01-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Utangulizi

 

Utangulizi

 

 

Mmoja katika wana falsafa wa zamani alisema:

“Haki yote haiwezi kumilikiwa na upande mmoja, wala makosa yote hayawezi kuwepo upande mwingine, bali kila upande husibu sehemu yake. Mfano wa kundi la vipofu waliopelekwa mbele ya tembo wakatakiwa wamguse mwili wake, kisha kila mmoja aelezee umbile lake.

Katika muda mfupi waliopewa, hapana aliyewahi kukamilisha kuushika mwili wote. Kila mmoja alifanikiwa kugusa sehemu tu.

Aliyeushika mkonga akidhani kuwa amemshika tembo wote akasema: “Mwili wa tembo ni mrefu mfano wa gogo la mti”,

Aliyeshika mgongo akasema:

“Hapana, bali mwili wa tembo ni mfano wa jabali dogo”,

Aliyeshika sikio akasema:

“Nilivyouona mimi mwili wa tembo ni mpana, duara na laini”.

Kila mmoja anahadithia juu ya ile sehemu aliyodiriki kuishika katika muda mfupi ule akidhani anatoa maelezo kamili. Wote wamesema kweli, lakini kila mmoja amehadithia sehemu tu ya ukweli anaoujua yeye akidhani kuwa ndio ukweli wote.”

 

Hitilafu husababishwa na mambo mengi, yakiwemo upeo wa kufahamu, kupenda, matamanio ya nafsi, mielekeo ya elimu, ya kifikra, kuiga waliotangulia, kupenda umaarufu, kupenda ukubwa, hitilafu za ustaarabu. Wengine huiga waliyowakuta nayo wazee wao, na wengine wanafuata mafundisho ya walimu wao wanaowaamini n.k. Na wengine huiendeleza hitilafu kwa sababu ya ubishi au kiburi tu, hata kama wataiona haki mbele yao.

Si vibaya kuhitilafiana, kwa sababu Allaah Ametuumba kila mmoja na akili yake pamoja uwezo wake wa kufahamu.

Allaah Anasema:

 

وَلَوْ شَاء رَبُّكَ لَجَعَلَ النَّاسَ أُمَّةً وَاحِدَةً وَلاَ يَزَالُونَ مُخْتَلِفِينَ .إِلاَّ مَن رَّحِمَ رَبُّكَ وَلِذَلِكَ خَلَقَهُم

«Na Mola wako Angelipenda Angewafanya watu wote wakawa umma mmoja. Lakini hawaachi kukhitalifiana, Isipokuwa wale ambao Mola wako Amewarehemu; na kwa hiyo ndio Allaah Amewaumba.»

Huud-118-119

 

Anasema Al Hasan Al Basry: وَلِذَلِكَ خَلَقَهُمْ maana yake ni kuwa; Amewaumba ili wakhitalifiane.

 

Wenye kukhitilifiana wanaweza kusikilizana na kufahamiana ikiwa hapana chuki baina yao, lakini chuki inapoingia, hayapatikani tena masikilizano wala kufahamiana. Chuki inaondoa mapenzi na inavunja uhusiano mwema na inaendeleza bughudha na kuondoa uwezekano wowote wa masikilizano.

 

Imepokelewa kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) usiku mmoja aliamka uso wake ukiwa mwekundu huku akisema:

 

لا إِلهَ إِلاّ الله، وَيْلٌ للعَرَبِ، مِنْ شَرَ قَدِ اقْتَرَب

Laa ilaaha illa Allaah, Ole wao Waarabu kwa shari iliyo karibu

Alirudia maneno haya mara tatu.

 

Maulamaa wanasema kuwa;‘Hii ilikuwa ishara kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) juu ya hitilafu itakayotokea baada yake’.

 

Hitilafu iliyopo hivi sasa baina ya Shia na Sunni inakula kibichi na kikavu.

Mamia ya Waislamu wanauliwa kila siku huko Iraq, na wanaendelea kuuliwa, na mamilioni wengine wamejeruhiwa. Mamilioni wamekwishaihama nchi yao, na mamilioni hawana kazi wala bazi.

Lebanon, nchi iliyojaa neema, nchi ya elimu na ziraa. Nchi ya historia na sanaa, leo kila kitu kimesimama katika nchi hii kwa sababu ya fitna ya umadhehebu. Nchi haina serikali, ina majeshi mawili, kila moja linadai kuwa wao ndio wenye kuipenda nchi. Ina makundi mawili, kila moja linalituhumu jingine kuwa ni vibaraka. Watu hawaelewi wanapelekwa wapi, kila siku mapambano ya risasi na mabomu.

 

Huko Yemen, maelfu ya watu wamekwishapoteza maisha yao katika mapambano baina ya majeshi ya serikali na makundi ya watu wa kabila la Houthi wenye kufuata madhehebu ya Shia Ithnaashariyah.

