Abuu Ayyuwb Al-Answaariy (رضي الله عنه)

Abuu Ayyuwb Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu 'anhu)

 

Muhammad Faraj Saalim As-Sa'y (Rahimahu-Allaah)

 

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Masjid Qubaa

 

 

Jina lake ni Khaalid bin Zayd bin Kulayb, na umaarufu wake ni Abuu Ayyuwb Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyeanza kuwa maarufu siku ile Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipohajir kutoka Makkah kwenda Madiynah na kufikia katika nyumba yake.

 

Kabla ya kuingia Madiynah Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliwasili Qubaa mji uliopo nje kidogo ya Madiynah na kukaa hapo muda wa siku nne, na katika siku hizo aliujenga Msikiti wa mwanzo 'uliojengwa kwa taqwa ya Allaah'.

 

Allaah Anasema:

 

لَا تَقُمْ فِيهِ أَبَدًا ۚ لَّمَسْجِدٌ أُسِّسَ عَلَى التَّقْوَىٰ مِنْ أَوَّلِ يَوْمٍ أَحَقُّ أَن تَقُومَ فِيهِ ۚ فِيهِ رِجَالٌ يُحِبُّونَ أَن يَتَطَهَّرُوا ۚ وَاللَّـهُ يُحِبُّ الْمُطَّهِّرِينَ﴿١٠٨﴾

"Usisimame humo abadani.  Bila shaka Msikiti ulioasisiwa juu ya taqwa tokea siku ya kwanza unastahiki zaidi usimame humo..." [At-Tawbah: 108]

 

Msikiti uliokusudiwa katika aya hii ni Masjid Qubaa ambao zimepokelewa Hadiyth nyingi Swahiyh katika Al-Bukhaariy na Muslim na wengine kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiuendea msikiti huo kila Jumamosi akiwa amepanda mnyama na mara nyingine kwa miguu na kuswali rakaa mbili. Na imepokelewa pia kuwa thawabu za kuswali rakaa mbili katika msikiti wa Qubaa ni sawa na thawabu za ‘Umrah.

 

Baada ya kukamilisha ujenzi wa Msikiti Qubaa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliondoka akiwa amepanda ngamia wake na kuingia mjini Madiynah huku watu wa mji huo wakimfungulia milango ya nyumba zao na kumkaribisha, kila mmoja akitaka afikie kwake.

 

Watu mbali mbali wakiwemo viongozi wa makabila makubwa ya hapo walikuwa wakimfuata na kujaribu kumsimamisha ngamia wa Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku wakimuambia: “Fikia kwetu ee Rasuli wa Allaah, sisi tunao uwezo na nguvu za kukulinda.”   Lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akiwaambia: “Muacheni, (ngamia) huyu anaongozwa."

 

 

Mbele Ya Nyumba Ya Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Ngamia akaendelea kwenda, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwa juu yake na macho ya watu yakimfuata huku nyoyo zao zikidunda. Kila ngamia anapopita karibu na nyumba, mwenye nyumba hiyo hufurahi akidhani kuwa bahati itamuangukia yeye na ngamia atasimama nyumbani kwake na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) atafikia kwake. Lakini ngamia alikuwa akiendelea na safari yake, na kila anapoipita nyumba mwenye nyumba ile huhuzuika huku furaha ikiingia nyoyoni mwa wenye nyumba za mbele, kila mmoja akiwa na tamaa kuwa ngamia atasimama mbele ya nyumba yake.

 

 

Akaendelea katika hali hiyo huku watu wakimfuata mpaka alipofika penye uwanja mbele ya nyumba ya Abuu Ayyuwb Al-Answaariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na hapo ndipo ngamia alipopiga magoti. Furaha isiyoweza kuelezeka iliinga moyoni mwa Swahaba huyu mtukufu kwa kufikiwa na bahati hiyo. Lakini furaha haikudumu, maana baada ya muda mfupi ngamia yule akainuka na kuanza kutembea tena, lakini safari hii alikwenda masafa madogo huku Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiiregeza kamba yake, na baada ya kutembea hatua chache ngamia akarudi tena na kupiga magoti pale pale alipopiga mwanzo mbele ya nyumba ya Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu).

 

 

Na Kwa Nini Asifurahi?

 

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alimkimbilia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumkaribisha nyumbani kwake huku akimbebea mizigo yake kwa tahadhari na unyenyekevu na furaha kubwa kama kwamba amebeba hazina za ulimwengu mzima.

 

Na kwa nini asifurahi wakati nyumba yake ndiyo iliyobahatika kufikiwa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ataishi hapo na kuifanya kazi kubwa ya kuufikisha ujumbe, kuieneza elimu, imani na kuingiza roho katika mwili wa ulimwengu usiokuwa na uhai. Atakuwa hapo mpaka pale atakapoweza kujenga nyumba yake mwenyewe.

