiti katika Hadiyth ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wakati aliposema:

“Ni juu yenu kusema kweli… Na ole wenu na kusema uongo… kwani uongo unampeleka mtu motoni” Imepokelewa na Muslim, kitabul Birr na as-Silah na al-Adab, mlango ubaya wa uwongo na uzuri wa ukweli na fadhila zake.

 

Wakati fulani Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa je Muislamu anaweza kusema uwongo?! Akasema: Laa.

 

Sababu kubwa ya haya ni kuwa mtu huwa hataki kulipa kodi ya nyumba au vyengine, na vyote ni katika mambo yanayotakiwa kusimamiwa na mume ili astahiki kuitwa mume na kustahiki uqawanah kwa mkewe na kufanya hivyo ni sadaqa na malipo yake kwa Mola wake kama atakuwa anamhudumia mkewe na watoto wake, vinginevyo anajikosesha thawabu na kheri nyingi.

Ingia pia kwenye kiungo hiki kwa faida zaidi:

 

Nasaha Kwa Wakimbizi Wanaoishi Kusema Hawajaoana Ili Wapate Ruzuku Ya Serikali

 

Hivyo kwa mwanamke au mke wa mtu kwenda serikalini na kusema kuwa hana mume ili ahudumiwe si jambo linalokubalika katika Uislamu kwani huko ni kuutukanisha Uislamu na Waislamu kwa ujumla na ni kusema uwongo ambao makemeo yake yako wazi.  Hata hivyo huwa hajaachika.

 

Pia mume mtu anaposema kuwa huyu si mke wangu huwa bado hajaachika kwani hilo si miongoni mwa matamshi ya talaka, lakini huwa amesema uwongo na haukubaliki pia katika dini; kwani hapo si pahala paliporuhusiwa kusema uwongo.

 

Watoto au mtoto huwa wa huyo mume pamoja na hayo waliyoyafanya, na ndoa yao bado ipo kwani hakuna kilichoivunja.

 

Nasaha ni kuwa tuangalie nini cha kukifadhilisha na cha kuchagua; kusema uwongo na kufanya ujanja ili upate urahisi wa maisha –kama wanavyodhania wengi- na kujiwekea mapesa ili kuyatuma Afrika huku ukijipalilia majinga ya moto na kukosa fadhila za kuwahudumia ahli zako? Au kujiandaa na maisha ya Aakhirah –yasiyoaminiwa na wengi -ambayo ni bora na ya kudumu, Qur-aan inasema:

 

“Lakini nyinyi mnakhiari maisha ya dunia!  Na Akhera ni bora na yenye kudumu zaidi.” Al-A'laa:16-17.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share