Watoto Wa Mume Wa Pili Hawapendwi Na Mama Yao Wafanyeje?

SWALI:

 

Assalamu aleikum warahmatullah wabarakatuh, naomba kuuliza swali langu ivi, sisi tupo ndugu 9 kwetu, 5 baba wa mwanzo na 4 baba wa pili, baba wa mwanzo ameshafariki, tupo na mama etu na baba etu ambae mimi ni wa 8 kwetu.

 

Sasa ndugu zetu wa mwanzo wanamjaza maneno mama etu ili aachane na baba etu na asiwe na mapenzi kwetu kwa kua sisi tuna kazi na pia sio kama hatusaidiani ila hawapendelei na kuona choyo kwetu sisi. wallah tunasikia unyonge sana mama etu anapoongea na ndugu zetu wa mwanzo kwa uzuri na sisi kuongeleshwa kama tuliokua sio wanawe...

 

Naomba kupata ushauri wenu waislam wenzangu manake nyumba yetu inatengana sehem mbili saivi hamna utulivo wala raha na furaha...kila mtu anaiona nyumba nzito mama etu yupo hali ile...tunampenda sana mama etu na tunafanya kila anachokitaka ili afurahi lakini bado sisi tunaonekana wabaya kwake...naomba kwa hisani zenu mutusaidie. Wabillahi tawfiq


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutopendwa nyie watoto wa baba wa pili na mama yenu. Hakika hili ni jambo la kushnagaza sana, kwani mara nyingi sana kina mama wanakuwa msitari wa mbele katika kuwapenda na kuwashughulikia watoto kwa kuwa wao ndio waliohangaika kwa kiasi kikubwa.

 

Ndio kwa ajili hiyo, ukamkuta Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) akihimza kuwa kina mama wapawe haki mara tatu zaidi kuliko kina baba. Hii ni kwa ile shida ya kubeba mimba, kuzaa na kunyonyesha. Kwa hiyo, kawaida kunakuwa na mafungamano ya karibu baina ya mama na watoto wake. Ikiwa hali ni hiyo, kuwa mama hawapendi kwa kuwa anatiliwa na watoto wake wa kubwa, mama yenu atakuwa anapata dhulma iliyo kubwa kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amewausia wazazi wafanye uadilifu baina ya watoto wao.

 

Inatakiwa nyinyi msilipize kisasi kwa kuwa mama yenu anafanya dhulma hizo bali mumsaidie mama yenu kutoka katika janga la kuweza kumuingiza yeye Motoni Siku ya Kiyama. Na wale ambao wanaweza kumsaidia ni nyinyi watoto wake. Kwa kuwa lau nanyi mtataka kulipiza kisasi, mama atakuwa mkosa wa kwanza nanyi mtakuwa wakosa namba mbili na kila mmoja wenu atapata madhambi yake.

 

Nasaha ambayo tunaweza kuwapa na kwa uwezo wa Allaah Aliyetukuka huenda akabadilika ni kufanya yafuatayo:

 

  1. Jaribuni kumnunulia zawadi na vitu mama yenu kila wakati kulingana na uwezo wenu. Hii ni kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Peaneni zawadi mtapendana”.

 

  1. Jaribuni kuwa karibu naye na kumtumikia na kujipendekeza kwake. Mfano mama anapovua nguo yake ambayo ni chafu chukueni nyinyi muifue, hata akikataa lazimisheni kwa njia nzuri kuwa mama hata kama kuna mfanya kazi leo mimi nimetia nia ya kukuoshea nguo yao au zako.

 

  1. Nunueni kaseti, kanda za video, VCD au DVD za mawaidha. Na mwanzo anzeni mbali kwa mambo ya kwa mfano kufuata Qur-aan na Sunnah za Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘Alayhi wa aalihi wa sallam). Pia vitabu vya Kiislamu ambavyo vitamfundisha mengi kuhusu mambo ya Dini yake.

 

  1. Watumieni watu wa karibu kwenu mnaofahamiana nao na walio karibu na mama yenu, kwa mfano baba yenu mzazi, dada zake na kaka zake ili wazungumze naye ili kumuokoa na Moto.

 

  1. Muombeni Allaah Aliyetukuka sanasana katika nyakati du’aa hukubaliwa kama mnapoinuka usiku kwa ajili ya Swalaah ya Tahajjud, mnapokuwa mmefunga wakati wa kufungua, baina ya Adhana na Swalaah. Na Allaah Aliyetukuka ni mwenye kusikiliza du’aa.

 

Tuna yakini katika hayo mambo ambayo baadhi mkiyafanya basi kutapatikana natija iliyo mzuri kwa uwezo wa Allaah Aliyetukuka.

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

Share