 

Kwa nini asifurahi wakati juu ya ardhi hiyo utajengwa Msikiti ambao ndani yake watu watafundishwa Dini yao na ndani yake Msikiti huo zitatoka sauti za Allaahu Akbar na kuenea ulimwengu mzima. Zitaendelea hivyo mpaka siku ambayo Allaah Atairithi ardhi na kila kilichokuwemo juu yake – Siku ya Qiyaamah.

 

 

Haikuwa Mara Ya Mwanzo

 

Haikuwa mara ya mwanzo kwake kuonana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), kwani katika mwaka wa 13 Hijriyah, Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa miongoni mwa Waislamu 75 waliokuja Makkah kutoka Madiynah kwa siri kwa ajili ya kufungamana na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika fungamano lililokuja kujulikana kwa jina la Fungamano la ‘Aqabah la pili.

 

 

Siku hiyo Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) pamoja na wenzake kila mmoja aliingiza mkono wake wa kulia ndani ya mkono wa kulia wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) huku wakitoa ahadi ya kumlinda atakapokwenda Madiynah, na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwaahidi Pepo.

 

 

Nyumba Yake

 

Nyumba yake ilikuwa ya juu na chini, na Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akaanza kuviteremsha vitu vyake chini ili mgeni wake mtukufu afikie juu, lakini Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikataa na kumtaka mwenyewe akae juu.

 

 

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alifanya kama alivyoambiwa, lakini usiku ulipoingia na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipokwenda kulala, na yeye kupanda juu na kufunga mlango wake akamwambia mkewe: “Ole wetu! Tumefanya nini sisi? Inawezekana kweli Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) awe chini yetu na sisi tuwe juu yake? Haiwezekani sisi tuwe tunatembea juu ya Rasuli wa Allaah tukiwa baina yake na baina ya Wahyi unaomteremkia? Hakika sisi tutaangamia.”

 

 

Hawakuweza kulala usiku ule wala hawakuwa na raha, na wakati huo huo hawakujua la kufanya mpaka walipoamua kutandika sehemu ya pembeni isiyokuwa juu ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Wakawa wanatembea sehemu za pembeni tu ya nyumba yao wakihofia wasije wakatembea sehemu iliyo juu yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

 

Asubuhi ilipoingia Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikwenda moja kwa moja kwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuambia:

 

"Wa-Allaahi hatukuweza kulala usiku wa leo, mimi wala mke wangu."

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: "Kwa nini?"

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema: "Kila nikikumbuka kuwa mimi nipo juu ya nyumba ambayo chini yake upo wewe, na kwamba kila ninapotembea ninakupukutishia vumbi, kisha mimi nipo katikati baina yako na baina ya Wahyi unaoteremshiwa."

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia: "Usiishughulishe nafsi yako kiasi hicho ee Abuu Ayyuwb. Kwetu sisi bora tuwe chini kwa sababu ya wageni wengi wanaokuja kututembelea."

 

 

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikubali, lakini siku moja katika usiku wa baridi kali gudulia la maji lilimuanguka na kumwagika. Anasema Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu):

 

"Tukaanza mimi na Ummu Ayyuwb (mkewe) kupangusa kwa kitambaa, na hicho ndicho kilichokuwa kitambaa chetu tulichokuwa tukijifunikia kwa ajili ya kujikinga na baridi kali, na hatukuwa na kitambaa kingine isipokuwa hicho. Tukawa tunapangusa maji tukihofia yasije yakafika chini alipo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Asubuhi ilipoingia nikamuendea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumuambia: "Kusema kweli mimi sipendi wewe uwe chini yangu na mimi niwe juu yako." Kisha nikamuhadithia yaliyotokea usiku, akanikubalia na kuhamia juu, na mimi na mke wangu tukakaa chini."

 

 

Yuwapi Abuu Ayyuwb

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikaa katika nyumba ya Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) muda wa miezi saba, na wakati wote huo Msikiti ulikuwa ukijengwa mbele ya nyumba ya Abuu Ayyuwb mahali alipopiga magoti ngamia. Msikiti uipomalizika, Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akahamia katika mojawapo ya vyumba vilivyojengwa ndani ya Msikiti huo.

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alikuwa akimpenda na kumuheshimu sana Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu), na kila anapoiangalia nyumba aliyofikia alikuwa akihisi kama kwamba anaiangalia nyumba yake.

 

 

Imesimuliwa na Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Abu Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alitoka siku moja akielekea Msikitini wakati wa mchana, na jua siku hiyo lilikuwa kali sana. ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipomuona akamuuliza:

“Ee Abu Bakr jambo gani lililokutoa wakati huu?" Akasema: "Hapana kilichonitoa isipokuwa njaa kali." ‘Umar akasema: "Na mimi Wa-Allaahi  nimetoka kwa sababu hiyo hiyo."

