Rumayswaa: Ummu Sulaym Al-Answaariyah (رضي الله عنها) - Mama Wa Anas Bin Maalik

Rumayswaa Ummu Sulaym Al-Answaariyah (Mama Wa Anas Bin Maalik)

 

Kutoka Kitabu Cha: Sayyidaatu Mubashiraati bil-Jannah (Wanawake Waliobashiriwa Pepo)

 

Mwandishi: Muhammad Jabliyy

 

Mfasiri: Binti Ahmadah

 

www.alhidaaya.com

 

 

 

Alisema mtoto wangu: Na nani yule ambae aliyebashiriwa pepo vilevile ee baba? 

 

 

Nikasema: Hakika huyo ni Ummu Sulaym al-Answaariyah ee mwanangu. Baba yake ni Milhaani mtoto wa Khaalid mmoja kati ya Answaari katika kabila la Khazraji. Na mama yake anaitwa Malika mtoto wa Maalik.

 

Ama mumewe anaitwa Maalik mtoto wa Nadhar, na walikuwa na watoto wao kwa majina ya Anas na Baraa waliokuwa Swahaba zake Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Akasema: ee baba nihadithie kuhusiana na uislamu wa Ummu Sulaym na lipi lilikuwa jina lake? 

 

 

Nikasema: Alikuwa jina lake ni Rumayswaa au Ghumayswaa. Alisilimu baada ya ubalozi wa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uliposafiri kwenda Madiynah, ili kuwafundisha watu wake Uislamu, kuwapa utambuzi kuhusiana na Diyn na kuwasomesha juu yao Qur-aan. Kisha wakafungamana na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na wanawake wa ki-Answaar. Kuingia kwake katika Uislamu kulitimia pale mumewe (Maalik) aliposafiri katika biashara zake. Wakati aliporejea katika safari yake, alijua kuhusiana na Uislamu wa Ummu Sulaym akamshambulia.

 

Akasema mumewe: Umefanya ujinga (gani)?

 

Akarejesha juu yake kwa maneno yake: Hapana, lakini nimeamini.

 

Alikuwa akimchezesha kitoto Anas, akimtamkisha shahada mbili huku akimwambia aseme: Ee Anas sema: Ash-hadu ann laa ilaaha Illa Allaah.

 

Anas akawa anarejesha juu yake: Ash-hadu alaa ilaaha Illa Allaah.

 

Naye mama mtu akasema kumwambia Anas, sema: Ash-hadu anna Muhammadan Rasuwlu-Allaah.

 

Anas naye akaiga kwa kusema:

 

Ash-hadu anna Muhammadan Rasuwulu-Allaah.

 

Mpaka ikamkaa vizuri.

 

Wakati wote huo mumewe alikuwa akimsikia Ummu Sulaym akimsemeza mwanawe maneno hayo.

 

Mumewe akasema kumwambia Ummu Sulaym huku akimkodolea macho ya hasira: Usinifisidie mwanangu juu yangu.

 

Ummu Sulaym akarejesha kauli kwa maneno haya: Mimi simfisidii.

 

Uislamu ulikuwa ni sababu ya ugomvi ambao ulisimama baina yao. Hadi siku moja akaondoka Maalik katika safari zake huku akiwa mwenye kuuweka ugomvi ndani ya moyo. Yakamfikia mauti kwa kuuliwa.

 

Akapambazukiwa Ummu Sulaym akiwa kizuka, akaendelea kumlea Anas huku akiwa anasema: Sitomuachisha mpaka atakapoliwacha chuchu kwa nafsi yake, na wala sitoolewa mpaka atakaponiamrisha Anas.

 

Akaanza Anas kukua mkubwa na akaenda Ummu Sulaym kumpeleka Anas kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Akamuomba amuombee du'aa Anas. Wakati huo huo akimuomba Nabiy amfanye mwanawe kama ni mfanyakazi wake.

 

Akamkabili Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuombea du'aa Anas kwa Allaah Amzidishie mali na watoto. Na akapambazukiwa ni mmoja kati ya matajiri wa Madiynah wenye kuhisabiwa. Akapata Anas watoto na kumpatia mama yake wajukuu wengi. Hii ilikuwa baraka ya du'aa ya Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Akasema: kulikuwa na nini baadaye kwa Ummu Sulaym ee baba?

