Mama Ameolewa Na Mume Mwengine Baada Kutengana Na Baba Kisha Baba Karudi Kudai Ni Mkewe

SWALI:

Kwanza Namshukuru ALLAH (SUBHANNAH .WATAALA) Kwa Kutujalia Afya (Pumzi) Mpaka Muda Huu, Kwani Ni Wachache Wanoomba Kuwa Na Neema Hii Lakini Wameshindwa, Pili Napenda Kuwashukuru Sana Kwa Kazi Yenu Nzuri Kwa Hakika Ujira Wenu Mtaukuta Kwa Lilahi Mwingi Wa Rehema.

Mimi Ni Bint Niliyezaliwa Miaka 25 Iliyopita, Ktk Kukuwa Kwangu Nimelelewa Na Mama Yangu Mzazi, Sikuwahi Kumjua Baba Mzazi Kwani Nilikuta Wameshatengana Na Mama. Mama Yangu Alinitunza Kwa Kila Kitu Mpaka Nilipofika Kidato Cha Pili, Nilipofika Kidato Cha Pili Alinipeleka Kwa Mjomba,

Nililelewa Kwa Mjomba Kwa Muda Wa Miaka Miwili Nikamaliza Kidato Cha Nne, Mjomba Wangu Alinifundisha Dini (Maarifa Ya Uislamu) Nikaelewa Dini Yangu Vizuri Mno Mpaka Sasa Hivi Namshukuru ALLAH  (SUBHANNAH .WATAALA)  Kwa Hakika Amlipe Kila Rakheri Mjomba Wangu.

Lakini Ktk Kukuwa Kwangu Nilikuwa Nikiomba Kila Siku Ktk Swala Zangu ALLAH (S.W) Anijalie Nimjue Baba Yangu Mzazi, Awe Hai Nijue Na Kama Alishafariki Napo Pia Nielewe Ili Niweze Kuwafahamu Hata Ndugu Zangu Upande Wa Baba. Nilianza Juhudi Za Kumtafuta Baba Kwa Kila Hali Na Ninamshukuru ALLAH (SUBHANNAH .WATAALA)   Kwani Niliweza Kutumia Vitu Kama Computer Hivyo Nilijitahidi Kwa Kila Hali Kumtafuta Baba.

Baada Ya Kumweleza Mama Yangu Mzazi Kuwa Mimi Sasa Nimeshakuwa Mtu Mzima Hivyo Nahitaji Kumjua Baba, Kwahiyo Niliitaji Msaada Kutoka Kwake Wa Kumpata Baba Yangu Mzazi. Alinieleza Kwa Kirefu Naweza Kutumia Njia Kufanikiwa Kumpata. Na Akanieleza Kuwa Yeye Alitengana Na Baba Yangu Mzazi Kwa Sababu Za Utafutaji Kwani Baba Yangu Alikuwa Ni Mfanyabiashara Na Alikuwa Akienda Sehemu Anamsahau Kabisa Mama Pamoja Na Mimi Kwa Kipindi Cha Mwaka Mzima, Familia Ya Kwao Na Mama Walimwita Baba Na Kumkanya Kuwa Hajali Familia Yake Kwani Alikuwa Na Uwezo Wa Kuondoka Miezi 9 Mpaka Mwaka Mzima Hana Habari Na Familia Na Hajui Wamekula Au Wamelala Njaa, Hivyo Tabia Yake Ilivyoendelea Mama Akabidi Atoke Yeye Mwenyewe Kwa Baba. Akakaa Kwa Ndugu Kama Mwaka Alafu Baadae Akaolewa Na Mume Mwingine Ambaye Mpaka Sasa Wako Wote  Ambaye Ni Baba Yangu Wa Kambo.

