Abu Bakr Asw-Swiddiyq (رضي الله عنه)

 

Abu Bakr  رضي الله عنه  Na Sababu Za Kupewa Cheo Cha  'As-Swiddiyq' (Msema Kweli)

 

Al-Imaam An-Nawawiy amesema: "Ummah umekubaliana kwa pamoja bila ya kupingana kwamba amepewa cheo cha 'As-Swiddiyq' kutokana na kuitikia kwake haraka kumuamini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  bila ya kusita na kukubali maneno yake kwamba daima ni ya ukweli. Alibakia kuwa mkweli maishani mwake kote wala hajapata kusema uongo  hata mara moja". 

Ibn Kathiyr amesema: "Kuhusu cheo chake cha  'As-Swiddiyq', inasemekana kwamba alipewa tokea zama za Ujaahiliyyah kutokana na ukweli uliojulikana kwamba alikuwa ni mkweli. Vile vile imesemekana kwamba amepewa cheo hicho kwa sababu alikuwa daima yuko tayari kumuamini Mtume صلى الله عليه وآله وسلم katika kila jambo alilosema".

Baadhi ya matukio yaliyodhihirisha ukweli wake na wepesi wake wa kuamini lolote alilosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم :

1.    Katika kisa cha Israa Wal-Mi'raaj alipobakia kuwa thabiti na kuwaambia makafiri kwamba ikiwa Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم  mwenyewe ametamka maelezo hayo basi ni kweli!

Ibn Kathiyr amesema: "Al-Hasan Al-Baswriy na Qataadah wamesema: "Alijulikana kwa mara ya kwanza kwa cheo hiki asubuhi ya siku ya tukio la Israa". Al-Haakim amesimulia kutoka kwa Bibi 'Aishah رضي الله عنها  ambaye amesema: Washirikina walikuja kwa Abu Bakr wakamwambia: "Umemsikia rafiki yako anavyodai? Anadai kwamba amesafiri kwenda Baytul-Maqdis kwa usiku mmoja" Akauliza: "Je, amesema mwenyewe hivyo?". Wakajibu: "Ndio". Akasema: "Basi amesema ukweli! Naamini ukweli wake katika mambo yaliyo ya ajabu zaidi kuliko hayo, kama 'habari kutoka mbinguni asubuhi na jioni" (yaani wahyi wa Qur-aan). Tokea hapo Abu Bakr akapewa cheo cha 'As-Swiddiyq'.  [Ibn Kathiyr kasema Isnaad yake ni nzuri].

Al-Haakim amesimulia kutoka Nazaal ibn Swabrah ambaye amesema: "Tulimwambia 'Aliy: "Ewe kamanda wa waumini! Tuelezee kuhusu Abu Bakr". Akasema: "Ni mtu aliyepewa jina la 'As-Swiddiyq' na Allaah سبحانه وتعالى kwa kauli ya Jibriyl عليه السلام na kauli ya Muhammad  صلى الله عليه وآله وسلم . Alikuwa ni Khalifa  wa Mtume صلى الله عليه وآله وسلم. Yeye Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliridhika naye katika dini yetu na aliridhika naye katika mambo yetu ya kidunia".  [Ibn Kathiyr kasema: Isnaad yake ni nzuri]

Na katika Hadiyth ya vita vya Uhud, Mtume صلى الله عليه وآله وسلم aliliambia jabali        la Uhud lilipotikisika (kwa kulipapasa)

((أثبت أحد فإنما عليك نبي وصديق وشهيدان))

((Tulia kwani juu yako yumo Mtume, As-Swiddiyq na mashahidi wawili)) (yaani ‘Umar na ‘Uthmaan رضي الله عنهم) [Al-Bukhaariy]

2.    Kuhama (Hijrah) kwake na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akiwa ameacha familia yake ili abakie na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم . Maswahaba wote waliruhusiwa na Mtume صلى الله عليه وآله وسلم kuhama (Hijrah kutoka Makkah kwenda Madiynah) isipokuwa Abu Bakr. Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alikuwa akimwambia abakie ili awe swahib (rafiki) yake katika Hijrah na Allaah سبحانه وتعالى Akatimiza pendekezo la Mjume Wake  صلى الله عليه وآله وسلم .  Kisha yaliyotokea walipokimbilia katika pango la At-Thawr na   Aayah iliyoteremeshwa kuelezea hivyo:

  ((إِلاَّ تَنصُرُوهُ فَقَدْ نَصَرَهُ اللّهُ إِذْ أَخْرَجَهُ الَّذِينَ كَفَرُواْ ثَانِيَ اثْنَيْنِ إِذْ هُمَا فِي الْغَارِ

 إِذْ يَقُولُ لِصَاحِبِهِ لاَ تَحْزَنْ إِنَّ اللّهَ مَعَنَا فَأَنزَلَ اللّهُ سَكِينَتَهُ عَلَيْهِ وَأَيَّدَهُ بِجُنُودٍ

لَّمْ تَرَوْهَا وَجَعَلَ كَلِمَةَ الَّذِينَ كَفَرُواْ السُّفْلَى وَكَلِمَةُ اللّهِ هِيَ الْعُلْيَا وَاللّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ))

((Ikiwa nyinyi hamtamnusuru Mtume, basi Allah  Alikwishamnusuru walipomtoa waliokufuru, naye ni wa pili katika wawili walipokuwa katika pango, naye akamwambia swahibu yake: Usihuzunike. Hakika Allah Yu pamoja nasi. Allah Akamteremshia utulivu wake, na Akamuunga mkono kwa majeshi msiyoyaona, na Akalifanya neno la waliokufuru kuwa chini, na Neno la Allah kuwa ndilo juu. Na Allah ndiye Mwenye nguvu Mwenye hikima)) [At-Tawbah:40

3.    Alipolia wakati Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alisema: ((Hakika kuna mja alipewa uchaguzi na Allaah سبحانه وتعالى   baina ya Duniya na Akhera, mja akachagua Akhera)). Abu Bakr alijua kuwa huyo mja ni Mtume صلى الله عليه وآله وسلم na alitambua kauli hiyo imemaanisha kwamba Mtume صلى الله عليه وآله وسلم  ataaga duniya karibuni. [Al-Bukhaariy]

4.    Alipobakia kuwa thabiti katika kifo cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم wakati Maswahaba waliduwaa hawakujua la kufanya na khutbah yake aliyotoa ya kuwatuliza.

5.    Kuthibitika kwake ingawa alikuwa pekee katika kupeleka jeshi na    kumfanya Usaamah bin Zayd awe mwenye kuongoza jeshi.

6.    Kung'ang’ania kwake katika kupigana na watu waliotoka nje ya Uislam baada ya kifo cha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم

7.    Alipomchagua 'Umar bnul-Khattwaab رضي الله عنه kuwa Khaliyfah wa Waislam, lilikuwa ni chaguo tukufu lililokubalika na Ummah na ni jambo ambalo limeainishwa na Maulamaa kuwa ni jambo mojawapo muhimu la mafanikio katika historia.

 

 

 

 

Share