Ipi Bora Kuhifadhi Qur-aan Yote Bila Ya Kujua Maana Au Kuhifadhi Kidogo Kwa Maana?

 

Ipi Bora Kuhifadhi Qur-aan Yote Bila Ya Kujua Maana Au Kuhifadhi Kidogo Kwa Maana?

 

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

Assalam alaykum warahmatuLLaahi  wabarakatuhu. Nataka nipate ufumbuzi kuhufadhi Quran ni kusoma zwahiri, au nikuhifadhi bila ya kujuwa maana yake au ni kuhifadhi na maana yake? Kwa sababu nilisikia kama mtu akihifadhi Quran hataingiya motoni.

 

Na nani kahifadhi kati ya yule anasoma Quran yote bila kuifaham maana yake na yule anae juwa sura kumi na maana yake? Barakallahu  fikum  wasalam alaykum warhamatullahi wa Barakatuhu

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hakika ambayo haipingiki na yeyote mwenye akili timamu ni kuwa Qur-aan imeteremshwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kutimiza malengo fulani kwa wana Aadam. Lengo kubwa zaidi ni kuwaongoza watu wote katika njia nyoofu na ya sawa kama Anavyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):

شَهْرُ رَمَضَانَ الَّذِي أُنزِلَ فِيهِ الْقُرْآنُ هُدًى لِّلنَّاسِ وَبَيِّنَاتٍ مِّنَ الْهُدَىٰ وَالْفُرْقَانِ ۚ  

Mwezi wa Ramadhwaan ambao imeteremshwa humo Qur-aan ili iwe mwongozo kwa watu na hoja bayana za mwongozo na pambanuo (la haki na batili).  [Al-Baqarah: 184]

 

 

na hivyo hivyo kwa wenye taqwa kama Anavyosema pia Allaah ('Azza wa Jalla):

 

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ ﴿٢﴾

Hiki ni Kitabu kisicho na shaka ndani yake, ni mwongozo kwa wenye taqwa [Al-Baqarah: 2]

 

 

Kwa minajili hiyo ni bora na muhimu zaidi kwa Muislamu kuisoma Qur-aan kwa kuizingatia maana yake pamoja na kufuata kimatendo yaliyomo ndani. Hivyo ndivyo walivyokuwa wakifanya Wema waliotangulia.  Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu 'anhuma) alikuwa akisoma Aayah kumi, anazihifadhi na kutekeleza kimatendo maagizo yaliyomo ndani yake. Kwa njia hiyo alichukua miaka kumi kuihifadhi Suwratul-Baqarah [Maalik].

 

 

Maswahaba nao ndivyo walivyokuwa wakifanya walikuwa hawachukui Aayah nyengine hata kama zimeteremka siku hiyo mpaka zile walizokuwa nazo kuzihifadhi pamoja na kutwabikisha amri zilizomo ndani.

 

Japokuwa kuhifadhi Qur-aan kuna fadhila zake, na kila unaposoma  herufi utapata thawabu kumi, lakini henda mtu akawa anasoma Qur-aan na huku inamlaani lakini hajui wala hatambui hilo.

 

Pia sisi hatutakiwi tuwe na ile sifa ya Mayahudi kama Anavyosema Allaah ('Azza wa Jalla):

 

 

مَثَلُ الَّذِينَ حُمِّلُوا التَّوْرَاةَ ثُمَّ لَمْ يَحْمِلُوهَا كَمَثَلِ الْحِمَارِ يَحْمِلُ أَسْفَارًا ۚ بِئْسَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ ۚ وَاللَّـهُ لَا يَهْدِي الْقَوْمَ الظَّالِمِينَ﴿٥﴾

Mfano wa wale waliobebeshwa Tawraat, kisha wasiibebe ni kama mfano wa punda abebaye mijalada ya vitabu. Ubaya ulioje mfano wa watu waliokadhibisha Aayaat za Allaah, na Allaah Haongoi watu madhalimu. [Al-Jumu’ah: 5]

 

 

Udhalimu unakuwa mkubwa ikiwa tutaibeba Qur-aan vifuani mwetu lakini hatuitilii maanani. Ndipo Allaah ('Azza wa Jalla)  Anasema:

 

أَفَلَا يَتَدَبَّرُونَ الْقُرْآنَ أَمْ عَلَىٰ قُلُوبٍ أَقْفَالُهَا﴿٢٤﴾

Je, hawaizingatii Qur-aan; au nyoyoni (mwao) mna kufuli? [Muhammad: 24]

  

Nasiha zetu za dhati kwa ndugu zetu ni kuwa mtu asome juzuu au hizbu au hata ukurasa mmoja wa Qur-aan kila siku bila kuacha pamoja na kufanya bidii kuhifadhi Suwrah au baadhi za Aayah anazoweza. Hivyo hivyo atenge wakati wa kusoma Tafsiyr kuanzia mwanzo wa Suwratul-Faatihah kidogo kidogo na kufanya juhudi kutekeleza hayo kimatendo.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

Share