'Aaishah (رضي الله عنها): Historia Ya 'Aaishah Bint Abiy Bakr Asw-Swiddiyq

Imetayarishwa na Ummu Faraj

 

بسم الله الرحمن الرحيم

 

الحمد لله تعالى وحده والصلاة والسلام على من لا نبي بعده، نبينا محمد وعلى آله وصحبه ومن تبعهم بإحسان إلى يوم الدين.

أما بعد:

 

Kwa hakika Uislamu umemkirimu mwanamke takrima kubwa kabisa, awe mtoto wa kike, awe mke, awe mama, au awe dada.

 

Na Qur-aan imetaja baadhi ya wanawake,

mfano Mama yake Muusa (‘Alayhis Salaam), mke wa Fir’aun na Maryam bint ‘Imraan.

 

Na vile vile kuna miongoni mwa surah katika Qur-aan Kama vile Suratun Nisaa na At-Twalaaq zimezungumzia wanawake, vile vile kuna baadhi ya wanawake kama vile Bibi ‘Aaishah ( رضي الله عنها), Bibi Khawlah,  ziliteremshwa Aayah za Qur-aan kwa ajili yao.

 

Kadhaalika imehadithia Qur-aan kuwa walimjia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) Wanawake Waumini ambao walimpa bai’ah walohama toka Makkah kwenda Madiynah, kama ilivyobainishwa katika  Surat Al-Mumtahinah.

 

Kwa hakika hizi ni miongoni mwa fadhila kubwa kabisa Alizowafadhilisha nazo Allaah wanawake na kuna nyingi nyenginezo.

 

 

'AAISHAH BINT ABIY BAKR ASW-SWIDDIYQ (رضي الله عنها) ALIYETAKASWA KUTOKA JUU YA MBINGU YA SABA

 

Hakika yeye ni mwalimu wa wanaume ni mkweli na mtoto wa mkweli Al-Qurayshiyah At-Taymiyah Al-Makkiyah.

 

Mama wa Waumini na ni mke wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na  katika mke aliyekuwa akipendwa sana na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) vile vile ni mtoto wa Swahaba mtukufu aliyependwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Bibi ‘Aaishahرضي الله عنها) ) aliyewekwa mbali na kutakaswa na machafu kutoka mbingu ya saba.

 

ثبت في الصحيحين أن عمرو بن العاص رضي الله عنه - سأل النبي صلى الله عليه وسلم - أي الناس أحب إليك يارسول الله؟ قال: "عائشة"  قال: فمن الرجال؟ قال: "أبوها" (أخرجه البخاري)

 

Imethibiti kutoka kwa ‘Amru bin Al-‘Aasw alimuuliza Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) ni watu gani unaowapenda ee Mjumbe wa Allaah? Akasema, “'Aaishah” akasema na katika wanaume? akasema “Baba yake” [Imepokewa na Al-Bukhaariy].

 

'Aaishah bint Khaliyfatir RasuwliLLaahi Baba yake ni Abu Bakr 'Abdullaahi bin Abi Quhaafah, na Mama yake ni Mama Rummaan bint ‘Aamar Al-Kinaaniyah ambaye ni katika Swahabiyah mtukufu aliyesilimu katika kundi la mwanzo katika waliosilimu na aliolewa mwanzo na 'Abdulaah bin 'Abdil-Asad kabla ya kuolewa na Abuu Bakr. Na alizaa na mume wa mwanzo mtoto aitwaye Tufayl. Alihama kwenda Madiynah na alikufa baada ya Hadiythul Ifki katika uhai wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم), na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) aliteremka katika kaburi lake na akamtakia maghfirah.

 

 

KUOLEWA KWAKE ‘AAISHAH رضي الله عنها))

 

‘Aaishah (رضي الله عنها) aliolewa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kabla ya kuhama Makkah kwenda Madiynah katika mwezi wa Shawwaal baada ya kufa Bibi Khadiyjah ((رضي الله عنها nae alikua na umri wa miaka (6) sita, na akaingia dukhuli katika mji wa Madiynah akiwa na umri wa miaka (9) tisa akiwa bikra, na wala Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuoa mke bikra isipokua yeye.

 

'Aaishah ((رضي الله عنها amesimulia kwamba Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuoa nae akiwa na umri wa miaka sita (6) na kuitimiza ndoa yake kwa kitendo cha ndoa (dukhuli) akiwa na umri wa miaka tisa, (9) na baadae alibaki nae kwa miaka tisa. [Swahiyh Al-Bukhaariy].

 

 

ELIMU YAKE

 

Hakika yeye ni Swahabiyah mtukufu ambae amejifunza katika Madrassah tukufu ambayo alilelewa kutoka utoto wake nae ni Baba yake m’bora na alie mkweli Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه).