Hii ni fitna iliyopenyezwa katika mwili wa Waislamu kwa ajili ya kuwagawa. Inatumiliwa na kuchochewa na wale wasiopenda kuuona umma wao umetulia huku ukipiga hatua katika kuziendeleza nchi zao na kuwaelimisha watu wao.

Na katika kila pembe ya ulimwengu chuki hizi zinaanza kupasua njia kidogo kidogo na ni Allaah peke Yake Anaelewa wapi yataishia.

 

Mambo yaliyotokea miaka elfu moja mia nne iliyopita yanaendelea kuwagawa na kuwafarikisha Waislamu hadi hivi sasa katika karne hii ya satellite na computer.

Umma huu ni Umma mmoja, Mungu wetu ni Mungu Mmoja, na Dini yetu ni moja na Mtume wetu ni mmoja, Lengo letu ni moja na adui yetu ni mmoja, kwa nini basi hatuungani tukawa kitu kimoja?

Ikiwa kuwapenda watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni Ushia, basi sisi sote ni Mashia, na ikiwa kuwapenda Masahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum) ni Usunni, basi sote tuwe Masunni. Waislamu hawatakuwa na kheri yoyote ikiwa watawachukia watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ambao Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ametuamrisha tuwaswalie kila tunapomswalia.

 

Na Waislamu hawatakuwa na kheri yoyote ikiwa watawachukia Sahibu zake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) (Radhiya Allaahu ‘anhum), ambao baada ya kufariki dunia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), wao ndio walioibeba bendera na kuueneza Uislamu kila pembe ya ulimwengu.

Waislamu wanatakiwa waone fahari kubwa kila wanapotajwa Masahaba hawa watukufu (Radhiya Allaahu ‘anhum), kwa sababu wao ndio waliotuletea Uislamu. Wao ndio waliotufikishia Qur-aan tukufu ambayo ni Nuru itokayo kwa Mola wetu.

 

Allaah Amewajaalia wao kuwa ndiyo sababu ya kutufikia dini hii kote huku tuliko. Kwa juhudi yao kubwa na kujitolea kwao mhanga kwa hali na mali waliuwezesha Uislamu kuingia na kuenea na kufuatwa na kupendwa Arabuni kote, Iran, Asia, Afrika hadi Ulaya na Marekani.

Wangelikuwa watu hawa ni makafiri basi wangelituletea ukafiri badala ya Uislamu. Wangelituletea misalaba na masanamu badala ya Qur-aan na Swalah na salamu amani.

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) kuwa hitilafu baina ya madhehebu ya Kiislamu si katika kiini cha dini na asili ya mafundisho yake, kama vile kuabudiwa Allaah Mmoja na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ni Mtume Wake. Hitilafu haikuwa juu ya Qur-aan tukufu, kwani AlhamduliAllaah Waislamu wote kwa pamoja wanaamini kuwa Qur-aan hii tuliyonayo hivi sasa ndiyo ile ile aliyoteremshiwa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) miaka elfu moja mia nne iliyopita.

 

Tunaelewa kuwa walikuwepo baadhi ya Maulamaa wachache wa madhehebu ya Kishia mfano wa Nuwriy At-Tubrusiy aliyeandika kitabu ‘Faswlul Khitwaab fiy ithbaat tahriyf kitaab Rabbil Arbaab’, akidai ndani ya kitabu hicho kuwa Qur-aan hii tuliyonayo ilibadilishwa na kupunguzwa na kuzidishwa. AlhamduliAllaah katika wakati wetu huu hapana tena anayeziamini kauli hizo hata miongoni mwa wengi kati ya Mashia, kiwa si wote, na kama watakuwepo basi watakuwa wachache sana.

 

Tunamshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) pia kuwa hitilafu hii haikuwa katika kuharamisha au kuhalalisha mambo yanayojulikana katika dini kuwa ni ya dharura kama vile uharamu wa Pombe, kula nyama ya nguruwe n.k. Juu ya kuwa hapana shaka yoyote kuwa ipo hitilafu juu ya baadhi ya mambo yanayohusiana na Itikadi ‘Aqiydah’.

Hapana shaka yoyote kuwa ipo hitilafu juu ya baadhi ya mambo yanayohusiana na Itikadi ‘Aqiydah’, kama vile kumuomba mwengine asiyekuwa Allaah na kuyatukuzu makaburi ya watu wema.

Naelewa pia kuwa wapo wanaojinasibisha na Ahlus Sunnah wenye kuwaomba wengine wasiokuwa Allaah na kuyatukuza makaburi ya watu wema, lakini tofauti iliyopo baina ya Sunnah na Shia ni kuwa Maulamaa wa Ahlus Sunnah wanayakemea na kuyakataza mambo haya, wakati maulamaa wa Shia wanayanyamazia na kuyapa kipaumbele.

 

Share