11-Mapenzi Ya Ahlus-Sunnah Juu Ya Ahlul-Bayt: Wajibu Wetu

 

Wajibu Wetu

 

Itakuwa siku ya furaha kubwa tutakapowaona wafuasi wa Sunni wakipeana mikono na wafuasi wa Shia kwa furaha bila kinyongo wala undani. Lakini hatuwezi kulifikia lengo hilo ikiwa Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wataendelea kutukanwa na kukashifiwa na kulaaniwa.

Hatuwezi kulifikia ikiwa watu wataendelea kulizuru kaburi la Majusi Abu Luulua aliyemuua Khalifa wa Waislamu na Swahibu yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) ‘Umar bin Khattwaab (Radhiya Allaahu ‘anhu) na kuliita kaburi la Majusi huyo ‘Baba Shujaa ddiyn’ ‘Baba shujaa wa  dini.’

Dini gani wakati mtu huyu hakuwa Muislamu? Kwa nini wanakubali kuisherehekea siku ambayo Mmajusi aliyekuwa akiabudu moto alimuua Khalifa wa Wasilamu?

 

«Enyi viongozi wa Shia wenye akili na hekima, upigeni vita mnasaba huu kwa ajili ya umoja wa Waislamu. Inatosha jamani kueneza chuki kwa mambo yaliyotokea miaka 1500 iliyopita.»

 

Msisahau kuwa ‘Umar huyu ni ‘ami yake Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), kwa sababu Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amemuoa bini yake Hafswah (Radhiya Llahu ‘anha), na ‘Umar huyu huyu ni mume wa Ummu Kulthuum binti ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu).

Nilifurahi sana nilipomskia Dr. Sabah Al-Khuza’iy katika channel Al-Mustaqillah, na huyu ni mtaalamu anayesomesha katika mojawapo ya Vyuo vikuu huko Uingereza, na ni mfuasi wa madhehebu ya Shia.

Anasema Dr. Khuza’iy:

 

«Sielewi kwa nini viongozi wetu wa Shia wanashadidia sana jambo hili la kufanya matanga kila mwaka wakidai kuwa hiyo ni siku aliyouliwa Bibi Faatwimah binti wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na ndani ya matanga hayo wanalaaniwa Maswahaba wakubwa wa  Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) hasa Makhalifa wawili wa mwanzo, Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhum).

Mimi siamini kuwa ‘Umar wala Abu Bakr walimshambulia Bibi Faatwimah! Haya yote ni uzushi mtupu uliotungwa na watu wasioitakia kheri dini yetu, na baadhi ya watu wakausadiki uongo huo na kuueneza.

Inaingia akilini jamani kwa watu hawa waliosifiwa ndani ya Qur-aan tukufu na katika hadithi mbali mbali za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam), na huyu Abu Bakr aliyeruhusiwa na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuswalisha wiki nzima ya mwisho kabla ya kufariki Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alikuwa akimtizama huku akitabasamu, na hii ni dalili ya kuridhika naye.

Na ‘Umar ambaye ‘Aliy alikubali kumuozesha binti yake Ummu Kulthuum. Kama kweli ‘Umar ndiyo sababu ya kufariki kwa Bibi Faatwimah wangelikubali kumuozesha binti yao mtu katili?

Hadithi sahihi kwa pande zote mbili Shia na Sunni inasema:

« Atakapokujieni mtakayeridhika na dini yake na khulka zake muozesheni. »

Bila shaka ‘Aliy na Faatwimah waliridhika na dini ya ‘Umar ndiyo maana wakakubali kumuozesha binti yao.

Hivyo ‘Aliy huyu aliyepigana vita vya Khaybar kwa ushujaa mkubwa akapambana na ‘Amr ibn ‘Abdi Wudd wakati Maswahaba wengine walihofia kupambana naye, leo ‘Aliy huyu avunjiwe heshima ya mke wake kisha anyamaze kimya? Isitoshe  ampe tunza muovu huyo ya kukubali kumuozesha binti yake?

Mimi, aliendelea kusema Dr. Al-Khuzaiy:

«Ni Shia wa ‘Aliy yule shujaa aliyeuvunja mlango wa Khaybar, nilikuwa pamoja naye siku ile, na nilikuwa pamoja na ‘Aliy siku ile alipokubali kuswali nyuma ya Abu Bakr wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alipokuwa akiumwa maradhi yake ya mwisho. Nilikuwa na ‘Aliy siku ile alipochaguliwa Abu Bakr kuwa Khalifa wa Waislamu na ‘Aliy akamkubali na akaswali nyuma yake, na nilikuwa pamoja na ‘Aliy siku ile alipokubali kuswali nyuma ya ‘Umar bin Al-Khattwaab baada ya kuchaguliwa kuwa Khalifa wa Waislamu. Na nilikuwa pamoja na ‘Aliy siku ile ‘Abdur-Rahmaan bin ‘Awf alipowashauri Waislamu juu ya nani awaongoze, nusu yao walimchagua ‘Uthmaan na nusu nyingine walimchagua ‘Aliy. Mimi siku ile nilikuwa pamoja na ‘Aliy.