Na akakulia katika nyumba tukufa kabisa katika ujana wake nyumba ambayo ni madrasa ya Iymaani, mwalimu wake mtukufu na m’bora wa viumbe Mume wake kipenzi chake Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Hakika yeye ni muelewa sana mwenye akili mpaka ikasemwa ana robo ya hukmu tukufu alizobeba. Amepokea Ahaadiyth kutoka kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) elfu mbili mia mbili na kumi (2210).

 

Alikuwa mwalimu wa wanaume na ni marejeo kwao kutoka katika Hadiyth, Sunnah na Fiqh.

 

عن أبي موسى الأشعري رضي الله عنه قال:

ما أشكل علينا أصحاب رسول الله صلى الله عليه وسلم قط فسألنا عائشة رضي الله عنها إلا وجد نا عنها منه علما.

 

Kutoka kwa Abuu Muusa Al-Ash’ariy amesema:

“Hakukuwa na jambo lolote lililotutatiza sisi Maswahaba wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) katu isipokuwa tulimuuliza ‘Aaishah (رضي الله عنها) na kupata jawabu la kielimu kutoka kwake.”

 

وقال الإمام الزهري رحمه الله:

لو جمع علم عائشة إلى علم جميع علم النساء لكان علم عائشة أفضل.

 

Amesema Imaam Az-Zuhriy:

“Lau ingekusanywa elimu ya ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa elimu ya wanawake wote basi elimu ya ‘Aaishah ni bora”

 

عن مسروق قال:

فحلف بالله لقد رأينا الأكابر من أصحاب رسول الله صلى الله عليه وسلم يسألون عائشة عن الفرائض

 

Kutoka kwa Masruuq amesema:

“Naapa kwa Allaah nimewaona Maswahaba wakubwa wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wakimuuliza ‘Aaishah kuhusu masuala ya Mirathi.”

 

يقول ابن عبدالبر: إن عائشة كانت وحيدة وعصرها في ثلاثة علوم:علم الفقه،علم الطب،علم الشعر.

 

Amesema Ibn ‘Abdil-Barr:

“Hakika ‘Aaishah ni mwanamke pekee katika zama hizo ambae amekusanya elimu tatu;

(1) Elimu ya Shari’ah

(2) Elimu ya Matibabu

(3) Elimu ya Mashairi

 

 

SUBIRA YAKE

         

Kwa hakika ni mwanamke aliyebeba elimu nyingi na zenye manufaa na tunafaidika nazo hadi leo, na mwenye subira ni mfano wa kuigwa kwa Wanawake hakika ni Mwalimu kwa kila Mwanamke katika ulimwengu wa zama zetu hizi na ni mwalimu wa wanaume.

 

Kwa hakika alikuwa ni Mke bora na mkarimu wa nafsi na ni mwenye kutoa kwa ajili ya Mola wake amesubiri katika maisha yake pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya ufaqiri na njaa mpaka zimepita baadhi ya masiku hakuwashwi moto katika nyumba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم); walikuwa wakiishi kwa maji na tende.

 

Huu ni mfano mzuri sana wa kuigwa kwetu sisi wanawake twatakiwa tuwe na Subira ingawa ni jambo gumu lakini subira ndio itatuwezesha kufaulu katika maisha yetu ya Dunia ili tuweze kufikia ufaulu wa njia ya Akhera.

 

 

UKARIMU WAKE NA UZURI WA TABIA YAKE

 

يروى عن أم ذرة قالت: بعث ابن الزبير إلى عائشة رضي الله عنها بمال وهي يومئذ صائمة، فجلست تقسمه إلى بين الناس، وليس في بيتها شيء، فلما أمست قالت: ياجارية هاتي فطوري فجائتها بخبز وزيت وقالت لها أم ذرة أما استطعت مما قسمت اليوم أن تشتري لنا لحما بدرهم تفطر عليه؟ فقالت عائشة رضي الله عنها: لا تلومني لو كنت ذكرتني لفعلت.

 

Imepokewa kutoka kwa Ummu Dharrah amesema: “Alituma pesa Ibn Az-Zubayr kwa ‘Aaishah (رضي الله عنها) nae siku hiyo alikuwa amefunga Swawm, basi akakaa kuzigawa kwa watu pesa zote, Na ndani ya nyumba yake hamna kitu ilipofika jioni akasema ee Kijakazi lete futari, akaja na mkate na mafuta, Akasema Ummu Dharrah kumwambia hukuweza katika ulichogawa ukabakisha japo dirham tukanunua nyama ukafutaria na mkate? Akasema ‘Aaishah usinilaumu lau ungenikumbusha basi ningefanya hivyo”.

 

Huyu ndie Mama wa Waumini, ‘Aaishah bint Abiy Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنها)

         

Je, mimi na wewe tumefikia wapi katika kutoa fiy sabiyliLlaahi?

