Zingatio: Tuwe Macho Kuhusu Ofa Za Maangamizi

 

Tuwe Macho Kuhusu Ofa Za Maangamizi

 

Naaswir Haamid

 

 Alhidaaya.com

 

 

Wakati Ibliys alipochukua ahadi kwamba atawapotosha wana Aadam, hakuwa na masikhara kwa kauli hii na aliazimia kwa kutekeleza hilo. Ndani ya karne hii inayoitwa ya sayansi na teknolojia, amerahisishiwa mambo kabisa katika kuwapotosha wana Aadam hadi unaweza kusema kwamba hakuna hata mmoja aliye nje ya wasajiliwa wa daftari la Ibliys!

 

 

Wala hakuna kipya ambacho kimerahisisha wana Aadam kupotea ulimwengu wa leo kama zilivyo simu. Tumeshaelezana mengi katika makala zilizopita, lakini kwa haya maovu yanayoendelea kufanywa yabidi tukumbushane tena kwa namna jamii ya Waislamu inavyozidi kupotoka. 'Asaa huwenda tukatanabahi ukweli wa upande wa pili wa shilingi.

 

 

Kwa kiwango kikubwa matumizi ya simu yamepenya kwa kila rika: vijana na wazee, wake kwa waume, wagonjwa na wazima, matajiri na masikini, wote takribani ni wenye kutumia huduma hii. Tunapozungumzia kuhusu simu, tusirudi zama za mababu na mabibi zetu tukadhani ni zile za kukamata kwa mikono miwili, mmoja ukiwa ukishika cha kuzungumzia na mwengine cha kusikilizia. Hakika tunazungumzia hizi simu za mkononi maarufu kwa jina la mobile.

 

 

Kumekuwa na ushindani mkubwa katika mashirika ya simu hadi kusikia ya kwamba kuna huduma zinazokaribiana kuwa bure. Wenyewe wanatangaza ya kwamba kutakuwa na ofa usiku kucha kuzungumza bure. Lakini kabla ya kwenda mbali, tujiulize: "Kweli hii ni bure?" Simu unaihudumia kwa kuigharamia, bila ya kuigharamia huwezi kutumia ofa hizo. Halkadhalika ofa nyingi ni lazima ujisajili japo kwa kiwango cha chini ili uweze kutumia ofa hizo. Hapo ndio tunaamini ule msemo wa kimombo – There is no free lunch. Unapoalikwa chakula cha mchana, basi hiyo kuitikia du’aa ndicho ulichoitiwa. Dunia hii haina bure kabisa.

 

 

Cha kusikitisha zaidi ni wale vijana wa jinsia tofauti wanapokaa wakizungumza ndani ya simu hizi usiku mzima! Sio hivyo tu, bali Waumini wakiwa kwenye visimamo vya usiku wao hata habari hawana. Tabia hii ilishtadi zaidi maeneo yetu katika mwezi mtukufu wa Ramadhwaan. Kweli hili lina kheri na sisi Waislamu?

 

 

Kama utafuatilia kwa makini mazungumzo hayo ya simu za bure, basi utakuta kwamba asilimia kubwa ni ya usengenyaji, uongo, uzushi, udaku na baya zaidi ndio mlango wa zinaa. Masaa matano Muislamu mzima kagandia simu, kinachofanywa hapo si chengine isipokuwa ni kuzikata dakika za uhai bure bure. Yareti angepitia Aayaat za Qur-aan na kuzijua maana yake ili kuzifanyia kazi angepata fadhila kubwa. Wenye akili tu ndio wanaelewa umuhimu wa kuchunga muda.

 

 

Hii tabia ya kujiingiza kichwa na miguu katika ofa inatudhihirishia kwamba wana Aadam wote wapo kwenye khasara. Isipokuwa tu kwa Waumini, ambao wanachunga muda wao katika kutenda mema kupitia simu hizo kwa kuusiana juu ya kushikamana na subira pamoja na katika kutenda haki. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema ndani ya Qur-aan:

 

 

بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ

 

وَالْعَصْرِ ﴿١إِنَّ الْإِنسَانَ لَفِي خُسْرٍ ﴿٢إِلَّا الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ وَتَوَاصَوْا بِالْحَقِّ وَتَوَاصَوْا بِالصَّبْرِ ﴿٣

Naapa kwa Al-‘Aswr (zama). Hakika mwana wa Aadam bila shaka yumo katika khasara. Isipokuwa wale walioamini na wakatenda mema na wakausiana haki na wakausiana subira. [Al-‘Aswr: 1-3]

 

 

Kama Muislamu ajijua ni dhaifu wa nafsi yake, basi ajizuilie kujiunga katika ofa hizo. Kwani itakuwa ndio sababu ya kuangamia kwake na jamii inayomzunguka.

 

 

Waislamu tuchunge muda wetu hapa duniani kwa kufuata yale yenye kuleta natija (matokeo) ya kheri na salama. Tuwe ni wenye kuchunguza na kuwa waangalifu kabla ya kufanya maamuzi ya kutumia huduma hizi. Haya mambo sio bure wala hayajaanzishwa kuzipatia nchi utajiri wa mali tu, bali lengo kuu ni kudumaza harakati za Waislamu makundi kwa makundi.

 

Tunamuomba Allaah Ar-Rahmaan, Ar-Rahiym Atujaalie tawfiyq ya kutenda mema, kuusiana haki na subira. Aamiyn!

 

 

 

Share