Mume Amenitoa Katika Nyumba Sababu Kukataa Kulea Mtoto Aliyezaa Nje, Hanihudumi Lolote - Nikidai Talaka Je, Nitamdhulumu Mtoto?

SWALI:

 

Assalam aleikum, mimi ni mwanamke niliyeolewa na kuishi na mume wangu kwa mda wa miezi mitatu unusu, kwa mda huo mume wangu kanitoa nyumbani sababu nilikataa kuishi na mtoto wake wa haramu ambaye hakuniambia wakati anaponioa. Nilipotoka nilikuwa ni mja mzito mwezi moja. Mda wote huu wa uja uzito wangu hakuniangalia kwa lolote. Nimejifunguwa mtoto wa kike. Sasa naomba talaka lakini mume wangu hataki kunipa. Swali langu ni nimefanya makosa? Na mume akiwa anamtaka mkewe si humuangalia kwa hali na mali? Mume kama huyu aweza kweli kuniangalia kwa uzuri? Maana aliwahi hata kusema mimba si yake. Hivi sasa anaishi na mwanamke bila kmuoa. Na je namdhulumu binti yangu sababu ataleleka bila ya babake? Naomba minijibu maswali zangu. Shukran

 


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu mume kukutoa katika nyumba kwa sababu uliyoitaja hapo juu.

Hakika yapo makosa mengi ambayo yanapatikana katika kuingia katika ndoa au unyumba. Matatizo kama haya yanapatikana kwa wingi sana na wale wanaodhulumika ni wasichana au wanawake kwa sababu moja au nyingine. Na kwa kuwa sisi Waislamu tumekataa kufuata Sunnah ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) katika mas-ala ya ndoa huwa tunakumbana na matatizo na changamoto nyingi sana ambazo zinatupelekea katika matatizo ya kifamilia.

 

Tumekariri mara nyingi kuwa Muislamu anatakiwa kuingia katika ndoa kwa sababu ya Dini, maadili na tabia njema sio ukabila, nasaba, utajiri au uzuri. Maafa yanatokea kwa kuwa inapokuja posa wazazi au msichana mwenyewe huwa anataka kuingia katika ndoa bila kutaka kujua huyo mwanamme yuko vipi katika mas-ala ya Dini na maadili. Na lau kama kabla ya kukubali posa, wazazi na msichana mwenyewe wangetafuta maalumati kuhusu mwanamme huyo basi shida hizi zingepungua sana katika jamii zetu. Bila shaka katika uchunguzi huo mngekuja jua kuwa mwanamme mwenyewe hana maadili na pia ana mtoto wa nje ya ndoa. Kwa hivyo kabla ya kuingia katika ndoa ungeweza kuamua kuwa naye au la, na kama kuwa naye basi kuwe na mkataba baina yako na mwanamme kuhusu mahusiano yenu na mtoto huyo. Lakini hilo halikutazamwa kabisa limekuja kujulikana baadae kuonyesha kuwa mwanamme mwenyewe hana maadili mema. Bila shaka, huenda akawa mwanamme ameomba msamaha kutoka kwa Mola wake Mlezi na kujirekebisha na ikiwa ni hivyo hilo pia lingefahamika kwa yeye kujieleza na kueleza uhakika wake, lakini pia hilo halipo kutokana na maelezo yako kuwa hivi sasa anaishi na mwanamke nje ya ndoa.

 

Hata hivyo, hilo ni kosa ambalo tayari limefanyika na mmeshaingia katika unyumba, nawe ukafanya kosa kwa upande wako bila kujali maadili ya Dini au kwa kutojua kwa kukataa kuishi na mtoto ambaye si wake kisheria. Ilikuwa wakati huo baada ya kugundua hilo kukaa na mumeo na kulizungumzia suala hilo kwa njia iliyo nzuri ya upole na ulaini baina yako na yeye. Mke huwa ana mazoea na mumewe na anajua jinsi ya kuweza kumkinaisha na wakati wa kuzungumza naye. Ikiwa hukufanikiwa basi ilikuwa uende katika hatua ya pili ya upatanishi ambayo ilihitajia wewe uitishe kikao ambacho kitakujumuisha wewe, mumeo, mwakilishi wako na wa mumeo. Na ikiwa pia kwa kikao hicho hakukupatikana suluhisho aina yoyote basi ilikuwa ni wewe uende kwa Qaadhi ambaye ungemueleza shida unayoipata naye angekuwa ni mwenye kuhukumu na kumpatia haki mwenye haki hiyo.

 

Kadhalika yalikuwa ni makosa kwa mumeo kukutoa nyumbani kwa sababu yoyote ile ila tu kama angekupata na uasherati. Hata kama angekuwa amekupatia talaka basi ilikuwa eda yako upitishe katika nyumba hiyo. Hayo maelezo mengine yote uliyoeleza yakiwa ni kweli, basi yanaonyesha jinsi gani mumeo si mume wa sawasawa kwa mwanamke kukaa naye lakini hata hivyo inabidi ufuate njia za kisheria ili kujitoa katika unyumba kwa njia iliyo nzuri.

 

Katika maelezo yako inaonyesha kuwa mumeo kakutuhumu au kakusingizia uzinzi kwani anaposema kuwa huyo binti si wake ni kuwa ni wa mume mwengine. Na kwa hilo inabidi mulaaniane kwani yeye hana mashahidi wanne kwa shutuma hiyo. Na ikiwa mtafanya hivyo mtakuwa kisheria mmeachana. Kwa kadhiya hii yako itabidi sasa uende kwa Qaadhi ili umshitakie na bila shaka mtapata suluhisho kwa utata huo unaokutia katika fikra na matatizo makubwa. Ikiwa unaomba talaka wewe ndiye utakaehasirika kwa makosa ya mumeo. Njia iliyo bora ni kwako kwenda kwa Qaadhi na ikiwa sehemu uliyoko hakuna Qaadhi itabidi uende kwa Shaykh anayeaminika kwa ucha Mngu na usomi ili atatue hiyo kesi yenu. Ama kuhusu mtoto kwa kuwa yeye amemkataa atakua ni wako peke yako.

 

Nasaha yetu kwako ni kuwa ikiwa utaipata hiyo talaka, basi uwe makini sana inapokuja posa nyingine baada ya eda ili usiingie katika shida hiyo mara nyingine tena. Na kwa suala la kutaka talaka ni vyema uswali Swalah ya Istikhaarah.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share