Basi huu ni mfano mzuri wa kuiga wa kutoa, kuwapendelea wenzetu kheri kabla ya nafsi zetu. Inahitaji Iymaan na Ikhlaasw ya hali ya juu, kwani unapotoa kwa ajili ya Mola wako ni akiba unajiwekea kesho Aakhera utaikuta in shaa Allaah.

 

 

MAMBO 9 ALIYOPEWA ‘AAISHAH (رضي الله عنها)

 

Anaeleza mwenyewe:

 

Kwa hakika nimepewa mambo (9) tisa hajapewa Mwanamke yeyote baada yangu:

 

1)      Ameteremka Jibriyl (عليه السلام) na sura (picha) yangu mpaka akaamrishwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) anioe.

2)      Amenioa nikiwa bikra wala hakuoa mke bikra isipokua mimi.

3)      Na mimi ni mtoto wa Khalifa na Mkweli.

4)      Na nimeteremshiwa utakaso kutoka mbinguni.

5)      Na amefariki Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na kichwa chake kiko juu ya mapaja yangu.

6)      Na kaburi lake Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) liko nyumbani kwangu.

7)      Na nimeahidiwa na Mola msamaha na rizki bora.

8)      Na nimeumbwa katika wema kutoka kwa mwema.

9)      Na ilikua wahyi ukishuka niko ndani ya shuka moja pamoja na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

 

TUKIO LA UZUSHI

 

Katika maisha yake Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) Mama wa Waumini lilimtokea tukio kubwa ambalo ni la kuzushwa (حادثة الإفك) ambalo wanafiki walilipokea kwa furaha na kuendeleza uzushi huu siku hadi siku wakawa wanalizungumzia na kulieneza kwa Waislamu na kuleta mpasuko baina yao.

 

Kwa hakika alikuwa huyu ‘Abdullaah bin Ubayy bin Saluul ndie aliyezalisha unafiki na hasadi katika moyo wake tokea mwanzo alipousikia Uislamu, na akawa anatamani limfike jambo baya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Uislamu kwa jumla, lakini Allaah (سبحانه وتعالى) kwa hikma kubwa na namna ya kuwadhihirisha wanafiki waliumbuka.

 

Kwa hakika uzushi huu ulimuuma sana Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) ndani ya moyo wake na maumivu haya yakapita ndani ya nyumba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na nyumba ya Abu Bakr As-Swiddiyq ((رضي الله عنه.

 

Ulikuwa wakati mgumu sana, ulichukua takriban mwezi mzima mpaka zikashuka aya za Qur-aan kumtakasa na uchafu huo Mwanamke mtukufu ‘Aaishah (رضي الله عنها) na pia kumtakasa Swahaba mtukufu Swafwaan bin Mu’utal (رضي الله عنه) ambae ndie aliesingiziwa kuwa pamoja na Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) katika dhambi hiyo. Mola Aliwatakasa.

Basi wanafiki wakafedheheka na ikawa ndio mwisho wa mazungumzo hayo.

 

 

TUKIO LENYEWE

 

Lilikua tukio hili ni katika vita vya Bani Al-Mustwaliq mwaka wa (5) tano wa Hijiriyah, na umri wa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) ulikuwa miaka (12) kumi na mbili.

Na hii ni Hadiyth anazungumzia mwenyewe Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) tukio lililomuumiza moyo wake anaelezea:

 

Alikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akitaka kusafiri anapiga kura baina ya wake zake, ikatokea mimi kusafiri nae pamoja katika msafara huo baada ya kuteremka Aayah ya Hijaab.

Na nilibebwa katika haudaj (haudaj ni kibanda chenye sitara ambacho anasitiriwa mwanamke na kinawekwa juu ya ngamia) tukaondoka na jeshi na ilikuwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wanaposafiri huwa wanapumzika njiani. Wakati tunarudi tukapumzika nami nikashikwa na haja nikatoka kwenye haudaj kwenda kukidhi haja nilipomaliza wakati narudi nikagundua kidani changu kimenipotea baada ya kukatika mkufu nikawa nimerudi kukitafuta, huku nyuma jeshi likaondoka wakabeba haudaj na kuweka juu ya ngamia wakidhani mimi nimo ndani na hawakuhisi kama mimi sipo kwani tulikuwa wanawake zamani ni wepesi sana nami nilikuwa mwembamba na tena nilikuwa mdogo, na tulikua tukila chakula ambacho si cha kunenepesha. Jeshi likaendelea na msafara huku wakidhania mimi nimo ndani ya haudaj.

 

Baada ya kukitafuta kidani nikakiona, ndio niliporudi sikulikuta jeshi limeshaondoka, nikenda ile sehemu ambayo nimeteremka nikaanza kulia na kukaa hapo kwa kudhani huwenda wakajua kama mimi sipo wakarudi kunifuata, nikawa nalia hadi usingizi ukanichukua.

Na alikua Swafwaan bin Mu’utal As-Saalimiy (رضي الله عنه) alibaki nyuma ya jeshi ili kuangalia kama kuna kilichosahauliwa au kudondoka katika jeshi.