 

Nikasema: Alikuwa Ummu Sulaym ni mwanamke mwenye fadhila, na kwake yeye pia alikuwa na utimamu wa akili na sifa za fadhila kwa yale aliyojaaliwa. Alikuwa ni tegemeo la watu wengi, wanawake watukufu wa ki-Answaar na wanaume baada ya kufa mumewe.

 

Bwana Zayyid bin Sahli alitokea katika kabila la mafundi wa mbao (seremala), akipewa jina la kupanga la Abuu Talha. Alipotambua ya kwamba Ummu Sulaym amepambazukiwa na ujane (hana mume), alifanya haraka asitanguliwe na mmoja kati ya waposaji.

 

Kwa hakika Abuu Talha aliona hatokataliwa kwani alishtadi kwa mali nyingi anayeweza kutanguliza kutokana na manjano au nyeupe – dhahabu na fedha. Anachohitaji mtu kupitia kwa Abu Talha huweza kukipata kama vile anavyoomba. Akaja kwa Ummu Sulaym bila ya kufikiri katika akili yake na kumrejesha kutokana na udhaifu wake. Kwani Abuu Talha alikuwa ni mpambaji na mrembeaji mzuri mwenye kujua usanifu wa vitu.

 

Akakazania Abuu Talha jambo lake la kumposa Ummu Sulaym. Akatoka tena kuelekea kwenye nyumba ya Ummu Sulaym, akapiga hodi na kukaribishwa kupitia kwa mwanawe Ummu Sulaym (Anas). Akamruhusu kuingia wakati alipoweka wazi Abuu Talha nia ya ndoa yake.

 

Alisema Ummu Sulaym: Je unadhani mfano wa mtu kama wako anarejeshwa ee Abuu Talha? Lakini kwako kuna kitu kimoja kinanizuia nisiolewe na wewe. Na unadhani Abuu Talha ya kwamba amebakia juu yako mposaji wa mwisho na ameweka juu yako mahari makubwa ambayo hayatoweza kwa yeye kuyatoa au kuzidisha juu yako?

 

Akasema Abuu Talha: Ee Ummu Sulaym, hakika mimi ni mtu niliyemiliki mali nyingi, na nitajaalia kuwa swadaqah yako (yaani mahari yako) kutokana na dhahabu na fedha, na watashindwa wengine kutanguliza mfano wa mali hiyo.

 

Akatabasamu Ummu Sulaym, ya kwamba huwenda fikra za Abuu Talha zilimpeleka katika biashara, lakini ni kinyume na alivyofikiria Abuu Talha. Isipokuwa kilichokuwa kinamzuilia yeye kukubali jambo hili ni kinyume na mali ya Abuu Talha.

 

Alisema Abuu Talha: Una nini? Nitakupa lolote lililokuwa muhimu bila ya kujikalifisha kwa hayo kutokana na thamani yoyote.

 

Alisema Ummu Sulaym: Ee Abuu Talha, hakika wewe ni mtu mshirikina, na mimi ni mwanamke Muislamu, haisihi kuwa pamoja kwa mfano huo.

 

Kisha akaendelea kwa maneno yake: Je hutambui ee Abuu Talha unaye kwako unayemuabudia juu yake, na unafanya ibada kinyume na Allaah ambaye amekuumba?

 

Akasema Abuu Talha: Hapana.

 

Akasema Ummu Sulaym: Huoni vibaya ee Abuu Talha ya kwamba kigogo cha mti kimekuwa ndio ilaah (muabudiwa) wako? Na kinyume chake wanatengeneza juu yake unga au kufanyia kuni kwa kupikia chakula au kuwashia moto siku za baridi kali.

 

Hatimaye Abuu Talha yalimuingia kwenye moyo wake maneno ya Ummu Sulaym pamoja na ugumu wake na yanaelekea kwenye ukweli. Wala hayarejei kwenye njia ya haki.

 

Kisha akasema Abuu Talha: Na yepi mahari ambayo unayaridhia ee Ummu Sulaym?

 

Akasema: Ikiwa utasilimu nitakubali kuolewa na wewe kinyume na dhahabu wala fedha.

 

Akaelekea Abuu Talha kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kujitambulisha Uislamu baina ya mikono yake.

 

 

Ikatimia ndoa nzuri kabisa na wakasema wanawake wa ki-Answaar: Hatukutambua mahari makubwa kuliko mahari ya Abuu Talha kwa Ummu Sulaym. Kwa hakika mahari yake yalikuwa ni Uislamu.

