Ameoa Mwanamke Asiye Muislamu Baada Ya Kuzaa Naye Nje Ya Ndoa, Naye Bado Hakubadili Dini Wala Hana Niyah, Nini Hukmu Yake?

SWALI:

 

Assalam aleykum warahmatullah taaala wabarakatu!

 

Napenda kuuliza swali hili kwa niaba ya kaka yangu wa kiislamu ambaye yuko katika ndoa ambayo kwamba hana uhakika inaswihi au haiswihi kwa mwanamme wa kiisalam. Kwanza kaka huyu aliishi na mwanamke wa kikatoliki bila kumuoa kwa zaidi ya mwaka, wakajaaliwa kupata mtoto na hapo ndipo alipochukua hatua yakumuoa mwanake huyo,je ndoa hii katika uislamu inakubalika? Na kama haikubaliki au inakubalika naomba unipe ufafanuzi nipate kuelimika na nukumuelimisha kaka yangu juu ya swala hili.

 

Pia mwanake huyu ambaye kaka yangu anaamini ni mke sasa wamekuwa pamoja kwa zaidi ya mwaka lakini bado hajawa mislamu na wala katika kipidi kitakatifu kama hiki hafungi wala kuswali. Je mwanamme wa kiislamu anaruhusiwa kuoa mwanamke wakikirsto nakuendelea kuishi nae muda wote hata kama hatobadili dini nakuwa muislamu?

 

 

Allah (Subhanahu wataala) akupe wepesi katika kujibu swali hili


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kumuoa mwanamke wa Kikristo katika sheria.

Awali ya yote tunataka kukunasihi kuwa mwanzo umpe nasaha kaka yako kwa yaliyopita katika maisha yake. Uzinifu katika Uislamu ni dhambi kubwa ambalo kusamehewa linahitaji aliyefanya atubie kwa Mola wake Mlezi toba ya sawa na kikweli. Kisha inafaa aelewe kuwa yule mtoto wake wa kwanza si wake kisheria, na mmoja akifa hawarithiani kabisa. Pia umetueleza kuwa kaka yako baadaye alimuoa huyo mwanamke bila kutueleza kama alimuoa Kiislamu, Kikatoliki au kimila? Ni ndoa ya Kiislamu tu ndio inayokubalika kisheria.

 

Uislamu umetupatia muongozo kuhusu kuwaoa watu wa Kitabu (Mayahudi na Wakristo). Ruhusa hiyo imetolewa lakini kwa kuwekewa sharti ambalo linahitajika lipatikane kusihi hiyo ndoa. Allaah Aliyetukuka Anatuambia: “Na ni halali kuwaoa wanawake wema walio waumini na wema miongoni mwa wale waliopewa Kitabu kabla yenu nyinyi ikiwa mtawapatia ujira wao (mahari) mkafunga nao ndoa, bila kufanya uzinzi wala kuwaweka wanawake wa kinyumba” (5: 5). Kwa kuwa kaka yako alikaa naye kinyumba hiyo inaondoa sifa ya mwanamke mwema miongoni wa waliopewa Kitabu.

 

Hata ikiwa mwanamke wa Kikristo ni mwema anayejitunza muruwa maadili na tabia yake itakuwa si katika maslahi kwa Waislamu kuwaoa kwani ikiwa kila Muislamu atakimbilia Mkristo, wasichana wetu wataolewa na nani? Itabidi wasichana wetu nao wachukuliwe na Wakristo hivyo kuleta maafa makubwa sana kwa jamii. Ndio baadhi ya madhehebu wana msingi wa sheria unatambuka kama maslahi.

 

Imepatikana pia katika maeneo mengi katika nchi kadhaa kwa watoto wanaozaliwa kuingizwa katika Dini za mama zao. Au ikiwa kunatokea ugomvi unaopelekea wanandoa hao kuachana, nchi nyingi inampatia haki ya ulezi mama. Na ikiwa mama ni Mkristo basi inatarajiwa kuwa na mtoto naye atakuwa wa Dini hiyo.

 

Hivyo, inatakiwa tutahadhari sana juu ya suala hilo tusije tukaingia katika balaa ambayo haitakuwa na mwisho mzuri kwa jamii.

 

La kufanya ni kumnasihi kaka yako na umjulishe kuwa misingi sahihi ya kuishi na huyo mwanamke ilikiukwa tokea mwanzoni na anatakiwa afanye Tawbah ya kweli kweli na afuate taratibu sahihi ikiwa atataka kuishi na huyo mwanamke. Na kisha akitaka amfanyie Da‘wah huyo mwanamke ili apate kusilimu na kisha afundishwe Dini ili ajikite katika hilo kwa ufanisi wake huyo mtoto hapa duniani na kesho Akhera.

 

Kwa hivi sasa ni bora umnasihi ajitenge naye ikiwa kweli anamuogopa Allaah, na atekeleze kwanza hayo tuliyoyaeleza hapo juu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share