 

Mara akaona kitu cheusi kwa mbali aliposogea akaona mtu amelala, kumuangalia akanijua baada ya kuniona, na alikua akinijua sura yangu kabla ya kushuka aya ya Hijaab, akasema:

 

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ

 

“Sisi sote ni wa Allaah na Kwake tutarejea”

 

Basi nikaamka baada ya kusikia hivyo kauli ikanishtua nikachukua Khimaar na kujifunika uso kwa Jilbaab, WaLlaahi hakuzungumza nami neno lolote wala sikumsikia kusema ispokuwa kauli ya istirja'a, akaniashiria kwa mnyama nami nikapanda nae akatembea mpaka tukalifikia jeshi katika mwendo wa mchana dhahir kabisa.

 

Hakika wakaangamia katika waloangamia baadhi ya Maswahaba katika jambo hili, na mkubwa kabisa wa wanafiki aloanza kueneza uzushi huu ni huyu ‘Abdullaah bin Ubayy bin Saluul.

 

Tukaingia Madiynah, ukapita takriban mwezi na watu wanaambizana jambo hili kutoka kwa wazushi wala mimi sina khabari kama kumezuka jambo.

 

Nami nilikuwa naumwa, Khabari hizi zinamfikia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) nami sijui kitu, lakini namuona Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akiingia ndani anatoa salaam na kusema vipi hali yako na kutoka hana uchangamfu kabisa, kwa jambo hilo akawa ana mashaka baina ya kuamini na kutokuamini.

 

Siku akaja mama yake Mistah tukatoka pamoja kwani nilikua na haja nikahitaji kutoka na tulikua hatutoki ila usiku usiku kabla hatujajenga choo karibu na nyumba, tulipokuwa njiani tunarudi mara Ummu Mistah akajikwaa na akasema aangamie Mistah, nae ni mtoto wake na pia huyu Ummu Mistah bint Ruhm bin ‘Abdu Manaaf, Mama yake ni Mtoto wa Sakhri bin ‘Aamir ni Khali yake Abu Bakr (رضي الله عنه).

Mistah ni mtoto wa Uthaathah bin Muttwalib.

 

Basi baada ya kusema neno hilo; Mama kusema juu ya Mtoto wake, nikasema kumwambia Ummu Mistah ni jambo baya umesema unamtukana mtu ambae ameshuhudia vita vya Badr? Akasema hivi hujui anayoyasema? nikasema Ni kitu gani? Nipe khabari, akanambia aliyonambia yakanizidi maradhi juu ya maradhi.

 

Niliporudi nyumbani akaingia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akanisalimia nikamuomba ruhusa ya kwenda nyumbani kwa wazazi, akanipa ruhusa, nami nilikuwa nataka yakini ya hizi khabari kutoka nyumbani ni kweli haya maneno yasemwayo?

 

Nikawauliza wazazi wangu kuhusu hii khabari, wakanambia ewe mtoto wetu tuliza nafsi yako, WaLlaahi ni mara chache kwa Mwanamke anayependeza zaidi kwa Mumewe naye anampenda illa watamzidishia.

 

Nikasema SubhaanaAllaah! kwa hakika hivi ndivyo wazungumzavyo watu? Nikaanza kulia usiku na mchana hayakuacha machozi kunitoka wala sijitii wanja wakati wa kulala hasha kwa kulia, nikaendelea na kilio changu.

 

Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akawa yuko baina wabaina kati ya kuamini na kutokuamini, akamuiita ‘Aliy bin Abiy Twaalib na Usaamah bin Zayd kutaka ushauri imma amuache au vipi, ama Usaamah akamshauri kua anajua kuwa familia yake imewekwa mbali na mabaya na anajua zaidi juu ya nafsi yake.

Akamwambia ee Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wa Allaah, mke wako yaani ‘Aaishah, sina ninachokijua kwake ila kheri.

 

Na ama ‘Aliy akasema kumwambia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) usijidhikishe na Allaah (سبحانه وتعالى) hajakudhikisha, wanawake wako wengi, na pia muulize mjakazi wake atakupa ukweli, Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akamwita na kumwambia Barirah je, umeona kitu chochote ambacho kinakutia mashaka juu ya jambo hili?

 

Akasema hapana naapa kwa yule aliekupa Utume kwa haki, mimi sina nijualo ila nafanya shughuli zangu na sijaona chochote wala sina mashaka juu ya hilo nadhania kheri.

 

Basi akasimama Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na akataka alipiziwe kisasi juu ya ‘Abdullaah bin Saluul, akasema hali ya kuwa yuko juu ya Mimbari.