Process Zangu Mie Za Kumtafuta Baba Hazikuishia Hapo Atimaye Allah (Subhanna Wataala) Akanitilia Wepesi Ktk Juhudi Zangu Nikampata Baba Yangu Mzazi. Nilifurahi Mno Nikampigia Cm Alikuwa Safari Nairobi Nilivyomweleza Kwa Kirefu Ktk Cm, Akafunga Safari Hadi Kwangu Akaniona Nami Nikamuona, Kwa Furaha Aliyokuwa Nayo Alisali Sunnat Shukru Kwa Kunipata. Nilimuhoji Mambo Mengi Mpaka Mengine Alishindwa Kunijibu Ila Tu Aliniambia Kuwa "Wewe Mshukuru Mola Umenipata Je? Ungesikia Mimi Nimekufaungefanyaje Hivyo Maswali Ya Kunihoji Naomba Uachane Nayo Maisha Ndio Yaliyosababisha Mimi Nikatengana Na Mama Yako". 

Sikuendelea Kumuuliza Maswali Tena, Tulipanga Safari Mimi Na Yeye, Akanipeleka Kwake, Nikakuta Ana Wake Wawili Na Watoto. Nikakaa Kipindi Cha Wiki Tatu Huku Nikifanya Uchunguzi. Ktk Uchunguzi Wangu Nikagundua: -

Hayuko Makini Na Familia Yake Kwa Ujumla, Nyuma Alishaoa Wake Ila Walikuwa Wanaondoka Kwa Kuachika Bila Talaka Kwa Sababu Alikuwa Haijali Familia, Familia Nzima Hawajishirikishi Kabisa Ktk Kumjua ALLAH (SUBHANNAH .WATAALA) Wanaishi Wanavyotaka Wao Bila Kufata Muongozo Wa ALLAH , (SUBHANNAH .WATAALA)  Elimu Hawaipi Kipaumbele Si Ya Dini Wala Dunia Wanaishi Maisha Ya Kufata Mila Jambo Linaloipelekea Familia Kumuasi ALLAH (SUBHANNAH .WATAALA), Baba ni mtu ambaye amesoma Dini anaelewa ila utekelezaji hana na ni sawasawa na mtu ambaye hajasoma kwa sababu elimu yake haimfai chochote.

Akanipeleka Kwa Babu Yangu Yaani Mjomba Wake Yeye, Nikakaa Siku Tatu Na Kuomba Kuondoka. Kabla Sijaondoka Wakaniambia Kuwa Lazima Wanitambikie Siwezi Kuondoka Bila Kufanyiwa Hizo Mila Zao. Nilikataa Kwa Sababu Nilijua Naingia Ktk Shirk, Baada Ya Kukataa Baba Yangu Akiwa Na Mama Yangu Wa Kambo Pamoja Na Ndugu Wengine Waliniita Wakaniambia Kubali Wakufanyie Alafu Ndio Uondoke. Nilikubali Ila Nikawapa Sharti La Kutochanjwa Chale Hata Moja Ktk Mwili Wangu Basi Walinifanyia Hayo Matambiko Yao Bila Kunichanja Ila Walinipa Maji Ya Kuoga Nikaoga Na Baada Ya Kumaliza Walinipa Dawa Za Kuoga, Kujipaka, Na Ya Kunuia Huku Unasema Kwa Kitu Unachotaka. Nikapokea Dawa Na Sikuonyesha Kuwapinga Pale Kijijini.

Tulivyofika Mjini Kwa Baba Niliitisha Kikao Nikawaeleza Maisha Wanayoishi Sivyo Inabidi Watoe Toba Na Dawa Zile Nikasema Sifanyi Hata Moja Nitazitupa Chooni Na Nikawaambie Wamwamini Mumgu Mmoja Tu Aliyeumba Mbingu Na Ardhi Wasitegemee Mambo Ya Mizimu.

Nikawa Nawahusia Kufanya Ibada Ila Wakawa Wanaleta Hoja Ambazo Hazina Maana. Nikamwita Baba Chumbani Nikamwambia Baba Wewe Sasa Ni Mzee Kweli Ni Mzee Wa Makamo Ila Kwa Maisha Mazuri Anayoishi anaonekana Hajazeeka Sana. Nikamwambia Baba Yangu Mpendwa Toa Toba Na Ufate Yale Yote ALLAH  (SUBHANNAH .WATAALA) Anayoridhia, Alinielewa Kwa Asilimia Chache Sana Na Mengine Akawa Ananipinga.