 

Haki! Hakika ilikuwa neema katika ndoa hiyo. Maadamu imejengwa na msingi madhubuti. Na je lipo jambo lenye maslahi kuliko Uislamu kuwa msingi wa ndoa madhubuti na mtukufu?

 

Hakika Uislamu ni kisaidizi na ni fadhila za chemchem za mambo yote. Wala usidhani hakika Diyn hii ni ya haki kwa watoto wako tu, bali ni tukufu kwa wote kama ilivyochaguliwa. Na ipi ajabu kwa hayo? Kwa hakika Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

 الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا ۚ

Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na Nimekutimizieni neema Yangu, na Nimekuridhieni Uislamu uwe Dini yenu.   [Al-Maa’idah (5: 3)]

 

Akasema: je hunipi habari ya kitu kilicho kuwa bora kwa Ummu Sulaym ee baba?

 

Nikasema: Hapana ee mwanangu. Alikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haingii katika nyumba ya mmoja kati ya waliooana ila kwa Ummu Sulaym. Nabiy akaulizwa kuhusu jambo hilo. Akajibu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

((Hakika mimi namrehemu, ameuliwa ndugu yake pamoja nami.)) [Imepokewa na Muslim: 04, 2455]

 

Pia kutokana na masimulizi ya Anas kutoka kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Aliingia Jannah akazisikia sauti – Ni sauti ipi – akasema – Nani huyu? Pakasemwa kuambiwa yeye (Nabiy): Huyu ni Ghumayswaa binti Milhaan mama wa Anas bin Maalik.)) [Imepokewa na Muslim: 105, 2456]

 

Na Ummu Sulaym ameudiriki ubora, na baraka hizi zimemsibu pia Abuu Talha kupitia ndoa hii yenye baraka ya Bibi Ghumayswaa mama yake Anas (Radhwiya Allaahu ‘Anhum).

 

 

 

Akasema: je hunipi habari ee baba ya kwamba Ummu Sulaym alikuwa ni mwenye akili madhubuti ambazo zimemuandalia yeye wema na mahangaiko na mipangilio yake ya usanifu, na ipi dalili ambayo imekupelekea kumsifu kwa hayo ee baba?

 

 

Nikasema: Naapa kwa Allaah, hakika vile vile ilipambika akili yake Ummu Sulaym kwa hikmah katika kujaalia (khayr) mahangaiko yake na kuweka mbali aibu zake na upungufu wa kitu. Na hii mifano inatosheleza kwako kwa hikmah zake kwa yale yaliyomtokezea juu yake.

 

 

Akasema: Na alitumia vipi hikmah na uongozi wake kutengeneza mambo?

 

 

Nikasema: Abuu Talha alikuwa ana mtoto mdogo aliyempenda katika nafsi yake kuliko kitu chochote. Na alikuwa Ummu Sulaym akimlea na akimchunga. Siku moja alitoka Abuu Talha katika kutafuta rizki. Muda si mrefu mwanawe huyu alifariki bila ya Abuu Talha kuelewa hilo. Akausia Ummu Sulaym kwa watu wa nyumba yake kwamba asipewe habari Abuu Talhah kuhusiana na kifo cha mtoto wake.

 

Wakati alipomaliza Abuu Talha kazi yake, akaswali Swalaah ya 'Ishaa Msikitini, akaelekea nyumbani na kumkuta Ummu Sulaym hakika amemuandalia yeye chakula na amezidisha mapambo juu yake kuliko anavyojipamba.

 

Wakati alipomuuliza hali ya mtoto, akampa habari ya kwamba ni nzuri kuliko ilivyokuwa. Kisha Ummu Sulaym akatanguliza Swala ya 'Ishaa. Abuu Talha akala mpaka akashiba, ukasimama usingizi juu yao.

 

Wakati walipoamka alisema Ummu Sulaym kumwambia Abuu Talha kuhusiana na kitendo cha jirani yake juu yao: Ee Abuu Talha, jirani ameazima cha kuazima, wakati alipotakiwa yeye akirejeshe, alichukizwa na alijizuilia juu ya kurejesha. Je amefanya kosa kwa jambo hilo na anaweza kujitetea kwa kujizuilia?