 

"يا معشر المسلمين: من يعذ رني من رجل, قد بلغني أذاه في أهل بيتي, فوالله ما علمت على أهلي إلا خيرا, ولقد ذكروا رجلا ما علمت عليه إلا خيرا, وما كان يدخل على أهلي إلا معي"                     

Enyi kundi la Waislamu nani atanilipizia kisasi kwa mtu aliyeiudhi nyumba yangu na kuichafua? Naapa kwa Mola sina ninalojua juu ya nyumba yangu ispokuwa kheri, na ametajwa mtu sina ninalojua kwake isipokua kheri, na wala haingii kwa watu wangu ispokuwa pamoja nami.”

Hapa anamkusudia Swafwaan bin Mu’utal (رضي الله عنه).

 

Akasimama Sa’ad bin Mu’aadh (رضي الله عنه) akasema ee Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wa Mola, mimi nitalipiza ikiwa ni katika kabila la Awsi nitamkata kichwa na ikiwa ni katika ndugu zetu wa Khazraj niamrishe nitafanya utakaloniamrisha.

 

Akasimama Sa’ad bin ‘Ubaadah nae ni bwana wa Khazraj nae alikuwa kabla ya hapo ni mtu mwema lakini uzalendo ukamshika kwa watu wake.

Akasema, muongo! Hutaua wala huwezi kuua, akasimama Asyad bin Hudhiyr nae ni mtoto wa ‘Ammi yake Sa’ad bin Mu’aadh.

Akasema, muongo! Tutamuua, hakika wewe ni mnafiki, basi wakazozana mpaka wakanyamazishwa wakanyamaza.

 

Nikaendelea na kilio changu! Anasema Bibi Aa’ishah (رضي الله عنها) mpaka nikadhani ini langu litaharibika kwa kulia, akaja mwanamke mmoja akataka idhini nikampa akakaa kulia na mimi.

Mara akaingia Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akatusalimia kisha akakaa na hakukaa karibu yangu tangu yaliposemwa maneno haya, ilichukua mwezi mzima wala hakuna wahyi.

 

Akamhimidi Mola Aliyetukuka kisha akasema Amma ba’ad,

 

“Ee ‘Aaishah! kwa hakika limenifikia kutoka kwako jambo kadha wa kadha basi ikiwa uko mbali na haya yasemwayo basi Mola Atakutakasa, Na ikiwa umefanya jambo hilo mtake msamaha Mola wako na utubie kwake. Kwa hakika mja anapojua dhambi yake na akatubia basi Mola humsamehe”.

 

Basi alipomaliza kusema nikanyamaza kulia nikamwambia Baba yangu mjibu Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa aliyoyasema, akasema WaLlaahi sijui nimwambie nini Mjembe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)! Akamwambia Mama yake mjibu Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa aliyoyasema, akasema sijui nimjibu nini Mjumbe wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

Basi nikasema mimi ni mdogo na sijui  vizuri Qur-aan mpaka iwatulize katika nyoyo zenu na mkaniamini, ama nikisema mimi niko mbali na hayo hamtaniamini, na Allaah Anajua kuwa mimi niko mbali na hayo, naapa kwa Allaah sina ninachowaambia isipokua kauli ya baba yake Yuusuf:

 

فَصَبْرٌ جَمِيلٌ ۖ وَاللَّـهُ الْمُسْتَعَانُ عَلَىٰ مَا تَصِفُونَ

 

“Basi (langu mimi) ni subira njema; na Allaah ndie aombwae msaada kwa haya mnayoyasema.” [Yuusuf: 18]

 

 

Tanbihi:

“Ama kwa hakika mpaka hapa tumepata mafunzo mengi sana moja kubwa tumeona madhara makubwa ya uzushi mtu huna uhakika wa jambo basi wasikia tu na waanza kueneza, hiyo ni dhambi kubwa na pia kunasababisha mfarakano baina ya watu, ndugu zangu katika Iymaan tujitahidi kujiepusha na tabia hizi mbaya za kusikia majambo bila ya ushahidi na kuyaeneza.

Ni chukizo kubwa mbele ya Allaah (سبحا نه وتعالى).

Na Mola Anajua zaidi.

 

Anasema 'Aaishah (رضي الله عنها):

Basi baada ya kusema maneno hayo nikageuka na kulala kwenye tandiko langu. Na hali najua mimi niko mbali na hayo yasemwayo, Na hakika Mola wangu Ataniweka mbali na hayo In shaa Allaah .

 

Lakini WaLlaahi sikudhania kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Atateremsha Aayah za Qur-aan iwe ni shani kwangu na ziwe zinasomwa, bali nilitaraji kuwa Allaah (سبحانه وتعالى) Atamuotesha Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) Wake katika usingizi iwe utakaso kwa njia ya ndoto.

 

WaLlaahi hakusimama Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) wala hakutoka na yeyote katika watu wa nyumbani mpaka ulipoteremka wahyi. Kwa maana Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakuwa na raha.

 

Basi kwa furaha kubwa kabisa akaja Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na huku anacheka, akasema:

 

“Ee ‘Aaishah kwa hakika Mola wako Amekutakasa.”