Na nilikuwa pamoja na ‘Aliy pia siku ile alipokubali kuswali nyuma ya ‘Uthmaan baada ya kuchaguliwa Khalifa wa Waislamu, na maisha yangu yote nitakuwa pamoja na ‘Aliy mpaka siku ya Qiyaama. Lakini siwakufurishi Maswahaba wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) wala wake zake wala sikubali mtu yeyote awaseme vibaya watu wa nyumba ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam).

Mimi naamini kuwa Bibi Faatwimah alikwenda kweli kwa Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) akidai ardhi ya Fadak na baada ya kufahamishwa hadithi ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) kuwa Mitume hawarithiwi akaridhika, juu ya kukasirika kwake kidogo.

Na Abu Bakr (Radhiya Allaahu ‘anhu) alipomuendea nyumbani kumuomba radhi Faatwimah alikubali bila kinyongo. »

Mwisho wa maneno ya Al-Khuza’iy

 

Hadithi hii ya Mitume kutorithiwa ni sahihi na imo ndani ya vitabu vinavayotegemewa vya Shia na Sunni.

Imesimuliwa na Al-Kulayni katika kitabu chake maarufu ‘Al-Kaafi’ kuwa:

 

“Abu Abdillaah (Imam Ja’afar asw-Swaadiq) amesema:

“Na hakika Maulamaa ni warithi wa Mitume. Na hakika Mitume hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa” Al-Kaafi 1/42.

 

Imam Muhammad Al-Baaqir Al-Majlisi katika kitabu chake kiitwacho Mir'at al-‘Uquul 1/111 amesema kuwa hadithi hii ni sahihi.

 

Khomeini ameiandika hadithi hii katika kitabu chake kiitwacho ‘Al-Hukuumah al-Islaamiyah’ (Serikali ya Kiislamu), na akaitumia kama ni ushahidi wa Wilayat al-Faqiyh chini ya kichwa cha maneno; (Sahihat al-Qaddah) aliposema:

“Amesema ‘Aliy bin Ibraahim kutoka kwa baba yake, kutoka kwa Hammaad bin ‘Iysa kutoka kwa Abdullah bin Maymun al-Qaddah kuwa Abu Abdillah (Ja’afar asw-Swaadiq (‘Alayhis Salaam) amesema:

 

“Atakayefuata njia ya kutafuta elimu, basi Allaah Atamsahilishia njia ya Peponi. Na Maulamaa ni warithi wa Mitume. Na Mitume hawarithiwi Dinari wala Dirham, bali wao wanarithiwa elimu, kwa hivyo atakayeipata elimu hiyo amepata bahati kubwa.”

Al-Kaafi, kitab fadhl Al-‘Ilm, mlango wa Swiffat al-‘Ilm wa Fadhlihi, hadithi nambari 2

 

Na katika kitabu hicho hicho cha ‘Al-Hukuumah al-Islaamiyah’ ukurasa wa 133 Khomeini ameiandika hadithi nyingine iliyopokelewa kwa njia ya Muhammad Yahya kutoka kwa Ahmad bin Muhammad bin ‘Iysa kutoka kwa Muhammad bin Kahalid kutoka kwa Abu Abdillah (Imam Ja’afar asw-Swaadiq (‘Alayhis Salaam) kuwa amesema:

 

“Hakika Maulamaa ni warithi wa Mitume, na hii ni kwa sababu Mitume hawaachi Dirham wala Dinari kwa ajili ya kurithiwa, bali wao wanaacha maneno yao.” Al-Hukuumat al-Islaamiyah uk. 133

 

Kutokana na yaliyotangulia tunamaliza kwa kusema kuwa;

Si haki kutoikubali hadithi hii ya Kutorithiwa kwa Mitume katika kadhia ya Fadak, na kuikubali katika kadhia ya Wilayat al-Faqiyh, kama alivyoandika Khomeni na kabla yake Majlisi.

Kwa nini tuzikubali kauli za Mtume wa Allaah (Swalla Laahu alayhi wa sallam) pale tunapotaka na tuzikatae tusipotaka juu ya kujua kwetu kuwa kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Llahu alayhi wa sallam) haiwezi kubadilishwa na kiumbe chochote kile.

 

Na hadithi hii imo pia katika vitabu vifuatavyo :

Katika At-Tahdhiyb ameandika At-Tuwsi na katika Bihaar al-Anwaar ameandika Al-Majlisi:

 

“Nilimuuliza Abu Abdillah juu ya wanawake na haki zao katika urithi akasema:

“Wana haki zao katika thamani ya udongo na ujenzi na mbao na miti tu, ama ardhi na nyumba, wao hawana haki ya urithi (wowote ndani yake).”

 

Na kutoka kwa Muhammad bin Muslim kutoka kwa Abu Ja’afar (‘Alayhi Salaam) kuwa amesema:

 

“Wanawake hawana haki ya kurithi ardhi wala nyumba”.

 

Na kutoka kwa ‘Abdul-Malik bin Aayun kuwa mmoja wa ma-Imam alimwambia:

 

“Wanawake hawana haki ya urithi katika ardhi wala nyumba”.

 

 

Share