Anaweza Kughushi Ili Mkewe Apate Shahada Za Kumwezesha Kuendelea Na Masomo Ya Juu?

Anaweza Kughushi Ili Mkewe Apate Shahada Za Kumwezesha

Kuendelea Na Masomo Ya Juu?

 

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam aleikum ndugu zangu alhidaaya. Shukran za dhati kwa kazi hii ngumu ya daawah. Mimi ni kijana ambae nilioa mapema kwa kuhofu mtihani wa zinaa, bila ya kutarajia nililazimika kwenda kusoma nje ya nchi yangu ambako fitna ni nyingi zaidi. Nimejaribu kila njia kuomba adminstration ya chuo nimlete mke wangu bila mafanikio kwa hoja kuwa undergraduates hawaruhusiwi kufanya hivyo. Badala yake wakanihakikishia kuwa watampa nafasi ya postgraduate kama ana qualify, kitu ambacho haiwezekani kwa mke wangu kwa sababu ana elimu ya sekondari. Je, Kuna dharura yoyote ya kughushi vyeti ili niweze kustirika na hii mitihani?

 

 

JIBU:

 

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Tufahamu kuwa kughushi ambao ni udanganyifu ni mtihani mkubwa zaidi kuliko mtihani huo mwengine unaouzungumzia. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliulizwa: “Je, Muislamu aweza kuwa muoga?’ Akasema: ‘Ndio’. Akaulizwa tena: ‘Je, aweza kuwa bakhili?’ Akasema: Ndio’. Akaulizwa tena: ‘Je, Muislamu aweza kudanganya?’ Akasema: ‘Hapana” [Ahmad].

 

 

Katika Hadiyth nyingine, amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Yeyote mwenye kutughushi, si katika sisi” [Muslim]

 

Na fahamu kuwa kujulikana na chuo kuwa umeghushi inaweza kukuletea matatizo makubwa zaidi kuliko kuwa na mtihani huo ulio nao sasa. Tazama hali ya kuwa umepata cheti hicho na mkeo amefanyiwa mtihani, je, ataweza kuupita kwani daraja ya elimu ya mtu wa sekondani na aliye na digrii ni tofauti kubwa sana. 

 

Hivyo, ki-Shariy'ah haifai kwako kufanya hilo. Tunakuomba uvumulie na uzidi kumuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Akufanikishie mambo yako yote. Nasaha nyingine ni kuwa unaweza kuomba chuo kikupatie usaidizi kwa kumpatia mkeo fursa ya kufanya digrii ya kwanza.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share