10-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Kuoleana Na Majina Ya Watoto

 

Kuoleana

 

Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ameoa mabinti wa Abu Bakr na ‘Umar. Na ‘Uthmaan alioa mabinti wawili wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), Mabibi Ruqayyah na Ummu Kulthuum, na alijulikana kwa jina la 'Dhiy Nnurayn', na maana yake ni Mwenye Nuru mbili kwa sababu ya mabinti hao wawili (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Alihuzunika sana alipofariki mkewe wa pili Bibi Ummu Kulthuum (Radhiya Allaahu ‘anha) na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipomuona katika hali ile akamuuliza:

 

"Kipi kinachokuliza ewe ‘Uthmaan?"

‘Uthmaan akajibu:

"Ninalia ewe Mtume wa Allaah kwa sababu kumekatika kunasibiana kwangu na wewe."

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akamwambia:

"Usilie ewe ‘Uthmaan, naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake, lau kama nina mabinti mia wanakufa mmoja baada ya mwengine, basi ningekuozesha mpaka wasibaki katika mia hao hata mmoja." At-Twabaraaniy na wengine.

 

Hii ni katika dalili za mapenzi makubwa yaliyokuwepo baina ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) pamoja na watu wa nyumba yake juu ya Maswahaba (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimuoa Bibi ‘Aaishah binti wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq na alimuoa Hafswah binti wa ‘Umar bin Al-Khattwaab na alimuoa pia Ummu Habiybah Ramlah binti Abi Sufyaan (Radhiya Allaahu ‘anhum).

 

‘Aliy (Radhiya Allaahu ‘anhu) alimuozesha binti yake Ummu Kulthuum kwa ‘Umar bin Al-Khattwaab.

(Al-Kafi/346/5)

Alipouliwa Ja’afar bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu), mkewe Asmaa binti Umays (Radhiya Allaahu ‘anha) aliolewa na Abu Bakr Asw-Swiddiyq na alipofariki Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu), Bibi Asmaa aliolewa na ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Ja’afar Asw-Swaadiq ni mjukuu wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq, kwa sababu Muhammad Al-Baaqir mjukuu wa Al-Husayn alimuoa Ummu Farwah mjukuu wa Muhammad bin Abi Bakr, na kutokana na ndoa hiyo akapatikana Ja’afar Asw-Swaadiq. Kwa hivyo Ja’afar ni mjukuu wa Abu Bakr na mwanawe Muusa Al-Kaadhwim anakuwa pia mtoto wa mjukuu wa Abu Bakr na kwa njia hii Maimam wote waliofuata wa Shia ni wajukuu wa Abu Bakr Asw-Swiddiyq (Radhiya Allaahu ‘anhum jamiy’an).

 

Imepokelewa kuwa Ja’afar Asw-Swaadiq alikuwa akisema:

“Amenizaa Abu Bakr mara mbili.”

Siyar A’alaam an-Nubalaa

 

Abaad bin ‘Uthmaan bin ‘Affaan alimuoa Ummu Kulthuum binti yake AbduAllaah bin Ja’afar bin Abi Twaalib.

Shia wa Ahlul Bayt/141

 

Sakina bint Al-Husayn bin ‘Aliy bin Abi Twaalib aliolewa na Mus’ab bin Az-Zubayr bin Al-A’waam.

Twabaqaat ibn Sa’ad183/5

 

(Allaah Awe radhi nao wote)

 

 

 

Majina ya watoto

 

‘Aliy bin Abi Twaalib aliwapa wanawe majina ya Abu Bakr na ‘Umar na ‘Uthmaan.

Kashf al-Ghummah 2/67.

 

Al-Hasan bin ‘Aliy alimpa mmoja wa watoto wake jina la Abu Bakr.

Kashf al-Ghummah 2/198.

 

Muusa bin Ja’afar alikuwa na watoto aliowapa majina ya ‘Aaishah na ‘Umar.

Kashf al-Ghummah 3/29.

 

Share