Baada Ya Kuridhika Niliomba Kuondoka Kurudi Nyumbani, Baba Alinirudisha Hadi Nyumbani Nikampeleka Kwa Mama Yangu Mzazi, Akapokelewa Vizuri Sana Na Baba Yangu Wa Kambo Pamoja Na Mama. Baada Ya Muda Akaomba Kuondoka Tukamsindikiza Kwa Furaha Akaondoka. Ila kabla hajaondoka akaniambia kuwa anaenda kufanya process za kuja kurudiana na mama kwa sababu yeye bado anampenda na mama bado anampenda na halivyoachana naye hakumpa taraka hivyo yeye bado anajua ni mkewe na akanishukuru mimi kwa juhudi zangu za kumfafuta kwani nimeunganisha ukoo. Mimi nikamweleza kuwa haiwezekani amuoe mama tena kwa sababu mama yangu ana mume mwingine ambaye ni baba yangu wa kambo hivyo aridhike tu na hao wake zake, Nikamwambia hakuna ndoa hapo tena ila watakuwa (wanazini) nilipomweleza kwa ukali zaidi naye akaja juu, basi mie kwa kuwa ni motto nikawa mpole ila nikamweleza kuwa nitamtafuta shekhe anipe suluhu alafu mie nije niwaambie nyie wazazi mkifata nitashukuru, mkikataa nitawaacha ila siko tayari kuona mnafanya dhambi mbele yangu.

Nikachukua zile dawa nilizopewa nikazitupa, nikamuomba ALLAH (SUBHANNAH .WATAALA) kwa kutoa toba. Kwa sababu hayo mambo siyaamini hata kidogo na ninaamini chochote kinachomtokea mja ni KADAR kutoka kwa LILLAHI.

Sasa Naomba Mnisaidie Maswali Yangu Ni Haya: -

1.      Mwenyezimungu Amepokea Toba Yangu Niliyotoa Kwa Yale Matambiko Niliyofanyiwa Kule Kwa Babu.

 

2.      Nifanyeje Ili Familia Ya Baba Ifate Sheria Za Allah (S.W) Kwani Ni Watu Walio Ktk Upotevu.  

3.      Baba Yangu Wa Kambo Na Mama Yangu Kuna Ndoa Hapo Ktkt Wakati

4.      Nilivyomuuliza Mama Akaniambia Walifungia Ndoa Ya Selekarini.  

5.      Baba Yangu Mzazi Kweli Ni Halali Yake Kumchukua Mama Yangu Mzazi Kumtoa Kwa Huyu Baba Yangu Wa Kambo Ambaye Ameshazaa Nae Watoto.  

6.      Lipi Lifanyike Hapo Lililo La Haki Ili Niwaeleze Kabla Ya Kuharibu Zaidi Mambo.

7.      Je? Wakikataa Kufata Haki Wakafata Kinyume Na Maneno Ya Allah (S.W)

8.      Mimi Nitakuwa Nimeshiriki Hizo Dhambi? Kwa Sababu Mimi Niliyemtafuta Baba Ndiye Ninayeambiwa Nimewaunganisha.

9.      Baba Nina Haki Ya Kumtii Kama Baba Yangu Mzazi Kwa Lolote Analoniambia Na Lisiwe La Kumshirikisha Allah (S.W).

10.  Nina Haki Ya Kumtunza Baba Kwa Kila Jambo Kama Allah (S.W) Anavyotueleza Kuwafanyia Uadilifu Wazazi Wawili.

11.  Baba Na Mama Walifungia Ndoa Serikalini Je? Mimi Si Ni Mtoto Wa Zinaa, Na Kama Ndio Baba Ana Haki Yoyote Juu Yangu (Au Mimi Nina Haki Ya Kumfanyia Baba Uadilifu Ingawa Nitakuwa Ni Mtoto Wa Zinaa).

Nategemea kwa uwezo wa ALLAH  (SUBHANNAH .WATAALA) nitapata majibu ya maswali yangu haraka kabla mambo hayajaaribika zaidi. MWENYEZI MUNGU WATILIE WEPESI.