Walipokuwa katika hali ile akatokea Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwauliza: "Jambo gani lililokutoeni wakati huu?" Wakasema: "Wa-Allaahi hapana kilichotutoa isipokuwa njaa inayoumiza matumbo yetu." Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: "Na mimi naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake hapana kilichonitoa isipokuwa hicho. Nifuateni.” Wakaondoka pamoja kuelekea nyumba ya Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu), ambaye kila siku alikuwa akitenga chakula kwa ajili ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na asipokuja alikuwa akiwapa watu wa nyumba yake.

Walipowasili mlangoni walifunguliwa na mke wa Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyewakaribisha kwa kusema: "Karibu ee Rasuli wa Allaah pamoja na waliofuatana naye."

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Yuwapi Abuu Ayyuwb?"

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliyekuwa wakati ule akiishughulikia mtende yake iliyo karibu na mahali hapo aliisikia sauti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akaharakisha kumuendea huku akisema: "Karibu ee Rasuli wa Allaah pamoja na waliofuatana naye.  Ee Rasuli wa Allaah si kawaida yako kuja wakati huu."

Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Umesema kweli."

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akarudi penye mitende yake na kuchuma tawi lililojaa tende za kila aina. Tende mbichi, zilizoiva nusu nusu na nyengine zilizoiva vizuri.

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuambia:

"Sikutaka ulikate tawi hili. Si bora ungetuletea katika tende zilizokwisha chumwa tokea zamani?"

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

"Ee Rasuli wa Allaah, nilipenda ule katika tende hizi mpya zimo ndani yake kila aina, zilizoiva kidogo na zilizoiva vizuri na nitachinja pia kwa ajili yako.

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Kama utachinja usichinje aliye na maziwa."

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akachagua mbuzi aliyenona na kumchinja kisha akamuambia mkewe:

"Kanda unga utufanyie mikate na wewe ni mjuzi zaidi wa mikate. Kisha akachukua nusu ya mbuzi akaipika na nusu ya pili akaichoma. Chakula kilipoiva akakiweka mbele ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) pamoja na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu ‘anhum), na Rasuli (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akakata kipande cha nyama akakitia ndani ya mkate kisha akakiingiza mikononi mwa Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) na kumuambia:

"Ee Abuu Ayyuwb mpelekee haraka Faatwimah maana siku nyingi hajapata kuonja chakula kama hiki."

 

Baada ya kumaliza kula Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:

"Mkate na nyama na tende zilizoiva kidogo na zilizoiva vizuri." Baada ya kusema maneno hayo akatokwa na machozi. Kisha akasema: "Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu imo mikononi mwake kuwa hii ndiyo neema mtakayoulizwa juu yake siku ya Qiyaamah. Mtakapopata mfano wa hiki kabla ya kula pigeni

بِسْمِ الله

BismiLlaah, na mkishashiba semeni:

 

الحمد لله الذي هو أشبعنا فأنعم علينا فأفضل

Namshukuru Allaah Aliyetushibisha Akatuneemesha na Akatuongeza katika fadhila Zake.

 

 

 

Jihadi Yake Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘Anhu)

 

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) aliishi akiwa mpiganaji jihadi katika njia ya Allaah, na alishiriki karibu vita vyote walivyopigana Waislamu tokea wakati wa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mpaka wakati wa ukhalifa wa Mu’aawiyah bin Abi Sufyaan (Radhwiya Allaahu ‘anhuma).

 

Vita vya mwisho alivyoshiriki vilikuwa vya Costantinople (Uturuki) wakati Mu’aawiyah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipotayarisha jeshi kubwa chini ya uongozi wa mwanawe Yaziyd kwa ajili ya kuifungua nchi hiyo iliyokuwa ikitawaliwa na Warumi. Wakati huo Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alikuwa mzee mwenye umri wa miaka themanini.

 

 

Umri huo haukumzuwia kushiriki katika vita hivyo na kuivuka bahari yenye mawimbi makali kwa ajili ya kupigana jihadi katika njia ya Allaah. Lakini haukupita muda mrefu tokea vita hivyo kuanza Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alipata maradhi yaliyomzuwia asiweze kuendelea kupigana, na alipokuja Yaziyd kumtembelea alimuuliza:

“Una utumwa gani ewe Abuu Ayyuwb?”

Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akasema:

“Nitolee salaam kwa askari jeshi wa Kiislamu na waambie kuwa Abuu Ayyuwb anawausieni musonge mbele na kuingia ndani kabisa katika ardhi ya adui kiasi mnavyoweza na waambie kuwa wanichukuwe na kunizika penye kuta za Contantinople (Uturuki),”

 

Usia wake ulitekelezwa na askari wa Kiislamu waliomchukua Abuu Ayyuwb (Radhwiya Allaahu ‘anhu) akiwa juu ya farasi wake, wakapigana vita vikali dhidi ya adui mpaka wakaweza kuiteka nchi ya Costantinople. Na walipowasili penye kuta zake mahali panapoitwa hivi sasa 'Istanbul' wakachimba kaburi na kumzika hapo.

 

 

 

 

 

 

 

 

Share