Mkwe Mchawi, Mke Si Muaminifu, Nilimpa Talaka Lakini Amekwenda Mahakamani, Nifanyeje?

SWALI:

 

Asalaam alaykum warahmatullah wabarakatuh

 

Nimegundua mama mkwe wangu ni mchawi akishiriana na aliyekuwa mke wangu, mke wangu nilipomueleza kuhusu mama yake alikanusha nilifanya uchunguzi zaidi ya sehemu tata jibu lipo sawa, pia mke wangu alikuwa anitekelelezei unyumba vizuri na alikuwa akijiamini sana  ilifika mahali kila nikitaka unyumba inakuwa mzozo nikafanya uchunguzi nikagundua si muaminifu niliwahi kugundua alikuwa na mawasiliano na mtu kariakoo na alimtumia jirani yangu barua ili ifike kwa huyo mtu nilimrudisha kwao kisha nikamsamehe, nikawahi kupokea simu ya mtu katika simu yake ikidai kuwa kaka yake anaumwa siki hiyo hiyo nikaenda kazini kwa huyo anae daiwa anaumwa kumbe si kweli ila kwa sababu nilipokea mimi ile simu nikapotezwa lengo, nikaja kutumia namba ingine ya simu nikamwita gesti tena sikumtajia jina akaja hapo nikawa nimemaliza uchunguzi wangu lakini hata hivyo roho iliniuma sana sikutegemea kama angeendelea na hayo mambo ambayo yaliotokea toka mwaka 2000, 2004 hadi 2008 kumbe yaliendelea nikawa sina tena mapenzi nae hata hivyo akawa anazidi kuniudhi kwa maneno madogo madogo usafi wa nyumba shida tupu dharau nyingi ninacho agiza akitekelezwi nikimwambia anasema namyanyasa baada ya kunipoza hata nilipoeleza ktk baraza kwa wazee wake hakuna cha maana walichoeleza na kumkanya atimae nikampa talaka, na akaenda kwa wasimamizi wa Kiislamu ikaamuliwa nimpe pesa mutaa  tukakubaliana baadae kageuka kaenda mahakamani. Lengo lake aniaribie mali zangu ambazo ni urithi wa watoto ambao nilizaa nae wawili, je nilikosea  kumpa talaka? 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu talaka uliyoitoa kwa mkeo. Maneno haya tunayonakili sasa tumeyarudia mara nyingi sana katika matatizo ambayo yanakuja kwetu kuhusiana na mas-ala ya kinyumba na wanandoa.

Tatizo hili limekuwa sugu japokuwa ufumbuzi tayari tumepewa karne 14 zilizopita. Sasa kule kupuuza au kuzembea kwetu ndio tunapatikana na shida hizi kila mara. Kutokana na tatizo hili ni lazima tuamue kuwa sisi katika mas-ala ya kuoa ni lazima tufuate maagizo ya Allaah Aliyetukuka na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ili tuweze kufanikiwa kwa kiasi kikubwa katika hilo. Kwa sababu sisi hatutaki kufuata hayo ndio tunakumbwa na matatizo mengi kisha tunakuja kujuta baadaye na majuto hayo huwa hayafalii lolote wala chochote. Tumehimizwa sana tutafute mke mwenye Dini na maadili lakini tunaacha mwongozo huo na kufuata matamanio yetu kwa kufuata ima uzuri, nasaba au utajiri na hasara yake inakuwa kubwa.

 

Ama kuhusu uamuzi wako wa kumuacha ulikuwa sawa sawa japokuwa ulichelewa sana kuchukua uamuzi huo muafaka kabisa. Na lau kama ungeendelea kubaki naye basi ungeingia katika wanaume wenye kuitwa Dayuth kisheria. Dayuth ni mwanamme asiyejali kabisa mkewe anafanya nini, hajali hata akimuona na mwanamme mwingine. Na tufahamu kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kuwa Dayuth hataingia Peponi. Umesalimika na kunusurika kwa hilo.

 

Nasaha yetu kwako ni kuwa sasa ni wakati muafaka kwako kusahau yaliyopita na kutafuta mke mwingine kwa misingi ya sheria ya Kiislamu. Na tunamuomba Allaah Aliyetukuka Akupe tawfiki katika hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share