Anayefanya Kazi Benki Anahesabiwa Kuwa Ni Mpokea Rushwa? Nini Hukumu Ya Kufanya Kazi Benki?

SWALI:

Assalam aleykum Warahmatollah wabaratoh.

Kwanza napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Al-hidaaya kwa ushirikiano mzuri wanaotoa kwa waislam wote duniani.

Swali langu ni nini hukumu ya mtu afanyae kazi Bank. Je anahisabika kama mtoa na mpokea rushwa? Natanguliza shukrani kwa ushirikiano wenu katika hili.


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

Kwanza tunakushukuru kwa shukurani zako na tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Atupe tawfiyq tuweze kuendelea kutoa ushirikiano na mafundisho yenye kuwanufaisha Waislam inshaAllaah.

Asli miongoni mwa mambo yanayosababisha watu kukosa haki zao au wengine kudhulumu haki za wengine kwa kujichotea haki zisizo zao au kupewa nyadhifa wasizostahiki kwa njia isiyo ya haki ambayo hueleweka kama ni Rushwa. 

Uislamu umepiga vita kila lenye kusababisha na kupelekea watu kufikia kuwadhulumu wengine kwa jina la aina yo yote ikiwemo rushwa, Uislamu umeipiga vita rushwa kwa nguvu zake zote na kutahadharisha kuwa wahusika wake ni watu wa motoni, hivyo Waislamu hawatakiwi kujishughulisha na jambo hilo kwani ni katika mambo yaliyo haramu na wenye kushiriki rushwa huwa ni watu wa motoni kama ilivyothibiti kati Hadiyth:

“Laana ya Allaah iwe juu ya ar-Raashiy (mtoa rushwa) na (mpokea rushwa).” At-Tirmidhiy.

Hiyo ndio hukumu ya mtoa rushwa na mpokea rushwa.

 

Hukumu ya mtu afanyae kazi benki.

Mabenki karibu yote huwa yanafanya kazi kwa kutumia riba (interest) katika mu’aamalat wake, na riba ni katika Aliyoyaharamisha Allaah na Mtumewe (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) , hivyo mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho hatarajiwi kuchepa katika fukwe za makatazo yake wachilia mbali kuogelea katika Aliloharamisha Allaah; kwa kufanya kazi katika mabenki haya tunayoyaelewa kuwa ni ya kuvutia na kushajiisha riba, pia hatakiwi kuchukuwa mikopo kutoka katika mabenki hayo vile vile kwani ndani yake huwa kuna riba isipokuwa ikiwa mkopo huo hauna riba (interest free), Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Anasema:

“Enyi mlioamini! Mcheni Allaah, na acheni riba zilizobakia, ikiwa nyinyi ni Waumini.  Basi mkitofanya jitangazieni vita na Allaah na Mtume wake. Na mkitubu, basi haki yenu ni rasilmali zenu. Msidhulumu wala msidhulumiwe.” Al-Baqarah: 278-279.

Kufanya kazi katika pahala ambapo yanayoshughulikiwa ni kila lenye kueleweka na kufahamika katika Uislamu kuwa ni vita na Allaah na Mtumewe ni haramu kwa mwenye imani ya Kiislamu, bali benki si pahala pa kujipachika na kuwepo mwenye kuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na mfanyakazi wa benki huwa anashughulika na uandishi na utayarishaji na ushughulikiaji wa mambo ya riba na tunajua kuwa imethibiti kuwa Muandishi (katika makubaliano na ushughulikiaji wa mambo ya mapatano ya riba, na hapa tunamzungumzia Muandishi (mfanyakazi) wa benki), na Mashahidi wawili, na Wakala kama ilivyo katika Hadiyth za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni watu waliolaaniwa:

“Allaah Amemlaani mla riba, wakala (muwakilishi) wake, mwandishi wake na mashahidi wake wawili; wote in sawa” Muslim.

Je anahisabika mfanya kazi benki kama mtoa na mpokea rushwa? Huenda ndugu yetu muulizaji anakusudia riba kwani mabenki hakuna rushwa labda iwe rushwa katika kuchaguliwa nani wa kupewa mkopo na kadhalika; hata hivyo tumejaribu kwa uwezo wake Allaah kugusia mambo yote mawili Riba na Rushwa na mfanya kazi benki huwa anahisabika bila ya shaka yoyote ile katika waandishi au mashahidi wa riba na hukumu yake pamoja na mtoa rushwa na mpokea rushwa ndio kama ilivyokuja na kuthibiti katika Hadiyth.

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share