 

Mama yangu akanambia inuka umuelekee Mume wako, nikasema WaLlaahi simuelekei wala simshukuru ispokuwa Mola wangu Aliyetukuka.

 

Na Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah hizi:

 

إِنَّ الَّذِينَ جَاءُوا بِالْإِفْكِ عُصْبَةٌ مِّنكُمْ ۚ لَا تَحْسَبُوهُ شَرًّا لَّكُم ۖ بَلْ هُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۚ لِكُلِّ امْرِئٍ مِّنْهُم مَّا اكْتَسَبَ مِنَ الْإِثْمِ ۚ وَالَّذِي تَوَلَّىٰ كِبْرَهُ مِنْهُمْ لَهُ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١١﴾

11. Hakika wale walioleta singizo la kashfa; (kumzulia ‘Aaishah  رضي الله عنها) ni kundi miongoni mwenu. Msiichukulie kuwa ni shari kwenu, bali ni kheri kwenu.  Kila mtu katika wao atapata yale aliyochuma katika dhambi. Na yule aliyejitwika sehemu yake kubwa miongoni mwao atapata adhabu kuu.

 

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾

12. Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao kheri, na wakasema: “Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?”

 

لَّوْلَا جَاءُوا عَلَيْهِ بِأَرْبَعَةِ شُهَدَاءَ ۚ فَإِذْ لَمْ يَأْتُوا بِالشُّهَدَاءِ فَأُولَـٰئِكَ عِندَ اللَّـهِ هُمُ الْكَاذِبُونَ ﴿١٣﴾

13. Kwa nini hawakuleta mashahidi wanne? Na kwa vile hawakuleta mashahidi, basi hao mbele ya Allaah ndio waongo.

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ لَمَسَّكُمْ فِي مَا أَفَضْتُمْ فِيهِ عَذَابٌ عَظِيمٌ ﴿١٤﴾

14. Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake duniani na Aakhirah, bila shaka ingekuguseni adhabu kuu kwa yale mliyojishughulisha nayo kuyaropoka,

 

إِذْ تَلَقَّوْنَهُ بِأَلْسِنَتِكُمْ وَتَقُولُونَ بِأَفْوَاهِكُم مَّا لَيْسَ لَكُم بِهِ عِلْمٌ وَتَحْسَبُونَهُ هَيِّنًا وَهُوَ عِندَ اللَّـهِ عَظِيمٌ ﴿١٥﴾

15. Mlipoipokea (kashfa ya uzushi) kwa ndimi zenu, na mkasema kwa midomo yenu, yale ambayo hamkuwa na elimu nayo; na mnalidhania ni jambo jepesi; na hali hili mbele ya Allaah ni kubwa mno.

 

وَلَوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ قُلْتُم مَّا يَكُونُ لَنَا أَن نَّتَكَلَّمَ بِهَـٰذَا سُبْحَانَكَ هَـٰذَا بُهْتَانٌ عَظِيمٌ ﴿١٦﴾

16. Na kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa) msiseme: “Haitupasi sisi tuzungumze haya; Subhaanak! Utakasifu ni Wako huu ni usingiziaji wa dhulma mkubwa mno!”

 

يَعِظُكُمُ اللَّـهُ أَن تَعُودُوا لِمِثْلِهِ أَبَدًا إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ ﴿١٧﴾

17. Allaah Anakuwaidhini msirudie abadani mfano wa haya, mkiwa ni Waumini wa kweli.

 

وَيُبَيِّنُ اللَّـهُ لَكُمُ الْآيَاتِ ۚ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ ﴿١٨﴾

18. Na Allaah Anakubainishieni Aayaat. Na Allaah Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.

 

 

إِنَّ الَّذِينَ يُحِبُّونَ أَن تَشِيعَ الْفَاحِشَةُ فِي الَّذِينَ آمَنُوا لَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۚ وَاللَّـهُ يَعْلَمُ وَأَنتُمْ لَا تَعْلَمُونَ ﴿١٩﴾

19. Hakika wale wanaopenda uenee uchafu wa kashfa kwa wale walioamini; watapata adhabu iumizayo duniani na Aakhirah. Na Allaah Anajua nanyi hamjui.

 

وَلَوْلَا فَضْلُ اللَّـهِ عَلَيْكُمْ وَرَحْمَتُهُ وَأَنَّ اللَّـهَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٠﴾

20. Na lau si fadhila ya Allaah juu yenu na rahmah Yake, na kwamba Allaah ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu.[Suratun-Nuwr: 11-20].

 

 

Aayah hizi zimemtakasa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) kutokana na yaliyozushwa na ndio maana yakaja makemeo na adhabu kali, kwa wenye kuzusha.

