02-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Al-Mahdi Na 'Umar

 

Al-Mahdi na ‘Umar

 

 

Anasema Dr. Ahmad Al-Kaatib mwanachuoni wa Kishia kutoka Iraq ambaye ni mwalimu katika vyuo vikuu mbali mbali vya dini huko Iraq, Kuwait na Iran na ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuia ya Majadilianao ya Ustaarabu, 'Al Hiwaar al Hadhwaariy', ambayo makao yake makuu yapo London, alisema:

"Nimefanya utafiti ulionipa uhakika kuwa hitilafu iliyopo baina ya Sunnah na Shia hauna msingi wowote na imenithibitikia baada ya kuidurusu kadhia hii kuwa hitilafu zilizokuwepo ni za kisiasa tu na wala si za itikadi.

Baada ya kufanya utafiti wangu ulionichukua muda mrefu sana imenithibitikia kuwa hitilafu iliyokuwepo baina yetu (Shia na Sunnah) ni juu ya Imam Al Mahdi na pia yale madai kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimpiga Bibi Faatwimah  siku ile watu walipofungamana na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Baada ya kumaliza utafiti wangu," anaendelea kusema Ahmad Al Kaatib ambaye hadi hivi sasa ni mwalimu mkubwa wa madhehebu ya Shia Ithnaashariyah; "imenidhihirikia kuwa madai hayo kuwa ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimpiga Bibi Faatwimah hayana msingi wowote na kwamba ni uzushi ulioenezwa na kuandikwa katika vitabu mbali mbali vya historia kwa ajili ya kuipa nguvu nadharia ya Uimamu, nadharia ambayo inafutika ikithibiti kuwa ‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alikubali kwa hiari yake kufungamana na Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan (Radhiya Allaahu ‘anhum) walipochaguliwa kuwa Makhalifa, kwa sababu angelikuwa Imam ‘Aliy amechaguliwa na Allaah, basi asingekubali kufungamana nao kwa hiari yake.

Wazushi wa kisa hicho walidai kuwa ‘Aliy alikubali kufungamana na Abu Bakr baada ya ‘Umar kuingia kwa nguvu nyumbani kwake na kumpiga mkewe ambaye ni  Bibi Faatwimah binti wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) mpaka mimba ikamtoka."

 

Anasema Ahmad Al-Kaatib:

"Nilikifanyia uchunguzi kisa hiki lakini sijakikuta katika kitabu chochote chenye kutambulika na kuaminika miongoni mwa vitabu vya Kishia kama vile Al-Kafi na vyenginevyo.

Kinachokikanusha zaidi kisa hicho ni ule uhusiano mzuri uliokuwepo baina yao hadi kufikia kuwa ‘Aliy na Faatwimah walimuozesha binti yao Ummu Kulthum kwa ‘Umar.

Itawezekanaje basi, kwa mama akubali kumuozesha binti yake mtu aliyempiga mpaka mimba ikamtoka?"

"Ama kisa cha Uimamu," anaendelea kusema Ahmad Al-Kaatib: "Hata Ayatollah Sistani ametamka kuwa jambo hili si katika mambo ya msingi wa dini kwa Shia, na kwamba linaweza kujadiliwa.

Nilifuatilia vitabu vilivyoandikwa na waandishi wa Kishia katika karne ya tatu na ya nne na ya tano Hijri nikaona kuwa hapana ushahidi wowote unaothibitisha kuwa Imam huyu alizaliwa, na kwamba Sayed Murtadha na Al Umani na wengine wanasema: "Sisi tunaona kuwa haya ni mambo ya kukisia tu kwa dalili za kiakili na hatuna dalili za kielimu zisizopingika.

Kwa hivyo nadharia ya kuwepo kwa Imam wa kumi na mbili mwenye kusimamia, anayetokana na Imam Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliyepewa jina na Muhammad bin Hasan Al-Askary na nadharia ya kutoweka kwake, si katika itikadi za Ahlul Bayt, bali wamenasibishwa nazo na baadhi ya waandishi.

Na hivi sasa kwa vile serikali ya Iran imeamua kuipa nguvu nadharia ya Utawala wa mwanachuoni 'Wilayat Al-Faqiyh' na imeamua kufuata nidhamu ya kuchagua viongozi wa dini kwa njia ya kushauriana, 'Shuura' na kuchagua viongozi wa nchi kwa njia ya demokrasia (democracy), kwa hivyo haya yanafuta ile kauli ya kuwa kiongozi lazima awe aliyechaguliwa na Allaah, na badala yake mtu yeyote anaweza kuwa kiongozi ikiwa watu wataridhka naye na kumchagua, (pia siyo lazima awe katika ‘Ahlul-Bayt’)

 

Kwa ajili hiyo ile khitilafu iliyokuwepo baina ya Shia na Sunnah juu ya Uimamu sasa itakuwa ishaondoka pia kwa sababu Shia hawaamini tena juu ya ulazima wa kuwepo Imam aliyetoweka akaingia ndani ya pango na wala hawasubiri tena kutoka pangoni alipoingia miaka elfu moja iliyopita ili wapate kuisimamisha dola ya Kiislamu.