 

Akastaajabu Abuu Talha: Hana udhuru kwa jambo hilo na ubaya ulioje kwa kujizuilia!

 

Akasema Ummu Sulaym: Kwa hakika ilikuwa kwa mtoto wako ni kiazimo cha kitu kutoka kwa Allaah na kukirejesha (ni haki), ikiwa utafanya (subra) basi kitarejea.

 

Akaendelea Ummu Sulaym kwa kusema: Hakika sisi sote tunamtegemea Allaah na kwake Yeye tutarejea.

 

 

Abuu Talha akaenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumsimulia kutokana na aliyoyafanya Ummu Sulaym.

 

 

Akasema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumwambia Abuu Talha: ((Akubarikieni Allaah usiku wenu))

 

Ikajibiwa du'aa hiyo na akabeba mimba Ummu Sulaym kisha akazaa kitoto cha kiume. Akamuamrisha mwanawe Anas kumbeba ndugu yake mdogo ili kwenda nae kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili amfungue koo na ampatie jina.

 

Akaelekea Anas na ndugu yake huku akiwa na tende. Alipowaona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wanakuja alisema kumwambia Anas: ((Je unayo pamoja nawe tende?)) Alisema Anas kumwambia Nabiy "ndio". Akaichukua tende huku akisoma du'aa na kuilainisha kwa kuitafuna tafuna. Kisha akakifungua kinywa cha mtoto na kumlisha baadhi ya tende hiyo. Akaanza kitoto kuramba ramba utamu tamu katika midomo yake miwili. Akasema Rasuli wa Allaah: ((Wamekanusha Answaar juu ya mapenzi ya tende)) Kisha akamwita jina la 'Abdullaah. Anas akamrejesha kwa mama yake.

 

 

Alisema mtoto: Niambie ukweli kuhusiana na jihaad ya kila mmoja baina ya watu wawili hawa, wana ndoa na maswahaba wazuri zaidi. na ni vipi ulikuwa ukarimu wao?

 

 

Nikasema: Kwa kila furaha ee mwanangu, walikuwa na mwenendo wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ukoo wa Abuu Talha uliokuwa na nguvu sana. Kwa hakika aliutumia vizuri Abuu Talha upanga katika kumlinda Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kama alivyoweka mali yake kwa ajili ya maandalizi ya vita na kutilia mkazo haja za Waislamu. Na alikuwa Abuu Talha ni mwenye kutaraji juu hayo kwa radhi za Rabb wake na Nabiy Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Kwa hakika alikuwa nayo bustani kubwa iliyojaa miti mizito mizito na aina tofauti za matunda. Siku moja alikuwa anaswali ndani ya bustani hiyo na alimuona ndege akiimba juu ya mti, alikuwa ana rangi tofauti. Akavutiwa juu ya kumuangalia kwa ukali wa uzuri wake, ikashughulika akili yake Abuu Talha mpaka hakuweza kukumbuka rakaa ngapi ameweza kuswali.

 

Wakati alipomaliza Swalaah yake alikimbilia kwa Nabiy wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), akamsimulia kwa kile kilichomtokea juu yake, na vipi aliweza kumshughulisha ndege mzuri ndani ya Swalaah yake.

 

Kisha akasema: Nishuhudie ee Rasuli wa Allaah, hakika mimi nimeijaalia bustani yangu hii ni swadaqah kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   na ifanye unavyotaka.

 

Hakika mfano wa kitu hichi kilichotolewa ni kizuri, hakipatikani kitendo hichi ila kwa yule mwenye mapenzi ya kweli kwa Rabb wake na Nabiy wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwa kuyakinisha kwamba mbele ya Allaah kuna khayr na ni yenye kubakia.

 

Ama kwa upande wa Jihaad, Abuu Talha hakika alifikia nafasi ya mbele katika vita vya Uhud. Hivi ni vita ambavyo walikwenda kinyume (kukhalifu) warembeaji wa mishale wa Kiislamu amri ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), wakaacha sehemu zao na kutaka kuokota na kunyang'anyiana ngawira ambazo zilienea kwenye uwanja wa mapambano. Kwa hakika ilikuwa hapana budi kubadilika muelekeo wa ushindi kwa maslahi ya washirikina badala ya kuwa ni kwa maslahi ya Waislamu. Wakakimbia Waislamu pale alipoeneza mmoja wa washirikina ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amekwisha uawa.