 

Na hili la kudhania ni baya pia kwani dhana mbaya nayo huzaa fitna kubwa, haiwi kumuona mtu amekaa na mwanamume au hata umewaona wanatoka chumbani pamoja ukajenga dhana kuwa wamezini ingawa ni kosa kwa mtu ambae si Mahrimu yake kukaa chumbani na kujifungia, lakini basi isiwe sababu ya kuwatuhumu kuwa wamezini hali huna ushahidi je, kama walikuwa wanaongea tu hawajafanya kitendo chochote utakuwa umebeba dhambi kubwa ya uzushi na ndio maana Allaah (سبحانه وتعالى) Akataka mwenye kusema fulani amezini alete mashahidi (4) wa nne kama hana apigwe bakora (80) themanini.

 

Na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) akasema ushahidi wa zinaa ni wa watu wa nne (4) washuhudie kama vile kamba inavyoingia kisimani.

 

 

Na ndio Allaah (سبحانه وتعالى) Akasema:

 

لَّوْلَا إِذْ سَمِعْتُمُوهُ ظَنَّ الْمُؤْمِنُونَ وَالْمُؤْمِنَاتُ بِأَنفُسِهِمْ خَيْرًا وَقَالُوا هَـٰذَا إِفْكٌ مُّبِينٌ ﴿١٢﴾

12. Kwa nini mlipoisikia (kashfa ya kusingiziwa), Waumini wanaume na Waumini wanawake wasiwadhanie wenzao kheri, na wakasema: “Hii ni kashfa ya kusingizwa iliyo dhahiri?” [Suratun-Nuwr: 12].

 

Amesema tena Allaah (سبحانه وتعالي):

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ

 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اجْتَنِبُوا كَثِيرًا مِّنَ الظَّنِّ إِنَّ بَعْضَ الظَّنِّ إِثْمٌ ۖ وَلَا تَجَسَّسُوا وَلَا يَغْتَب بَّعْضُكُم بَعْضًا ۚ أَيُحِبُّ أَحَدُكُمْ أَن يَأْكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوهُ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ تَوَّابٌ رَّحِيمٌ ﴿١٢﴾

"Enyi walioamini!  Jieupusheni sana na dhana kwani hakika baadhi ya dhana ni dhambi. [Al-Hujuraat: 12]

 

 

Tanbihi:

Kwa utakaso huu alotakaswa na Mola Mtukufu bado kuna makundi yanayojinasibisha na Uislamu wanamtukana mama wa Waumini tena hadharani pamoja na Maswahaba watukufu wa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na tujihadhari na makundi hayo tusije tukaangamia kama waloangamia.

 

Basi pindi ilipoteremka Qur-aan kumtakasa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها), Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه) nae alikuwa akimpa chakula na mahitaji mengine akimsaidia huyu Mistah, akasema WAllaahi simpi tena chochote huyu Mistah baada ya haya aliyoyasema kwa ‘Aaishah, ndipo Allaah (سبحانه وتعالى) Akateremsha Aayah isemayo:

 

وَلَا يَأْتَلِ أُولُو الْفَضْلِ مِنكُمْ وَالسَّعَةِ أَن يُؤْتُوا أُولِي الْقُرْبَىٰ وَالْمَسَاكِينَ وَالْمُهَاجِرِينَ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ ۖ وَلْيَعْفُوا وَلْيَصْفَحُوا ۗ أَلَا تُحِبُّونَ أَن يَغْفِرَ اللَّـهُ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ ﴿٢٢﴾

"Na wala wasiape wale wenye fadhila miongoni mwenu na wenye wasaa wa mali kuwa hawatowapa (swadaqah) jamaa wa karibu, na masikini, na Muhaajiriyn katika njia ya Allaah. Na wasamehe na waachilie mbali. Je, hampendi Allaah Akughufurieni? Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.[Suratun-Nuwr: 22].

 

Basi baada ya Aayah hii akasema Abu Bakr (رضي الله عنه) hapana Mola wangu napenda nami kusamehewe akarejesha yale yote aliyokua akimfanyia Mistah kama mwanzo na akasema sitamsumbua tena abadan.

 

Na hili ni fundisho kwetu sote la kusameheana usiweke kitu moyoni na vifundo na kuweka ahadi kama mtu kakukosea ukasema simfanyii kadha wala simsamahe mpaka Qiyaamah. Uislamu umetufunza kusameheyana kwani ukimsamehe ndugu yako Muislamu, Mola nawe Atakusamehe. Hakuna binadamu aliyekamilika. Alkamaaulu LilLlaahi.

 

Lau Allaah hakutuwekea msamaha na Rahma Zake kwa waja Wake basi hakuna mtu hata mmoja angenusurika na adhabu Zake.

Tunamuomba Mola Atumiminie Rahma Zake na Msamaha Wake Hakika Yeye ni mwingi wa kusamehe na mwingi wa kurehemu.