Na lile sharti ya kuwa Imam mwenye kuwaongoza Waislamu lazima awe Aliyechaguliwa na Allaah na awe aliyekingwa asiyefanya makosa anayetokana na ukoo maalum, nayo pia imeondoka kwa sababu kiongozi hivi sasa anachaguliwa kwa njia ya uchaguzi au kwa kushauriana ‘Shuura’."

Mwisho wa maneno ya Al Kaatib

(Website ya Al Arabiyah.net. Tarehe 27 May 2008)

 

Anasema mwanachuoni mwengine maarufu Dr. Muusa al Musawiy katika kitabu chake ‘Ash-Shi’ah wat-Tashyi’’:

«Baada ya utafiti mkubwa nilioufanya katika kulichambua tatizo hili la hitilafu kubwa iliyopo baina ya Shia Ithanaashariyah na Ahlus Sunnah, nimegundua kuwa yale yaliyotokea baada ya kufariki kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) siyo sababu ya hitilafu hii kubwa, wala si kwa sababu ya kuwa ‘Aliy ndiye anayestahiki ukhalifa baada ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kwa sababu nawaona wenye kufuata madhehebu ya Shia Zaydiyah wapo kwa mamilioni katika ulimwengu na wanaishi kwa wema na mapenzi na masikilizano baina yao na  Masunni.

Kwa hivyo sababu ya hitilafu baina ya Shia Ithnaashariyah na Madhehebu mengine ya Kiislamu ni ule msimamo wao dhidi ya Makhalifa walioongoka na kuwatukana kwao na kuwalaani, jambo ambalo halipo upande wa Shia Zaydiyah na makundi mengine. Lau kama Shia Ithnaashariyah walingelifuata mwenendo wa Shia Zaydiyah basi hitilafu ingelipungua sana na tatizo lingekuwa dogo. Lakini Shia Ithnaashariyah wameingia katika shimo la kuwatukana Makhalifa walioongoka na kuwalani na kuwashambulia,  jambo linalosababisha hitilafu hii izidi na kuongezeka.»

Ash-Shi’ah wat-Tashyi’. Uk.4

 

Kutokana na maelezo haya ya Maulamaa wa Kishia, inatubainikia kuwa laiti kama wafuasi wa Shia wangeliacha mwenendo wa kuwatukana na kuwalaani Masahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na wake zake Mama wa Waislamu, na lau kama wataacha mwenendo wa kuwatukana na kuwalaani Waislamu wenzao katika siku za Muharram na kuwaapiza kwa kula kiapo kuwa lazima watalipa visasi vya kuuliwa kwa Al-Husayn, basi sehemu kubwa ya chuki baina ya makundi mawili haya yangeondoka.

 

Masunni wanawaheshimu sana na kuwatukuza watu wote wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na wanawaheshimu pia Masahaba wake (Radhiya Allaahu ‘anhum), na wanaamini kuwa wao ni watu bora ambao Allaah Ameridhika nao, kama ilivyoandikwa katika Qur-aan tukufu.

Masunni wanajitenga na kila aliyeshiriki katika vile vita vilivyosababisha kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu), na wanajitenga na wote waliomuua na waliosababisha kuuliwa kwa Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) na aila yake, na wanaamini kuwa wameuliwa kwa dhulma na kwa uadui, na kwamba wote wamekufa Shahiyd.

 

Masunni wanashangazwa wanaposikia vilio na maneno ya kulipwa visasi katika vikao vya Al-Husayniyah يا لتارات الحسين. Wanajiuliza; visasi hivyo watalipiwa nani wakati wote waliomuua Al-Husayn (Radhiya Allaahu ‘anhu) wamekwishafariki dunia.

 

Al Hurr bin Yazid At-Tamimiy keshakufa, Shumar bin Dhil Jawshan keshakufa, Zara'a bin Shariyk keshakufa, ‘Umar bin Sa’ad  keshakufa, UbayduAllaah bin Ziyad naye pia keshakufa, na wote walioshiriki katika vita vile wamekwisharudi kwa Mola wao tokea miaka elfu moja mia nne iliyopita.

Maneno haya ya kutaka kulipa visasi yanatafsiriwa na Ahlus Sunnah kuwa wao ndio wanaokusudiwa, na haya ni katika chuki zilizopandikizwa na wasiopenda kuwaona Waislamu wa kila  Madhehebu wanapendana na kushirikiana katika kuziendeleza mbele dola zao.

 

 

Share