 

Na kilikuwa kichwa cha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kimepasuka, zimevunjwa taya zake na amejeruhiwa midomo yake. Ikaanza damu kumtiririka mtukufu, na alikuwa amezungukwa mbele yake na kikundi cha Maswahaba watukufu (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) kama vile bangili zinavyozunguka mkono. Sio hivyo tu, bali wamezitoa panga zao, wakamzunguka na kuvitoa vifua vyao bila ya kupita mmoja kati ya washirikina baina yao.

 

Naye hakuwa nyuma, kwani Abuu Talha alikuwa ni mmoja kati ya wale walioweka ngome kwa Nabiy siku hiyo. Akaanza Abuu Talha kuwarushia washirikina mishale isiyo na idadi.

 

Abuu Talha alimwambia maneno yafuatayo pale Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipotaka kujinyanyua kutoka sehemu aliyokaa, kwa ajili ya kuona wapi imeangukia mishale: Kwa baba yangu na mama yangu, ee Nabiy, usiwachungulie yakaja kukupata maudhi yao, nijaalie mimi kwa Allaah ni fidia yako.

 

Mara aliiingia kwao wao mmoja wa Waislamu akisema kwamba washirikina wanakimbia. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kumwambia: ((Rembea mshale wako baina ya mikono ya Abuu Talha na wala usipite (mshale) kutokana na wao ukakimbia))

 

Aliendelea Abuu Talha kurembea na kumlinda kutokana na hayo Rasuli wa Allaah mpaka akavunja mipinde mitatu. Na akauwa idadi kubwa ya maadui wa Allaah na maadui dhidi ya Diyn moja, ikafikia idadi yake watu ishirini (20).

 

Ikaja siku ya vita vya Hunayn, wakatoka wanandoa hao watukufu pamoja na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa ajili ya Jihaad dhidi ya washirikina. Na alikuwa Ummu Sulaym juu ya ngamia wa Abuu Talha, wakati alipomuona Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Ummu Sulaym alinadi: Kwa baba yangu na mama yangu ee Rasuli wa Allaah, nitawauwa hawa wote waliokimbia mlimani (Uhud), kwa ajili yako wewe kama walivyouawa wale ambao walitaka kukuuwa wewe. Rasuli wa Allaah akasema: ((Akutosheleze Allaah ee Ummu Sulaym))

 

Hakika Ummu Sulaym alikuwa ni jemedari aliye tayari kwa mapambano. Kwani katika vita hivyo vya Hunayn, Abuu Talha alimuona na kitu mikononi mwake, akamuuliza: Nini hichi ulicho nacho ee Ummu Sulaym.

 

Akasema Ummu Sulaym: Panga nimeichukua pamoja nami, atakaponikurubia mmoja kati ya washirikina nitalichoma tumbo lake.

 

Akasema Abuu Talha: Hivyo hukusikia yale aliyoyasema Rasuli wa Allaah?

 

Alisema Jubayr bin Mutwghama: Kwa hakika niliona kabla ya kushindwa kwa watu (yaani washirikina) huku watu wanapambana mfano wa mkusanyiko wa guo kubwa jeusi, limetanda kutoka mbinguni mpaka likaanguka baina yetu na baina ya watu. Nikaliangalia nikaona kana kwamba (hao wapiganaji) ni wadudu chungu weusi wametawanywa na wameenea katika jangwa. Basi nikawa nina shaka kwamba hao ni Malaika, na wala hawakuwa Malaika isipokuwa ni kushindwa kwa watu.

 

Amesema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

لَقَدْ نَصَرَكُمُ اللَّـهُ فِي مَوَاطِنَ كَثِيرَةٍ ۙ وَيَوْمَ حُنَيْنٍ ۙ إِذْ أَعْجَبَتْكُمْ كَثْرَتُكُمْ فَلَمْ تُغْنِ عَنكُمْ شَيْئًا وَضَاقَتْ عَلَيْكُمُ الْأَرْضُ بِمَا رَحُبَتْ ثُمَّ وَلَّيْتُم مُّدْبِرِينَ﴿٢٥﴾

25. Kwa yakini Amekunusuruni Allaah katika maeneo mengi, na Siku ya (vita vya) Hunayn (pia); ulipokupendezeni wingi wenu (kwa kujigamba), lakini haukukufaeni chochote; na ardhi ikawa dhiki juu yenu juu ya upana wake, kisha mkageuka na kurudi nyuma kukimbia.