 

 

Amesema ‘Aaishah (رضي الله عنها), Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alimuuliza Zaynab bint Jahsh kuhusu jambo hilo. Akasema Zaynab (رضي الله عنها), najikinga na macho yangu na masikio yangu sina ninachokijua kwa ‘Aaishah Isipokuwa kheri.

Hapa ni kuonyesha hakuna haki katika haki isipokua kusema ukweli. Japo Zaynab ni mke mwenza lakini kasema ukweli wa jambo, na haya ni mafunzo tunayojifunza kwa watu wema ya kusema ukweli.

 

Ikarudi furaha katika nyumba ya Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa Fadhila za Mola ('Azza wa Jalla).

 

 

KUFA KWAKE

 

Amekufa ‘Aaishah (رضي الله عنها) usiku wa Jumanne, tarehe kumi na saba (17) Ramadhaan mwaka wa khamsini na nane (58) wa Hijrah nae akiwa na umri wa mika sitini na sita (66), akazikwa katika makaburi ya Baqii usiku baada Swalah ya witri.

 

Mola Amuwie Radhi mkweli mtoto wa mkweli na Mola Mtukufu Amteremshe katika pepo tukufu milele. Aamiyn

 

Nasi Twamuomba Mola wetu mtukufu kwa kisa hiki cha Mama yetu ‘Aaishah (رضي الله عنها) tupate mazingatio na tuige mafundisho kwani ni mengi sana tumeyapata kutoka kwake Mama wa Waumini, tujitahidi kusoma na kutafuta yalo na faida na sisi katika maisha yetu

 

 

FAIDA TULIZOPATA KATIKA HISTORIA YA BIBI ‘AAISHAH (رضي الله عنها)

 

· Ubora wa Bibi ‘Aaishah kwa Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) juu ya wanawake wengine. Alikuwa akipendwa na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kuliko mwanamke mwengine yeyote. Kama alivyokuwa baba yake akipendwa zaidi na Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) kuliko wanaume wengine.

 

· Kumuozesha mtu bint yake kwa rafiki yake maadam ni mtu mwema, Kama alivyomuozesha Abu Bakr bint yake ‘Aaishah (رضي الله عنها) kwa Mtume wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).

 

· Hakuna ubaya mtu kumpenda mke mmoja zaidi ya wengine maadam atawafanyia wote uadilifu. Kama ambavyo Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akimpenda zaidi ‘Aaishah (رضي الله عنها) kuliko wake zake wengine lakini hakuacha kuwafanyia wote uadilifu bila kumpendelea fulani au kumbagua fulani.

 

· Subira juu ya mitihani. Tumeona namna Bibi ‘Aaishah alivyokuwa na subira kubwa baada ya tukio la kuzuliwa uchafu. Na subira pia kwa kuchelewa sana kushuka kwa Wahyi kwa mwezi mzima.

 

· Kutoharakisha kutoa hukumu ya jambo. Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) hakufanya pupa au haraka ya kutoa hukumu.

 

· Kujichunga na kumzulia Muislamu mwenzako. Na kujizuia na kutuhumu watu.

 

· Hukumu kwa wanaotukana wake za Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba kwa ujumla. Wamekubaliana Ma’ulamaa kuwa anayemsingizia Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) uzinifu, basi atakuwa amekufuru kwani Allaah Mwenyewe kamtakasa kwenye Qur-aan na hukumu imetoka mbinguni kuthibitisha usafi na utwahara wake. Hivyo anayemtuhumu anakuwa ameikadhibisha Qur-aan na vilevile kamtukana Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) pia.

 

· Kuwepo wanawake wenye elimu zaidi ya wanaume katika masaail ya Dini. Kama alivyokuwa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) na elimu kubwa ya Fiqh, Miyraath, Tafsiyr, Hadiyth n.k hata kuwafanya Maswahaba wengi kumwendea na kuchukua elimu na hukumu ya masaail ya kishari’ah.

 

· Allaah kumtakasa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) kutoka juu ya mbingu ya saba.

 

· Mtu kutaka ushauri kwa rafiki zake wema kuhusiana na suala la kutengena na mke wake.

 

· Kuwapendea wengine kheri kuliko nafsi yako. Tunaona katika upande wa kutoa Bibi ‘Aaishah (رضي الله عنها) alikua akiwafikiria wenzie kabla ya nafsi yake.

 

· Na katika upande wa elimu amebeba elimu kubwa kutoka kwa bwana Mtume (صلى الله عليه وآله وسلم) nasi hatuna budi kufanya juhudi katika kuitafuta elimu yenye manufaa na kuifanyia kazi.

 

· Kadhalika Suala la Niqaab (kufunika uso) tumepata dalili kutoka kwake pale aliposema Swafwaan alimjua kabla ya Hijaab.

 

Mola Atuwafiqishe Mema Tuyafate na Mabaya Tuyaepuke. Atusamehe pale tulipokosea na Asitunyime ujira pale tulipopatia.

 

 

Share