Zingatio: Subira Katika Kutomuasi Allaah

 

Zingatio: Subira Katika Kutomuasi Allaah

 

Naaswir Haamid

 

 Alhidaaya.com

 

 

Mwananchi yeyote anapokosa utiifu mbele ya wale wenye amri ataishia kwenye matatizo. Huenda akafunguliwa kesi na kuishia kifungoni bila ya kutarajia. Hali itakuwa kinyume kwa yule anayewatii viongozi.

 

Hiyo ndio hali anayotakiwa kuwa nayo Muislamu katika kuacha kumuasi Rabb Mlezi. Kwani athari za kumuasi Allaah ni kubwa na nzito na wala hazibebeki. Yatakikana kujisalimisha na kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika maisha yote anayoishi Muislamu hapa ulimwenguni.

 

Tendo la kutomuasi Rabb Mlezi sio jambo jepesi kama linavyozungumzwa. Kila kitu kina msingi wake na hakika subra ndio msingi wa kutomuasi Allaah(Subhaanahu wa Ta’aalaa). Kwani wengi wameshindwa kustahamili na kutumbukia au kurudia kwenye maovu yale yale. Wale Waislamu wenye marafiki wazinifu wamejikuta wakiwa baina ya toba na uasi. Ni mara nyingi wanarudia kwenye uasi kutokana na kukosa subra. Anaona hayaa kuitwa mshamba, ustadhi, mpumbavu na yanayofanana nayo.

 

Je, hatukumbuki na hatujifunzi kutoka Siyrah ya Bwana wa viumbe Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Kabla ya Utume aliitwa na kutambulika kuwa ni mkweli na mwaminifu. Hali ilibadilika ghafla alipotangaza Utume wake. Akaambiwa kwamba ni mchawi, muongo, mwenda wazimu, mwenye maradhi ya kifafa na mengi mengineyo. Nini alifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Je alirudi akaanza kumuasi Rabb Mlezi kutokana na kupewa majina yasiyofanana na khulqa yake? Hapana! Ndio iymaan yake ilipopamba moto na kuwa mgumu mithili ya chuma. Yote hayo yalitokana na subra aliyokuwa nayo katika kutomuasi Rabb Mlezi.

 

Na kwa hakika hata wenye kuwapatia mawaidha Waislamu wengine kingewashinda kibarua hicho kama wangelikosa subra. Kwani ni maneno mengi yanasemwa mbele ya uso wao na nyuma ya migongo yao. Huo ndio mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anaotakiwa kuwa nao kila Muislamu katika kuwa na subra. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kumwambia Nabiy (na Waislamu wote) kushikamana na subra: 

 

وَلَقَدْ كُذِّبَتْ رُسُلٌ مِّن قَبْلِكَ فَصَبَرُوا عَلَىٰ مَا كُذِّبُوا وَأُوذُوا حَتَّىٰ أَتَاهُمْ نَصْرُنَا ۚ

Na kwa yakini walikadhibishwa Rusuli kabla yako, wakasubiri juu ya yale waliyokadhibishwa; na wakaudhiwa hata ilipowafikia nusura Yetu. [Al-An'aam: 34]

 

Nusura inayozungumzwa ndani ya Aayah hiyo sio tu kuneemeshwa kwa fadhila za kifakhari hapa duniani. Bali yawezekana nusura isije kwa namna hiyo, ikaja wakati wa kukata roho au baada ya kuzikwa. Hiyo ndio subra inavyotakiwa, Muislamu anatakiwa kugandana nayo hadi imfikie yakini bila ya kuterereka.

 

Baadhi ya Waislamu wanarudi kwenye uasi kwa sababu wamejulikana ya kwamba walitenda dhambi kadha wa kadha. Ili kuridhisha jamii hujifanya kuwa wapo pamoja nao katika maasi aliyozoea kuyatenda. Kwa mfano alikuwa ni mwenye kuingia kumbi za miziki akaachana nazo, badala yake akashikamana na kuhudhuria darsa za Kiislamu. Pale tu anapotambulika kwamba huko nyuma alikuwa ni mwenye kuingia katika kumbi za disko, anajidai kuachana na darsa ili asijulikane kwamba ameachana na starehe hizo. Waislamu tufanye amali njema kwa ajili ya Muumba sio kwa binaadamu.

 

Tunakuomba Rabb wetu! Tumiminie subra, na Uzithibitishe nyoyo zetu katika kukutii na kuachana na maovu. Rabb wetu! Usitufanye mitihani kwa wale waliokufuru, na Tughufirie Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye nguvu, Mwenye hikmah. Amiyn!

 

 

 

Share