Naomba mnisamehe kwa kutuma barua yangu sehemu isiyohusika kwa sababu nimeshajali sana kutuma ktk kipengele cha maswali ila imekataa kwenda nadhani ni kwa sababu ya maneno kuwa mengi na nimejalibu kupunguza ila imeshindikana, samahani kwa usumbufu. 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Tunavyoona ni kweli una maswali ya kujibiwa na ni ya msingi lakini kwa umuhimu wa maswali na hatari yake kuendelea kuwa katika hali hiyo ni vyema na ushauri wetu uwe na kawaida bali ndio lengo na ndio jambo zuri kuwa na Shaykh au mtaalamu wa kumuuliza katika eneo ulioko ambaye ana uwezo wa kukujibu na kukufunua macho au uliza upendekezewe mtu atakayeweza kukusaidia katika kupata utatuzi wa masuali yako badala ya kusubiri kujibiwa katika tovuti jambo ambalo wahusika wana mambo mengine kwani wengi wao wana kazi za kufanya kuendesha maisha yao ya kila siku na wakati uliobaki huwa ndio wanajaribu kusaidia wenzao kwa kile walichopewa na Mola wao katika kufanikisha kazi aliyoianza Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hivyo basi kwa kuleta masuala kama haya huenda yakachukua muda na kumbe au kwa hakika katika eneo unaloishi yawezekana kuwepo wanaoweza kujibu tena kwa haraka na kwa ufanisi iwe uso kwa uso au vyenginevyo.

Na kama kuna hisia kuwa unahitaji ziada ya kueleza na kunasihiwa au kutanabahishwa na kutahadharishwa ubaya wa jambo kama hili la shirki na kuwa ni dhambi kubwa kabisa katika Uislamu si hilo tu bali ni jambo lenye kuangusha na kuangamiza mema yote aliyoyatenda mja na kubwa kuliko hilo ni kuwa mwenye kufa hali ya kuwa ni mshirikina hakuna uwezekano wa kupata kuingia peponi kabla mambo hayajaharibika zaidi kwani Allaah Ameharamisha Pepo kwa kila mshirikina kama atakufa bila ya kutubia; Allaah Anasema:

“Hakika wamekufuru walio sema: kuwa Allaah ni Masihi mwana wa Maryamu! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Allaah, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Allaah, hakika Allaah Atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na waliodhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru”. Al-Maaidah: 72.

Hivyo basi pendekezo letu ni kuwa tuwatumie walio karibu kutusaidia katika kuelewa dini yetu na hasa katika mambo yenye kutakiwa kupatikana ufumbuzi au hukumu ya dini kwa haraka kabla ya kuharibikiwa zaidi; kwani masuala hasa kama haya ambayo yana hatari kucheleweshwa si vyema mtu kuyatuma bali ni kumfuata mtaalamu au Shaykh na kumuuliza tena kwa haraka na kuyatuma katika tovuti ni kuongezea ufafanuzi kwa wengine na sio vyenginevyo.

Umesema, Mwenyezimungu Amepokea Toba Yangu Niliyotoa Kwa Yale Matambiko Niliyofanyiwa Kule Kwa Babu. Ndugu yetu, fahamu kuwa Uislamu umeweka wazi kuwa mwenye kutubia tawbah ya kweli kweli tawbatun Nasuwhah anakubaliwa tawbah yake na Allaah maadamu hajafikia wakati wa kutokwa roho; hivyo insha Allaah kama ulileta tawbah kama hiyo basi insha Allaah Allaah Ataikubali na uwe kila wakati unajuta kwa kitendo chako kile na usiwe tayari kukirejea katika maisha yako yoye mpaka ukutane na Mola wako.

Ukauliza, Nifanyeje Ili Familia Ya Baba Ifate Sheria Za Allah (S.W) Kwani Ni Watu Walio Ktk Upotevu. Kwa kweli huna la kufanya zaidi ya lile ulilofanya wewe na kuweza kwa tawfiqi yake Mola kufika kuwa na elimu ya kuelewa haya unayoelewa; hivyo la kufanya ni kuwaelimisha na kuwafahamisha kwa njia iliyo nzuri na kujaribu kuwa karibu nao kila wakati iwe wewe au waislamu wengine ambao wanaelewa dini yao ili wapate kuwaelekeza na kuwakataza yatayowapelekea kurejea tena hayo waliyonayo.  Elimu pekee ndio ufunguo wa matatizo ya familia yako, hivyo ni njia gani wataweza kuelimika au kuipata hiyo elimu hilo litawezekana kulingana na mazingira waliyoko kwani hapa hatukusudii kwenda kusoma darasani pekee bali ni mchanganyiko wa mbinu na njia zitakazoweza kuwasaidia kuelewa kuwa wanahitaji kutubia na kurejea kwa Mola wao Asiyehitaji mshirika.