 

 

ثُمَّ أَنزَلَ اللَّـهُ سَكِينَتَهُ عَلَىٰ رَسُولِهِ وَعَلَى الْمُؤْمِنِينَ وَأَنزَلَ جُنُودًا لَّمْ تَرَوْهَا وَعَذَّبَ الَّذِينَ كَفَرُوا ۚ وَذَٰلِكَ جَزَاءُ الْكَافِرِينَ﴿٢٦﴾

26. Kisha Allaah Akateremsha utulivu Wake kwa Rasuli Wake na kwa Waumini, na Akateremsha majeshi (ya Malaika) msiyoyaona; na Akawaadhibu wale waliokufuru. Na hivyo ndio jazaa ya makafiri.

 

ثُمَّ يَتُوبُ اللَّـهُ مِن بَعْدِ ذَٰلِكَ عَلَىٰ مَن يَشَاءُ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٢٧﴾

27. Kisha Allaah Anapokea tawbah baada ya hapo kwa Amtakaye. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.   [At-Tawbah: 25-27]

 

Vile vile alimkunjulia Allaah Rasuli Wake kwa (kumteremshia majeshi ya) Malaika na ushindi ukawa kwa Waislamu. Wakawashinda makafiri, shukurani zote ni za Allaah Rabb wa viumbe vyote.

 

 

Alisema mtoto: Ee baba nizidishie mimi masimulizi juu ya fadhila za Ummu Sulaym. 

 

 

Nikasema: Ummu Sulaym alihifadhi Hadiyth ambazo alizisikia kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Kisha akisimulia, na akawa amechukua juu yake idadi ya Hadiyth na baadhi ya Maswahaba wamesimulia kutoka kwake.

 

Jumla ya wapokezi waliosimulia kupitia kwake ni: mwanawe – Anas bin Maalik, 'AbduLlaah bin Abbaas, Ghamra bin Ghaaswim Answaari, Zubayr bin Thaabit, 'Abdur-Rahmaan bin 'Awf. Hizi ni fadhila za Allaah, Humpa Amtakae.

 

Amepokea Ghatwaa kutoka kwa Ummu Sulaym Al-Answaariy: Alisema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kumuuliza Ummu Sulaym: ((Kwa nini Ummu Sulaym hujaja kuhiji pamoja nasi mwaka huu?)) Akasema Ummu Sulaym: Ee Nabiy kulikuwa kwa mume wangu kuna watu wawili, ama mmoja amehiji juu yake, ama mwengine amemuacha akimwangalia juu yake mitende. Akasema: ((Pindi itakapokuwa Ramadhwaan au mwezi wa Swawm, fanya 'Umrah ndani yake, kwani hakika ya 'Umrah ni mfano wa Hijja, au huchukua nafasi ya Hijjah))

 

Akabaki Ummu Sulaym akikata masiku ya uhai wake baina ya funga na kisimamo na kupigana kwa ajili ya Allaah mpaka ikamfikia kikata ladha na kufarikiana na jamaa zake. Akalala katika ulinzi wa Allaah, ambao hakuna hata mmoja anaeweza kuwarehemu waja wake sawa sawa.

 

Akaishi Abuu Talha hadi kukutana na kipindi cha ukhalifa wa mwenye nuru mbili - 'Uthmaan bin 'Affaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Alimtaka Abuu Talha kutoka pamoja na jeshi la vita vya baharini aliloliandaa 'Uthmaan (Radhwiya Allaahu ‘Anhu). Abuu Talha aliweza kutanguliza kwa hilo upanga wake.

 

Wanawe wakamwambia: Tuache sisi tuende badala yako wewe, unahitaji kwa sasa mapumziko.

 

Walipokuwa katikati ya bahari yakamsibu maradhi Abuu Talha akafariki. Akawa miongoni mwa Maswahaba waliofariki ambao walitafutiwa sehemu ya kuzikwa miili yao kwa muda wa siku saba. Hatimaye wakakipata kisiwa. Na alikuwa amefunikwa kama vile amelala, na wala hakubadilika kitu chochote.

 

Amrehemu Allaah Abuu Talha na Ummu Sulaym na Awakutanishe wawili hao mbele Yake wakiwa ni wenye kung'ara na kufurahi.

 

 

Share