Umesema, Baba Yangu Wa Kambo Na Mama Yangu Kuna Ndoa Hapo Ktkt Wakati, ndoa yao kama ilifungwa kwa kufuata masharti ya ndoa ya Kiislamu basi haina mashaka vyenginevyo kama tulivyoshauri utahitaji kuwaona ma-Qaadhi wa eneo lako kama wako au ma-Shaykh wa hapo na kulijadili suala zima la uhalali wa ndoa ya baba yako wa kambo na mama yako kwani kama lilifungwa serikalini bila ya shaka yoyote ile litahitaji ushauri wa ma-Shaykh hapo ulipo au hapo ilipofungwa hiyo ndoa yenyewe.

Ukaeleza, Nilivyomuuliza Mama Akaniambia Walifungia Ndoa Ya Selekarini.  Kipi kiliwapelekea hata wakenda kufunga ndoa yao serikalini?! Kama kuna sababu basi zitachambuliwa na kama hakuna bali waliona kuwa hilo ndio sahihi kwa kuwa mama yako hakuachwa na baba yako na waliona kuwa hakuna njia ya kufanya ujanja wa kupata kuoana isipokuwa kwenda serikalini na kuoana basi mama yako bado ni mke wa watu na hakuachwa ilitakikana talaka na ndipo ifungwe ndoa na hilo kama halikupatikana basi wao walikuwa wakizini kwa hukumu ya dini waliyokuwa nayo kama ni Uislamu; hata hivyo hao ma-Shaykh ndio wataweza kutoa uamuzi.

 

Ukasema, Baba Yangu Mzazi Kweli Ni Halali Yake Kumchukua Mama Yangu Mzazi Kumtoa Kwa Huyu Baba Yangu Wa Kambo Ambaye Ameshazaa Nae Watoto.  Hili jawabu lake ni hapo juu kwani kama alimuoa kisharia na hakumuacha basi bado ni mkewe; lakini tunasisitiza kuwaona ma-Qaadhi au ma-Shaykh wa eneo lako ili wakupe uwazi wa hali ya ndoa kama ipo hiyo ndoa ya pili kwani ndoa ya kwanza haijavunjwa wala haijavunjika sasa vipi ataolewa na mume mwengine wakati mume wa kwanza hajamuacha wala hajajiachishwa?

Ukauliza, Lipi Lifanyike Hapo Lililo La Haki Ili Niwaeleze Kabla Ya Kuharibu Zaidi Mambo. Ushauri wetu ni kutafuta wazee wenye elimu ya dini yao ya kiislamu na kuwaeleza hayo na kuwataka wao kama ni wazee kumueleza huyu baba na mama kwani wewe kama ni mtoto wao hawatokuelewa na hilo litaweza kuwapelekea kuharibikiwa zaidi; tafuta wenye kuelewa dini na kuwaomba wawafahamishe na kuwatahadharisha kama ni Waislamu kuwa wanatakiwa wawe vipi na waachane na lipi?

Ukauliza tena, Je? Wakikataa Kufata Haki Wakafata Kinyume Na Maneno Ya Allah (S.W)? Usiwe na fikira hizi wao ni watu kama wengine na kauli laini itaweza kuwarejesha kwa Mola wao kwa tawfiqi yake Mola; hivyo wewe kubwa ni kuwaombea du’aa na kufanya hilo tulilokushauri hapo juu, tafuta wazee walio karibu na wao kama wako na wawe wenye elimu ya dini ya Kiislamu ili waweze kwa uwezo wa Mola kuwasaidia.

Swali lako jingine, Mimi Nitakuwa Nimeshiriki Hizo Dhambi? Kwa Sababu Mimi Niliyemtafuta Baba Ndiye Ninayeambiwa Nimewaunganisha. Huna dhambi ulivyoshiriki bali utakuwa umepelekea watu kutotenda madhambi kwani kama wao ndoa yao si halali basi watatakiwa mara moja waheshimiane na kutengana na hilo ni jambo jema na insha Allaah kwa Mola utapata ujiwa wako kama unafanya hayo kwa ajili yake kwani utakuwa unaondoa maovu na kukataza mabaya kama apendavyo Mola. Na hilo ni katika majukumu tuliyopewa na Mola kila Muislamu na wewe ni katika Waislamu.

Ukasema, Baba Nina Haki Ya Kumtii Kama Baba Yangu Mzazi Kwa Lolote Analoniambia Na Lisiwe La Kumshirikisha Allah (S.W).   pia Nina Haki Ya Kumtunza Baba Kwa Kila Jambo Kama Allah (S.W) Anavyotueleza Kuwafanyia Uadilifu Wazazi Wawili.

Ndio unayo haki hiyo bali unatakiwa uendelea na kusuhubiana na wazazi wako wote wawili kwani huna wengine isipokuwa hao hata kama walikuwa si waislamu basi bado Uislamu unakutaka ukae na uwatendee wema na ihsaan wazazi wako kwani wao ndio wazazi wako, Qur-aan inasema:

“Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Ni kwangu Mimi ndiyo marudio. Na pindi wakikushikilia kunishirikisha na ambayo huna ilimu nayo, basi usiwatii. Lakini kaa nao kwa wema duniani, nawe ishike njia ya anaye elekea kwangu. Kisha marejeo yenu ni Kwangu Mimi, na Mimi Nitakuambieni mliyo kuwa mkiyatenda.” Luqmaan: 14-15.

 

Ukaendelea kuuliza, Baba Na Mama Walifungia Ndoa Serikalini Je? Mimi Si Ni Mtoto Wa Zinaa, Na Kama Ndio Baba Ana Haki Yoyote Juu Yangu (Au Mimi Nina Haki Ya Kumfanyia Baba Uadilifu Ingawa Nitakuwa Ni Mtoto Wa Zinaa).

Hili tunakushauri usiwe na jazaba kwani wewe huna kosa na mtu kuwa mototo wa zinaa si katika makosa atayoulizwa kwani yeye si aliyetenda kosa na hata hao wazazi yawezekana kuwa hawakutenda kwa ridhaa yao kama tutasema kwani wako waliowapelekea kwenda kufunga ndoa serikalini kwa kutokufahamu kwao dini. Jambo ambalo linaeleweka kuwa mama yako bado alikuwa mke wa mtu na hakuna ndoa kwa mtu aliye na mume mpaka amwache au aachike au ajikomboe na haya yote yatahitaji ukae na wahusika tuliokupendekezea ili waweze kulitatua suala hili.

 

Wewe unatakiwa uwatendee wema na katika wema wa kuwatendea ni huko kuweza kuwafikisha pahala wakaelewa kuwa wao walikuwa katika ujahili na upotofu wa hali ya juu na hayo si mepesi kwani yanataka uwe na subira na ikhlaas kuwa unataka kuwasaidia hata kama sio wazazi wako wewe ni Muislamu na iymaan yako inshaAllaah ina nguvu na Allaah Ataizidisha. Hivyo usishughulike na hilo kwani hilo si katika yanayomtia mtu Motoni kama huna amali njema basi tunakukhofia kwenda pabaya kesho Akhera hata kama wazazi wako baba na mama ni waliofungishwa ndoa, na kama amali zako ni nzuri na kuridhiwa na Ar-Rahmaan basi inshaAllaah utakuwa katika waja wake hata kama wazazi wako baba na mama walikupata bila ya ndoa inayokubalika katika Uislamu, hili wataulizwa wao na wewe utaulizwa kwa yako na katika yako ni huku kuhakikisha kuwa wazazi wako waelewa uchafu wao na kuwa tayari kurudi kwa Mola wao na kushikamana na mafundisho ya dini mpaka kufa kwao.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share